Tafuta

Papa Francisko Imani kwa Kristo Yesu Ijenge Mahusiano ya Dhati

Papa Francisko asema: Imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake ni msingi wa maisha ya Kikristo. Imani hii inawawezesha waamini kujenga umoja na mahusiano ya dhati, hatua kubwa katika maisha ya Kikristo. Waamini wanapaswa kutoa majibu ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa, majibu yanayobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo zao! Imani inapaswa kumwilishwa katika ushuhuda.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kristo Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipo, akawauliza wanafunzi wake “Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?’’ Ndilo swali la kwanza. Lakini lililokuwa gumu zaidi ni lile la pili; ‘’Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?’’.  Jibu la swali lile la kwanza halikuwa gumu kwa Mitume wa Yesu kwa sababu wao hawakuwa wahusika wakuu au walengwa wa swali lile na badala yake wao walikuwa ni wawakilishi tu wa majibu na mitazamo ya watu wengine. Na jibu lao linaonesha jinsi walivyomwona Yesu kama mtu mashuhuri kama Yohane Mbatizaji, Eliya, Yeremia au mmojawapo wa manabii wa kale. Kristo Yesu “Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. “Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu’’. Kristo Yesu akamtambulisha kama Petro yaani “Mwamba” ‘’Πετρος’’, (Petros). Rej. Mt 16: 15-17.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume, Jumanne, tarehe 29 Juni 2021, amesema kwamba, Kristo Yesu aliamua kufanya maswali dodoso kwa Mitume wake ili kuweza kupata maoni yao kumhusu Yeye. Imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake ni msingi wa maisha ya Kikristo. Imani hii inawawezesha waamini kujenga umoja na mahusiano ya dhati, hatua kubwa katika maisha ya Kikristo. Waamini wanapaswa kutoa majibu ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa, majibu yanayobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo zao! Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kristo Yesu anapaswa kuwa ni kiini cha mawazo, kiasi cha kuwa ni rejea ya mahusiano na mafungamano ya kijamii, kwa kuhakikisha kwamba, Kristo Yesu anakuwa ni upendo wa maisha ya waamini wake! Watakatifu Petro na Paulo Mitume katika maisha yao wamevutwa na hatimaye, wakamwiga Kristo Yesu katika maisha na utume, kiasi cha kuwa ni wadau wakuu wa Habari Njema ya Wokovu na wala hawakubaki kuwa ni watazamaji tu! Hawa ni Mitume walioamini kwa dhati na imani yao wakaimwilisha katika matendo; Mtume Petro akawa ni mvuvi wa watu.

Mtakatifu Paulo, Mtume ni mwandishi wa Nyaraka za maisha na utume wake kwa watu wa Mataifa. Akasafiri huku akitangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Miamba hii ya imani, ikayamimina maisha kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Wakawa waaminifu kwa Injili na Kanisa la Kristo Yesu. Kanisa linapaswa kuwa aminifu kwa Kristo Yesu kwa kuwa karibu zaidi na waamini kwa njia ya ushuhuda wa kinabii na kimisionari. Hii ni changamoto ya kumwilisha yote haya katika matendo badala ya kulalama na kuwalalamikia wengine. Mwenyezi Mungu anapaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa njia ya matendo yenye mvuto na mashiko! Watakatifu Petro na Paulo ni mifano bora ya kuigwa na watu wa Mungu katika ujumla wa maisha yao. Wamekuwa ni watakatifu kwa neema na nguvu ya Kimungu iliyokuwa ikitenda kazi ndani mwao. Wameonesha udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu kama inavyoshuhudiwa katika Injili Takatifu. Mtakatifu Petro anaonesha udhaifu na nguvu ya Mungu inayotenda kazi ndani mwake. Mtakatifu Paulo Mtume, katika Nyaraka zake mbalimbali anaandika makosa na mapungufu yake ya kibinadamu.

Hawa ni mashuhuda wa ukweli wa maisha, wakapambana na udhaifu na mapungufu yao kwa neema na baraka ya Mungu, leo hii wamekuwa kama walivyo! Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini maswali dodoso yaliyotolewa na Kristo Yesu kwa Mitume wake hata wao leo hii wanaulizwa swali la msingi. Je, Kristo Yesu ni nani kwako? Leo hii wahakikishe kwamba, Kristo Yesu anakuwa ni kiini cha maisha ya waamini wake kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa awasaidie waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda amini wa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Kiri ya Imani
29 June 2021, 15:04

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >