Siku ya V ya Maskini Duniani itaadhimishwa tarehe 14 Novemba 2021. Siku ya V ya Maskini Duniani itaadhimishwa tarehe 14 Novemba 2021. 

Siku ya V ya Maskini Duniani 14 Novemba 2021: Ufafanuzi wa Kina!

Maadhimisho ya Siku ya V ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2021 yananogeshwa na kauli mbiu “Maana siku zote mnao maskini pamoja nanyi” Mk 14:7. Hayo yanabainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wa Siku ya V ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2021 na kilele chake ni tarehe 14 Novemba 2021. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma ya Mungu kwa maskini na wanyonge.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Maskini Duniani ni changamoto inayotolewa na Mama Kanisa kwa Jumuiya ya Kimataifa, kusikiliza na kujibu kilio cha maskini wa nyakati hizi, wanaoendelea kuteseka sehemu mbali mbali za dunia. Siku ya Maskini Duniani ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, na kwa mara ya kwanza siku hii imeadhimishwa kunako mwaka 2017. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni kumbukumbu endelevu ya huruma ya Mungu inayopaswa kuwa ni: dira, mwongozo na sehemu ya vinasaba na utambulisho wa waamini katika ujumla wao. Siku hii ni fursa ya kushikamana kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana kwa hali na mali kama alama ya: urafiki, umoja na udugu wa kibinadamu unaovunjilia mbali kuta za utengano kwa sababu mbalimbali. Maadhimisho ya Siku ya V ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2021 yananogeshwa na kauli mbiu “Maana siku zote mnao maskini pamoja nanyi” Mk 14:7. Hayo yanabainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wa Siku ya V ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2021 na kilele chake ni tarehe 14 Novemba 2021.

Baba Mtakatifu anatoa ufafanuzi makini kuhusu sehemu hii ya Injili kama ufunuo wa Uso wa huruma ya Mungu kwa maskini. Maskini ni wadau muhimu sana katika mchakato wa uinjilishaji mpya na kwamba, Kristo Yesu alionesha upendeleo wa pekee sana kwa maskini. Huu ni mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu ili kutambua, kusikiliza na kujibu kilio cha maskini katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, anadokeza kuhusu mifumo mipya ya umaskini duniani inayopaswa kushughulikiwa kwa kutumia sera na mikakati mbalimbali itakayokuza na kudumisha uhuru, ukarimu sanjari na kusoma alama za nyakati. Maadhimisho ya Siku ya Maskini Duniani ni fursa makini ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Ni wakati wa kujifunza maisha ya maskini na kuwa tayari kuwajibu kwa moyo wa upendo na ukarimu. Lakini ikumbukwe kwamba, kila mtu ni maskini kadiri ya kiwango na hali yake.

Baba Mtakatifu Francisko aliwahi kusema kwamba, Kanisa daima limekuwa likisikiliza na kujibu kilio cha maskini na wahitaji kama inavyoshuhudiwa kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume, kwa kuwachagua Mashemasi saba walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho na hekima, ili waweze kutoa huduma kwa maskini. Hii ni alama ya kwanza ya huduma kwa maskini kutokana na utambuzi kwamba, maisha ya Kikristo yanafumbatwa katika udugu na mshikamano. Yesu mwenyewe aliwapatia maskini kipaumbele cha kwanza katika Heri za Mlimani kwa kusema, “Heri maskini, maana hao watairithi nchi”. Jumuiya ya kwanza ya Wakristo iliuza mali na vitu vyake na kuwagawia watu kadiri ya mahitaji yao! Kuna sababu lukuki zinazopelekea umaskini wa hali na kipato kuendelea kushamiri duniani, licha ya sera na mikakati mbalimbali inayowekwa na Jumuiya ya Kimataifa. Kuna athari za mabadiliko ya tabianchi, vita, ghasia na machafuko ya kijamii.

Kuna watu wanaofungwa na kutupwa magerezani bila kuhukumiwa na wengine wanapotea katika mazingira ya kutatanisha! Maskini ni watu wanaonyimwa uhuru na utu wao kusiginwa kama “soli ya kiatu”. Ni watu wanaoteseka kwa ujinga, maradhi, njaa, kiu, ukosefu wa fursa za ajira, mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo na biashara ya binadamu na viungo vyake.  Hawa ni watu wanaolazimika kuzikimbia nchi zao ili kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi kwa ajili yao binafsi pamoja na familia zao. Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya, Jumatatu tarehe 14 Juni 2021, amewasilisha ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Maadhimisho ya Siku ya V ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2021, yanayonogeshwa na kauli mbiu “Maana siku zote mnao maskini pamoja nanyi” Mk 14:7. Mwaliko kwa waamini kumwangalia Kristo Yesu katika maneno na matendo yake ili kufahamu maana halisi ya umaskini na hivyo kuwatambua maskini, tayari kusikiliza na kujibu kilio chao! Kumekuwepo na mifumo mbalimbali ya umaskini duniani na katika nyakati hizi, kumeibuka pia mifumo mipya ya umaskini katika ulimwengu mamboleo.

Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limeendelea kuwa ni sababu mateso, mahangaiko na vifo kwa watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia. UVIKO-19 umepelekea kusuasua kwa huduma kwa maskini kwa watu kuhofia usalama wa maisha yao. Waamini wafuate mfano bora wa Mtakatifu Padre Damian wa Moloka’i: “Saint Damien de Veuster of Moloka’i” aliyeishi kati ya Mwaka 1840 – 1889 na hatimaye kutangazwa kuwa Mtakatifu na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI tarehe 11 Oktoba 2009. Ni Padre mmisionari aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wakoma, akawa kweli ni chemchemi ya furaha na matumaini; shuhuda na chombo makini cha uinjilishaji, leo hii Kanisa linamtambua na kumheshimu kama Mtume wa wagonjwa wa Ukoma. Padre Damian wa Moloka’i awe ni mfano bora wa kuigwa hata katika nyakati hizi za maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kamwe watu wasiwageuzie kisogo maskini, kwani sababu hawa ni ndugu zao wanaohitaji huduma, upendo na faraja!

Wanawake na wasichana wanapaswa kuangaliwa kwa umakini zaidi, kwa sababu ni watu wanaobaguliwa na kudhalilishwa utu, heshima na haki zao msingi. Bado wanaendelea kuathirika na mfumo dume katika uongozi, lakini wanawake wanao mchango mkubwa katika historia ya ukombozi. Huu ni mwaliko kwa waamini kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kwa kuwathamini na kuwajali maskini si katika maelekeo ya Yuda Iskarioti. Bali maskini ambao wanakuwa ni chachu ya toba, wongofu na utakatifu wa maisha. Ni changamoto ya kufanya mabadiliko katika uchumi kwa kujikita katika uchumi ambao unatoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi; utu, heshima yake kama binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu anawataka viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuzingatia kanuni maadili na utu wema, ili kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano, ili kukuza na kudumisha demokrasia shirikishi. Umaskini si nadharia au wazo linaloelea katika ombwe, bali ni hali halisi inayowakumba mamilioni ya watu sehemu mbalimbali za dunia.

Huu ni mwaliko wa kuondokana na uchoyo pamoja na ubinafsi tayari kujikita katika mchakato mfumo mpya wa maendeleo shirikishi kwa kujenga na kudumisha madaraja yanayowakutanisha watu ili kusaidiana na kukamilishana kama binadamu. Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella anasema, Maadhimisho ya Siku ya V ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2021 yatanogeshwa na matendo ya huruma kiroho na kimwili, kama kielelezo na ushuhuda wa Injili ya huruma na mapendo kwa maskini. Yawe ni maadhimisho yanayokita mizizi yake katika umoja, udugu na mshikamano wa kibinadamu. Kumbe, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanapaswa kuhamasishwa ili waweze kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya ambayo yanapaswa kuacha alama ya kudumu katika maisha ya maskini na utume wa Kanisa katika ujumla wake. Maskini wanapaswa kukumbatiwa na kuhudumiwa na wala si kuhesabiwa!

Maskini Duniani 2021
14 June 2021, 15:31