Papa Francisko Mfano wa Punje ya Haradali: Ukuaji wa Ufalme wa Mungu: Matumaini kwa Mwenyezi Mungu. Papa Francisko Mfano wa Punje ya Haradali: Ukuaji wa Ufalme wa Mungu: Matumaini kwa Mwenyezi Mungu. 

Mfano wa Punje ya Haradali: Ukuaji wa Ufalme wa Mbinguni: Matumaini!

Mungu anatenda kama mbegu ndogo ya haradali, katika udogo na ukimya wake, inakuwa na kukomaa polepole pasi na mashaka na hatimaye, unakuwa ni mti mkubwa chemchemi na asili ya maisha kwa viumbe vyote. Hata mbegu ya matendo adili yanayotekelezwa na binadamu yanapata asili na chanzo chake kutoka kwa Mwenyezi Mungu na yatazaa matunda kwa wakati wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kuhusu Mfano wa Punje ya Haradali. Kristo Yesu akasema, “Tuulinganishe na nini ufalme wa Mungu? Au tuutie katika mfano gani? Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake.” Kristo Yesu anaulinganisha Ufalme wa Mungu unaoishi katika sakafu ya mambo yote ya dunia kuwa ni kama punje ya haradali, yaani mbegu ndogo kuliko zote duniani. Lakini inapopandwa duniani inakuwa na kukomaa, kiasi cha kuwa ni mti mkubwa kuliko yote. Hivi ndivyo inavyotenda hekima ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Katika “maisha, shughuli na harakati mbalimbali kiasi hata cha nguo kuchanika”, bado Mwenyezi Mungu anaongoza historia ya maisha ya mwanadamu na ulimwengu katika ujumla wake. Mwenyezi Mungu anatenda kama mbegu ndogo ya haradali, katika udogo na ukimya wake, inakuwa na kukomaa polepole pasi na mashaka na hatimaye, unakuwa ni mti mkubwa chemchemi na asili ya maisha kwa viumbe vyote.

Hata mbegu ya matendo mema na adili yanayotekelezwa na binadamu yanapata asili na chanzo chake kutoka kwa Mwenyezi Mungu na yatazaa matunda kwa wakati wake. Jambo la msingi ni kukumbuka kwamba, matendo haya yanakuwa taratibu na katika hali ya unyenyekevu na kificho na hata wakati mwingine hayaonekani! Walatin wanasema, “Semen nostrorum bonorum operum parvi potest videri; omne tamen bonum Dei est et igitur fructum fert humiliter, lente. Bonum semper crescit humiliter, abdite, saepe occulte” Hii ni sehemu ya tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya Kumi na Moja ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 13 Juni 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Lengo kuu la Kristo Yesu katika mfano huu ni kuimarisha imani ya waja wake, ili katika maisha kamwe wasikate wala kukatishwa tamaa. Wanapoelemewa na udhaifu wa kibinadamu au kuelekea kushindwa na nguvu za dhambi na ubaya wa moyo, wakumbuke kwamba, Mwenyezi Mungu bado anatenda kazi zake hata katika hali ya ukimya! Kamwe wasibweteke na kuanza kulalama, bali wapige moyo konde na kujizatiti katika mapambano na matunda yatapatikana kwa wakati.

Tunu msingi za Kiinjili zinawahamasisha waamini kujiangalia na kuangalia mambo ya ulimwengu huu kwa jicho pana zaidi ili kugundua uwepo wa Mungu unaojifunua kama upendo mnyenyekevu unaotekeleza wajibu wake katika maisha ya waamini na katika historia kwa ujumla wake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ndiyo imani na nguvu inayowapatia “jeuri ya kusonga mbele” kila kukicha, kwa unyenyekevu, huku wakiendelea kupandikiza wema na uzuri utakaozaa matunda kwa wakati wake. Huu ni mwelekeo muafaka unaoweza kuwasaidia watu wa Mungu kuondokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambalo limesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, kiasi cha kuwakatisha watu tamaa ya maisha! Watu wa Mungu wajenge imani na kujizamisha katika ulinzi na tunza bora ya Mwenyezi Mungu. Lakini wakati huo huo, watu wenyewe waendelee kuchakarika usiku na mchana, ili kuanza ujenzi mpya katika uvumilivu na udumifu. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, hata Kanisa linaweza kujikuta limezongwa na “magugu ya kuwa na imani haba kutokana na mgogoro wa imani sanjari na kushindwa kwa utekelezaji wa miradi, sera na mipango mbalimbali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na jamii katika ujumla wake!

Lakini ikumbukwe kwamba, matunda ya shughuli zote za upandaji wa mbegu ardhini si juhudi binafsi zinazotekelezwa na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, bali hii ni kazi ya Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anawataka waamini kupandikiza mbegu hii kwa upendo, kwa kuwajibika na kwa uvumilivu zaidi, daima wakitambua kwamba, nguvu tendaji inatoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni mbegu inayoota yenyewe kama Kristo Yesu anavyokaza kusema “Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi; akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye. Maana nchi huzaa yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke. Hata matunda yakiiva, mara atapeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika. Mbele ya Mwenyezi Mungu hata ardhi kame kiasi gani, daima kuna matumaini ya maisha mapya. Bikira Maria, Mtumishi wa Bwana, awasaidie waamini kujifunza kuona ukuu wa Mungu katika kazi ya Uuumbaji inayojionesha hata katika mambo madogo madogo, ili kuvuka na kushinda kishawishi cha kukata na kujikatia tamaa, ili hatimaye, kujiaminisha mbele ya Mungu kila kukicha!

Ufalme wa Mungu
13 June 2021, 15:08

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >