Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu 2021 anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu na hatimaye, maandamano na Baraka ya Sakramenti kuu. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu 2021 anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu na hatimaye, maandamano na Baraka ya Sakramenti kuu. 

Papa Francisko Kuongoza Sherehe ya Ekaristi Takatifu Mjini Vatican

Fumbo la Ekaristi Takatifu ndio jumla na muhtasari wa imani ya Kanisa. Kumbe, namna ya waamini kufikiri hulingana na Fumbo la Ekaristi Takatifu na Ekaristi kwa zamu yake huimarisha namna yao ya kufikiri. Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 6 Juni 2021 majira ya 11: 30 za jioni, anatarajia kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, Ekaristi Takatifu ni chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo. Sakramenti nyingine, kama zilivyo pia huduma zote za Kanisa na kazi za utume, zinaungana na Ekaristi Takatifu na zinaelekezwa kwake. Kwani katika Fumbo la Ekaristi Takatifu mna kila hazina ya maisha ya kiroho ya Kanisa, yaani Kristo Yesu mwenyewe, Mwanakondoo wa Pasaka. Ekaristi Takatifu ndio ishara thabiti na sababu ya hali ya juu kabisa ya ushirika katika uzima wa kimungu na umoja ule wa Taifa la Mungu ambalo unalifanya Kanisa liwepo. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kilele cha tendo la Mungu la kuutakatifuza ulimwengu katika Kristo Yesu na kilele cha tendo la kumwabudu Mwenyezi Mungu wampalo watu Kristo Yesu, na kwa njia yake wampalo Baba katika Roho Mtakatifu.

Mababa wa Kanisa wanaendelea kusema kwamba, mwishowe, kwa njia ya adhimisho la Ekaristi Takatifu, waamini wanaungana tayari wao wenyewe na Liturujia ya mbinguni na wanaanza kutangulia kushiriki uzima wa milele Mungu atakapokuwa yote katika wote! Kwa ufupi kabisa, Fumbo la Ekaristi Takatifu ndio jumla na muhtasari wa imani ya Kanisa. Kumbe, namna ya waamini kufikiri hulingana na Fumbo la Ekaristi Takatifu na Ekaristi kwa zamu yake huimarisha namna yao ya kufikiri. Rej. KKK 1324 – 1327. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu, Jumapili tarehe 6 Juni 2021 majira ya 11: 30 za jioni kwa saa za Ulaya, anatarajia kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Mara baada ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kutafuatia maandamano ya Ekaristi Takatifu kuzunguka “Campo Santo Teutonico” na baadaye kutafuatia Baraka Kuu ya Ekaristi Takatifu. Kwa miaka mingi, maadhimisho haya yalikuwa yanafanyikia nje ya Vatican ili kutoa nafasi kwa ushiriki mkamilifu wa waamini. Lakini kutokana na janga la Ugonjwa wa Virus vya Korona, UVIKO-19, bado waamini wanashauriwa kuzingatia itifaki dhidi ya maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Corpus Domini
04 June 2021, 14:39