Papa Francisko: ROACO ni chombo cha huduma na uinjilishaji wa kina unaozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili Papa Francisko: ROACO ni chombo cha huduma na uinjilishaji wa kina unaozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili 

Papa Francisko ROACO Chombo cha Huduma na Uinjilishaji!

Papa Francisko tarehe 24 Juni 2021 amekutana na kuzungumza na Wajumbe wa ROACO. Katika hotuba yake, amegusia hija yake ya Kitume nchini Iraq, mateso na mahangaiko ya Watu wa Mungu nchini Lebanon, Mchango wa Ijumaa kuu; wawakilishi wa Vatican kwenye mkutano wa ROACO pamoja na mgogoro wa Ethiopia ambao athari zake pia zinaanza kujionesha nchini Eritrea. ROACO!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO, (R.O.A.C.O. Riunione Opere Aiuto Chiese Orientali), kuanzia tarehe 21- 24 Juni 2021 limekuwa likiadhimisha Mkutano wake wa 94. Hiki ni kipindi cha kusali na kuwaombea wafadhili wa ROACO ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia huduma mbalimbali zinazotolewa na ROACO kwa Makanisa ya Mashariki. Ni nafasi pia kwa ajili ya kuendelea kumlilia Mwenyezi Mungu ili aweze kuingilia kati na kuwakirimia waja wake amani, utulivu wa kisiasa, kijamii na kidini; mambo ambayo pia yamechangiwa kwa kiasi kikubwa kwa kuenea kwa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Wajumbe wa ROACO pamoja na mambo mengine, wamekuwa wakijadili kwa kina na mapana hali ya Nchi Takatifu, kwa kuwasikiliza viongozi wakuu wa Makanisa mjini Yerusalemu. Wajumbe wamepata fursa ya kujadili kuhusu Sadaka na Mchango wa Ijumaa kuu kwa ajili ya Nchi Takatifu: "Pro Terra Sancta" kwa Mwaka 2021 pamoja na hali ya Makanisa mahalia ambayo yako chini ya Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki.

Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 24 Juni 2021 amekutana na kuzungumza na Wajumbe wa ROACO. Katika hotuba yake, amegusia hija yake ya Kitume nchini Iraq, mateso na mahangaiko ya Watu wa Mungu nchini Lebanon, Mchango wa Ijumaa kuu; wawakilishi wa Vatican kwenye mkutano wa ROACO pamoja na mgogoro wa Ethiopia ambao athari zake pia zinaanza kujionesha nchini Eritrea. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq, kuanzia Ijumaa tarehe 5 hadi Jumatatu tarehe 8 Machi 2021 ilinogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Hija hii ilifumbata mambo makuu matatu: Ukaribu wa Baba Mtakatifu kwa Wakristo nchini Iraq, kuhamasisha ujenzi wa Iraq mpya katika haki na usawa na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene ili kudumisha udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu aliyemwezesha kutekeleza hija inayopania ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Tangu mwaka 2019, Baba Mtakatifu alitia nia ya kutembelea nchini Iraq na anawashukuru wajumbe wa ROACO kwa kazi kubwa wanayotekeleza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, licha ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ROACO katika miaka ya hivi karibuni imepata nafasi ya kujadili kuhusu hali ya Eritrea na Lebanon. Mlipuko uliotokea kwenye eneo la bandari ya Beirut, tarehe 4 Agosti 2020 ulisababisha watu zaidi ya 150 kupoteza maisha na wengine 5, 000 kujeruhiwa vibaya na watu 3, 000 kukosa makazi baada ya nyumba zao kuharibiwa vibaya na mlipuko huo. Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe wa ROACO kuwakumbuka na kuwaombea watu wa Mungu nchini Lebanon. Baba Mtakatifu ametia nia ya kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Jumuiya za Kikristo nchini Lebanon hapo tarehe 1 Julai 2021. Mkutano huu unatarajiwa kufanyika mjini Vatican, ili kutafakari kuhusu matatizo, changamoto na fursa wanazokabiliana nazo watu wa Mungu nchini Lebanon katika kipindi hiki. Itakuwa ni siku ya sala, ili kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia waja wake amani na utulivu.

Tangu sasa, Baba Mtakatifu anapenda kuwaweka watu wote wa Mungu nchini Lebanon chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu anayeheshimiwa kwenye Madhabahu ya Harissa nchini Lebanon. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza kwa sadaka na sala zao za mshikamano, tangu wakati huu wa maandalizi na hatimaye, siku yenyewe, ili Lebanon iweze kupata amani, utulivu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza watu wa Mungu wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuchangia gharama za miradi inayotekelezwa na ROACO, kielelezo makini cha umoja na udugu wa kibinadamu. Mtakatifu Paulo VI, kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, alitembelea Nchi Takatifu mwezi Januari 1964 na kuguswa na mahitaji ya Wakristo. Katika Wosia wake wa Kitume “Nobis in animo” yaani “Umuhimu wa Kanisa katika Nchi Takatifu” uliochapishwa tarehe 25 Machi 1974, alikazia umoja na mshikamano wa waamini. Huo ukawa ni chimbuko la Sadaka na mchango wa Ijumaa kuu kwa ajili ya Nchi Takatifu: "Pro Terra Sancta".  Mtakatifu Paulo VI alihimiza sana umuhimu wa uwepo endelevu wa Kanisa katika Nchi Takatifu, kama amana na urithi wa imani; ushuhuda endelevu wa Jumuiya ya Wakristo unaoonesha jiografia ya ukombozi.

Tangu wakati huo, Kanisa linaendelea kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanaoteseka kunyanyaswa na hata kuuwawa huko Mashariki ya Kati, lakini hasa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Sadaka na mchango wa Ijumaa kuu kutoka kwa Makanisa yote duniani, ni alama ya upendo na mshikamano wa Kanisa kwa watu wa Mungu wanaoishi katika Nchi Takatifu. Huu ni ushuhuda wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika uekumene wa damu, huduma na sala pamoja na kuendeleza majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu katika misingi ya: haki, amani na maridhiano. Baba Mtakatifu anasema, ameambiwa kwamba, Sadaka na Mchango wa Ijumaa kuu kwa Mwaka 2020 ulipungua sana ikilinganishwa na miaka mingine iliyopita. Haya ni matokeo ya UVIKO-19 sanjari na uyumba kwa uchumi wa kitaifa na kimataifa. Jambo la msingi ni kuzama kwa mambo msingi zaidi, ili kukoleza mshikamano wa Kanisa na Nchi Takatifu uliopewa kipaumbele cha pekee na Mtakatifu Paulo VI.

Mkutano wa ROACO imekuwa ni fursa ya kufanya upembuzi wa kina kuhusu hali ya Nchi Takatifu, uhusiano kati ya Israeli na Palestina. Watu wa Mungu wanatamani kuona amani ikitawala tena badala ya vita inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Mabalozi wa Vatican kutoka Lebanon, Iraq, Ethiopia, Armenia na Georgia ni kielelezo muhimu sana cha Kanisa kuendelea kujikita katika mambo msingi ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Uwepo wa ROACO ni ushuhuda wa Umama wa Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni vyema kujenga na kukarabati miundo mbinu, lakini jambo la msingi ni kujihusisha zaidi na mahitaji msingi ya watu wa Mungu ambao ni mawe hai, ambao wameathirika sana kutokana na vita; wamejeruhiwa na kusambaratishwa. Baba Mtakatifu anasema anafuatilia kwa umakini mkubwa mgogoro wa kivita nchini Ethiopia ambao unaathari zake nchini Eritrea. Haya ni matokeo ya uchu wa mali, madaraka na mafanikio ya chapuchapu. Kuna haja ya kukuza na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu. Hija ya yake ya kitume nchini Armenia kunako mwaka 2016 inaanza kuzaa matunda ya amani katika neo zima Caucasus. Kanisa litaendelea kuwa ni alama ya amani, matumaini kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Georgia na Armenia, mwaliko kwa wanajumuiya ya Wakatoliki kuwa ni chachu ya maisha ya Kiinjili.

Papa ROACO 2021

 

24 June 2021, 16:01