Tafuta

Vatican News
Papa Francisko Ekaristi Takatifu ni Sakramenti kuu, Sadaka ya sifa na shukrani ambayo waamini wanapaswa kushirikishana katika hija ya maisha yao! Papa Francisko Ekaristi Takatifu ni Sakramenti kuu, Sadaka ya sifa na shukrani ambayo waamini wanapaswa kushirikishana katika hija ya maisha yao!  (ANSA)

Papa: Ekaristi ni Sakramenti ya Wadhambi na Wanyonge

Kristo Yesu Mwishoni mwa maisha na utume anajitoa mwenyewe kwa wafuasi wake kuwa ni sadaka ya Pasaka. Hatima ya maisha ya mwanadamu ni kujitoa sadaka kwa ajili ya huduma ya upendo. Ukuu na utukufu wa Mungu unajionesha katika Mkate uliomegwa, katika hali ya udhaifu na unyonge unaobubujika upendo wa Mungu ambao waamini wanapaswa kushirikishana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa tarehe 6 Juni 2021 ameadhimisha Sherehe ya Mwili na Damu Azizi ya Bwana Wetu Yesu Kristo, “Corpus Domini”. Ni Sherehe inayowarejesha tena waamini Siku ya Alhamisi Kuu, Mama Kanisa alipokuwa anakumbuka Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Kristo Yesu, alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, yaani Mwili na Damu yake Azizi, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. “Nao walipokuwa wakila, alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa, akasema, Twaeni; huu ndio mwili wangu. Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa; wakakinywea wote. Akawaambia, Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi. Amin, nawaambia ninyi, Sitakunywa tena kabisa uzao wa mzabibu, hata siku ile nitakapounywa mpya katika ufalme wa Mungu.” Mk 22-25. Hii ni Sakramenti ya Sadaka: Shukrani, sifa na utukufu kwa Baba wa milele. Ni Kumbukumbu endelevu ya mateso yaletayo wokovu na ni sadaka ya uwepo wa Kristo kwa Neno na Roho wake Mtakatifu. Mama Kanisa anakumbuka pia Siku Yesu alipoweka Sakramenti ya Daraja Takatifu kwa kuwateuwa baadhi ya waamini na kuwaweka wakfu kwa ajili ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Hawa ni Makuhani waoliopewa dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, katika Nafsi ya Kristo Yesu ambaye ni kichwa cha Fumbo la Mwili wake, yaani, Kanisa lake! Hii ni Siku ambayo Kristo Yesu alikazia huduma ya upendo kwa kuwaosha Mitume wake miguu, kielelezo cha upendo unaonafsishwa katika huduma kwa watu wa Mungu!

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Sherehe ya Mwili na Damu Azizi ya Bwana Wetu Yesu Kristo, “Corpus Domini” kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amesema kwamba, Kristo Yesu kwa maneno na matendo yake, amewaachia waamini Sakramenti kuu, Sadaka ya sifa, ili kuweza kushirikishana. Mwishoni mwa maisha na utume wake hapa duniani, anajitoa mwenyewe kwa wafuasi wake kuwa ni sadaka ya Pasaka. Hatima ya maisha ya mwanadamu ni kujitoa sadaka kwa ajili ya huduma ya upendo. Ukuu na utukufu wa Mungu unajionesha katika kipande cha Mkate uliomegwa, katika hali ya udhaifu na unyonge unaobubujika upendo wa Mungu ambao waamini wanapaswa kushirikishana. Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni Mkate unaomegwa kielelezo cha nguvu ya upendo inayopaswa kupokelewa kwa mikono miwili, tayari kujisadaka kwa ajili ya wengine, ili waweze kupata maisha mapya; nguvu ya upendo inayowaunganisha waamini. Ekaristi Takatifu ni nguvu inayowahamasisha waamini kuwapenda wale wanaokosea. Usiku ule uliotangulia kuteswa kwake, Kristo Yesu aliwapatia wafuasi wake Mkate wa maisha ya uzima wa milele. Hii ni zawadi ya hali ya juu kabisa kutoka katika sakafu ya Moyo wake Mtakatifu. Anakula na Mtume wake ambaye atamsaliti. Hakuna uchungu mkubwa kama kusalitiwa na mtu unayempenda.

Yuda Iskariote “akatupilia mbali huruma na upendo wa Kristo Yesu katika maisha yake, lakini Yesu akamkirimia upendo wenye huruma. Hivi ndivyo anavyotenda Kristo Yesu katika maisha. Kwa wadhambi anawapatia nafasi ya kutubu na kumwongokea Mungu ili aweze kuwakirimia maisha ya uzima wa milele. Waamini wanapopokea Ekaristi Takatifu kwa ibada na uchaji, Kristo Yesu anawakumbusha kwamba, anawafahamu jinsi walivyo wa dhambi na kwamba, “kuteleza na kuanguka katika dhambi na udhaifu wa moyo” ni jambo la kawaida, lakini hata hivyo Kristo Yesu bado anathubutu kuunganisha maisha yake na maisha ya waamini wake. Fumbo la Ekaristi Takatifu si nishani ya watakatifu, bali ni Mkate wa Wadhambi, ndiyo maana wote wanaalikwa Kristo Yesu anaposema “Twaeni, mle wote: huu ndio mwili wangu utakaotolewa kwa ajili yenu… Twaeni, mnywe wote: hiki ni kikombe cha Damu yangu, Damu ya Agano Jipya na la milele, itakayomwagika kwa ajili yenu na kwa ajili ya wote kwa maondoleo ya dhambi”. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, kila mara waamini wanaposhiriki Mkate wa maisha ya uzima wa milele, Kristo Yesu mwenyewe anakuja na kupyaisha hali yao ya udhaifu na unyonge.

Hii ni kwa sababu, wanapendeka mbele ya Mwenyezi Mungu na kwamba, anafarijika sana, ikiwa kama Kristo Yesu mwenyewe anashiriki kikamilifu kuwainua kutoka katika udhaifu wao kwa upendo wake wenye huruma. Anawaganga, anawaponya na kuwatakasa kwa nguvu yake ya upendo, changamoto na mwaliko wa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu. Waamini wanapoponywa na kutakaswa, wawe ni chachu ya umoja na mshikamano unaowakirimia amani na utulivu wa ndani. Mkate wa maisha ya uzima wa milele unaganga na kuponya ugumu wa nyoyo za watu na kuwageuza kuwa ni wanyenyekevu. Ekaristi Takatifu ni dawa inayowawezesha waamini kuishi katika ukweli na uwazi. Ni Sakramenti inayoponya na kuwaunganisha waamini na Kristo Yesu, tayari hata waamini kujisadaka, kujitosa na kujimega kwa ajili ya upendo kwa jirani kwa kutenda wema dhidi ya ubaya wa moyo! Ni Sakramenti inayowapatia ujasiri wa kutoka katika ubinafsi wao, tayari kuwahudumia jirani zao kwa upendo mkamilifu, kama anavyotenda Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Hii ndiyo mantiki ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwamba, waamini wanampokea Kristo Yesu katika maisha yao kwa sababu anawapenda upeo na anaganga na kutakasa udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu, ili waamini wakisha kutakasika wao wawe pia mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao.

Kristo Yesu kwa kuzaliwa wake, amekuwa ni mwandani wa safari ya maisha ya mwanadamu. Katika Ekaristi Takatifu amekuwa ni chakula na kinywaji cha roho. Kwa mateso na kifo chake Msalabani, amewakomboa watu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kwa sasa atawala mbinguni, mwaliko kwa waamini kumwendea mbinguni huko aliko, ili waweze kushiriki maisha ya uzima wa milele. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko amesema, Kristo Yesu kwa njia ya Roho Mtakatifu amefanyika mwili, kwake yeye Bikira Maria, awasaidie waamini kupokea Ekaristi Takatifu kwa ibada na uchaji, tayari kujisadaka, kujitosa na kujimega kama sadaka safi kwa jirani zao!

Papa Sakramenti Kuu

 

 

06 June 2021, 16:10

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >