Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu woye wenye mapenzi mema kusimama na kusali kwa dakika moja tarehe 8 Juni 2021 ili kuombea amani Myanmar na Nchi Takatifu Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu woye wenye mapenzi mema kusimama na kusali kwa dakika moja tarehe 8 Juni 2021 ili kuombea amani Myanmar na Nchi Takatifu 

Papa Francisko Mwaliko wa Kuombea Amani: 8 Juni 2021

Papa Francisko: Jumanne, tarehe 8 Juni 2021, majira ya Saa 7: 00 mchana, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaalikwa kusimama walau kwa dakika moja na kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani. Kwa namna ya pekee kabisa, sala kwa Mwaka 2021 inawalenga watu wa Mungu wanaoishi katika Nchi Takatifu na huko Myanmar ambako kuna machafuko ya kisiasa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Amani inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru kamili mambo msingi yanayofafanuliwa katika Waraka wa Kitume wa Mtakatifu Yohane XIII “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani”. Amani ni msingi wa wema, heshima na maendeleo fungamani ya binadamu. Ni paji na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha na kumwajibisha binadamu. Amani ni tunda la upendo linalopaswa kuboreshwa kwa njia ya malezi ya dhamiri nyofu; ukweli na uhuru; usalama wa raia na mali zao; kwa kulinda na kuheshimu utu wa binadamu, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi.  Kwa ufupi, amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo! Amani inatishiwa sana na mashindano ya silaha duniani; utengenezaji na biashara ya silaha pamoja na mchakato wa ulimbikizaji wa silaha duniani! Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani duniani! Tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Kanisa limeendelea kuandika na kushuhudia Injili ya amani inayofumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika tunu msingi za Kiinjili yaani: haki, upendo, utu na heshima ya binadamu. Hii ni misingi inayopambana na vitendo vyote vya kigaidi, vita na machafuko ya aina mbali mbali ambayo kimsingi ni kashfa kubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Jumuiya ya Kimataifa anasema Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, haina budi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani dhidi ya ubinafsi, uchoyo na uchu wa utajiri wa haraka haraka unaonuka damu ya watu wasiokuwa na hatia! Kutafuta amani na kuidumisha ni kitendo cha kishujaa na ushupavu wa hali ya juu kabisa. Ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na kumwilishwa katika maisha ya kila siku. Nguvu ya imani, itawale zaidi kuliko silaha zinazosababisha maafa kwa watu na mali zao; nguvu ya majadiliano katika ukweli na uwazi, ipewe kipaumbele cha kwanza, kuliko kupimana nguvu kwani katika vita hakuna mtu anayeweza kujigamba kwamba, ameshinda! Nguvu ya kimaadili ipewe nafasi ya kwanza badala ya utawala wa mabavu! Hiki ni kipindi muafaka cha kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha amani duniani, kwa ujasiri na ushupavu; kwa kukazia umuhimu wa amani kama kikolezo kikuu cha maendeleo fungamani ya binadamu, ili kuondokana na vita inayosababisha maafa kwa watu wasiokuwa na hatia!

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuungana na Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC pamoja na Jukwaa la Umoja wa Vijana Wakatoliki Kimataifa, FIAC, kwa kushirikiana na wadau mbali mbali kuwaalikaa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kushirikiana na kushikamana ili kuombea amani duniani. Baba Mtakatifu wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 6 Juni 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatfu Petro mjini Vatican amesema Jumanne, tarehe 8 Juni 2021, majira ya Saa 7: 00 mchana, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaalikwa kusimama walau kwa dakika moja na kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani. Kwa namna ya pekee kabisa, sala kwa Mwaka 2021 inawalenga watu wa Mungu wanaoishi katika Nchi Takatifu na huko Myanmar ambako kuna machafuko ya kisiasa yanayoendelea. Huu ni mwaliko wa kushinda kishawishi cha kutaka kutumia vita kama suluhu ya migogoro, mipasuko na machafuko yanayoendelea kujitokeza katika uso wa dunia.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana pamoja naye kwa ajili ya kusali na kuombea amani katika Nchi Takatifu. Bado anakumbuka lile tukio la tarehe 8 Juni 2014 alipokutana na kusali pamoja na Patriaki Bartolomeo wa kwanza, Hayati Rais Shimon Peres wa Israeli pamoja na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina ili kuombea amani huko Mashariki ya Kati! Baba Mtakatifu anasema baadhi ya watu wanaweza kufikiri kwamba, mkutano ule wa sala haukuwa na mafanikio yoyote, lakini hii si kweli, kwani Sala inawasaidia waamini kutokatishwa tamaa na hivyo kushindwa na ubaya, wala matumizi ya nguvu kushika hatamu; badala ya majadiliano na upatanisho. Baba Mtakatifu anawaalika wadau mbali mbali kuongeza juhudi zao katika kukomesha uadui na chuki kati ya watu, ili amani, ustawi na mafao ya wengi yaweze kushika mkondo wake.

Kuombea Amani

 

06 June 2021, 15:43