Tafuta

Papa Francisko: Katekesi Waraka Mtume Paulo Kwa Wagalatia

Papa Francisko ameanza mzunguko mpya wa Katekesi Kuhusu Waraka Wa Mtume Paulo kwa Wagalatia, unaowawezesha waamini kumfahamu zaidi Mtume Paulo, Mwalimu wa Mataifa na tema msingi katika maisha na utume wake, zinazopamba uzuri wa Injili. Anakazia toba na wongofu wa ndani na jinsi alivyoyasadaka maisha yake kwa ajili ya huduma ya Injili na Kristo Yesu! Wagalatia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia uliandikwa kunako mwaka 57 B.K. Lengo kuu lilikuwa ni kupinga mawazo ya watu waliokuwa wanapotosha imani ya kweli kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Habari Njema aliyofundisha ilipata chimbuko lake katika Agano la Kale kwa kukazia si Torati peke yake bali imani kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Torati iliwekwa kama dira na mwongozo wa kuwapeleka watu kwa Kristo Yesu na kazi hii imetekelezwa kwa uaminifu mkubwa. Mtume Paulo anawaonya Wagalatia wadumu katika uhuru walioletewa na Kristo Yesu, wasithubutu kurejea tena katika utumwa wa Torati na kwamba, Wakristo wanapaswa kuheshimiana na kupendana kwa dhati. Baba Mtakatifu Francisko baada ya kumaliza Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala, Jumatano tarehe 23 Juni 2021 ameanza Katekesi Kuhusu Waraka Wa Mtume Paulo kwa Wagalatia. Ni Waraka unaowawezesha waamini kumfahamu zaidi Mtume Paulo, Mwalimu wa Mataifa na tema msingi katika maisha na utume wake, zinazopamba uzuri wa Injili. Anakazia toba na wongofu wa ndani na jinsi alivyoyasadaka maisha yake kwa ajili ya huduma ya Injili na Kristo Yesu.

Anazungumzia mambo msingi katika imani kwa kujikita zaidi kuhusu: uhuru, neema ya kuishi kikamilifu kama Mkristo. Huu ni Waraka unaogusa mambo msingi hata katika nyakati hizi, kana kwamba, ni Waraka ulioandikwa kwa waamini katika mapambazuko ya Millenia na Tatu ya Ukristo. Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa anatoa kipaumbele cha kwanza katika mchakato wa utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema, uliomwezesha kutembelea Jumuiya ya Wagalatia walau mara mbili, kwakati wa safari zake za kimisionari. Kuna mambo mengi ambayo hayana majibu ya moja kwa moja. Baadhi ya Wagalatia waliishi katika miji ya Antiokia, Ikonio, Listra na Derbe na wengine kati kati ya Asia Ndogo na wengine katika mji mkuu wa Ankara huko Uturuki. Katika fadhaa ya kuona Wagalatia wanakabiliwa na utumwa mpya, Paulo Mtume, aliwakumbusha kwamba, aliwahubiri Injili kwa mara ya kwanza kwa sababu ya udhaifu wa mwili na jaribu hilo hawakuridharau na badala yake wakalipokea kama Malaika wa Mungu, kama Kristo Yesu. Rej. Gal 4:13.

Mwinjili Luka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume anajikita zaidi katika sababu ya maisha ya kiroho kwa kumwelezea jinsi ambavyo Mtume Paulo alivyoitwa kwenda Makedonia. Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile Neno katika Asia. Rej. Mdo 16:6. Huu ni mradi wa uinjilishaji uliobuniwa na Roho Mtakatifu na kutekelezwa na Paulo Mtume katika maisha yake. Hata leo hii kuwa wamisionari wanaojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu wakiwa nje ya nchi zao wenyewe. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Mtume Paulo aliyetumwa kwenda kuwainjilisha Wagalatia. Alianzisha Jumuiya ya waamini wachache, walikuwa na hatimaye kukomaa katika imani. Hata leo hii bado kuna watu wasiomfahamu Kristo Yesu, kumbe, Jumuiya ndogondogo za Kikristo ni chachu ya uinjilishaji wa kina. Changamoto za shughuli za kichungaji zilipewa msukumo wa pekee kabisa na Mtakatifu Paulo, Mtume, ili kulinda na kudumisha imani, matumaini na mapendo. Mtume Paulo alipambana sana watu waliongokea dini ya Ukristo toka dini ya Kiyahudi wakafanya vurugu sana katika Makanisa ya Galatia kiasi hata cha kumbeza Mtume Paulo.

Waliwahimiza Wakristo kushika Torati ya Musa na watahiriwe, ili hatimaye, waishi kama Wayahudi. Hata leo hii anasema Baba Mtakatifu Francisko kutokana na ubinafsi, wivu na uchoyo kuwa watu wanapanga hata kumng’oa Paroko na hata Askofu wa Jimbo kwa mafao binafsi. Hii ni kazi ya Shetani, Ibilisi. Haya ndiyo yaliyokuwa yanataka kutokea kwa Kanisa la Wagalatia, lakini Paulo Mtume, akasimama kidete! Paulo Mtume, anakazia kuhusu mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, chemchemi ya maisha mapya yanayokita mizizi yake katika uhuru wa kweli, licha ya historia na matukio ya maisha yao ya kale. Baba Mtakatifu anakaza kusema, changamoto na ari na mwamko wa kichungaji ni mambo yaliyokuwa na uzito wa pekee. Waamini wakiangalia kwa jicho pana zaidi wanaweza pia kung’amua mambo haya katika maisha yao. Leo kuna wahubiri wanaotumia mitandao ya kijamii kwa faida zao binafsi wanaweza kusababisha taharuki kubwa katika maisha na utume wa Kanisa mahalia. Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu. Wahubiri “uchwara” wanadai kwamba, wao wanalinda na kutetea “imani ya kweli”. Wakristo wanapaswa kuwa makini ili wasipotoshwe imani yao na walaghai.

Baba Mtakatifu anasema, ni rahisi sana kuwatambua “Wainjilishaji feki” kwa sababu wao wanakazia mambo ya kale na wanadai kufuatwa kwa udi na uvumba. Kuna baadhi ya waamini wanataka kujichimbia katika mambo na tamaduni za kale. Hawa ni watu wenye shingo ngumu. Injili ya Kristo Yesu inapaswa kuwapatia waamini uhuru wa kweli na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Waraka kwa Wagalatia ni na mwangozo thabiti wa Habari Njema ya Wokovu pamoja na imani inayosimikwa kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Utangazaji na ushuhuda wa Habari Nje ya Wokovu inatekelezwa katika fadhila ya unyenyekevu, umoja na udugu wa kibinadamu. Hiki ni lielelezo cha imani na utii, matunda ya Kazi ya Roho Mtakatifu, anayeendelea kutenda kazi katika Kanisa la Kristo Yesu. Imani kutoka kwa Roho Mtakatifu ndani ya Kanisa inaokoa.

Waraka Kwa Wagalatia

 

 

 

23 June 2021, 15:08

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >