Tafuta

Papa Francisko Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala: Udumifu katika upendo na sala! Papa Francisko Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala: Udumifu katika upendo na sala! 

Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala: Udumifu Katika Upendo na Sala!

Udumifu katika upendo na sala ni mchakato unaokita mizizi yake katika sala ya moyo inayomkiri Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu na hivyo kuomba huruma na msamaha kwa kutambua kwamba, binadamu ni mdhambi, daima anahitaji msamaha na huruma ya Mungu. Hii ni sala inayopamba siku ya mwamini, kwa sababu sala hii ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya mwamini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi yake kuhusu Fumbo la Sala amepembua kuhusu: Sala na Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa kujielekeza zaidi kwa Roho Mtakatifu anayewafunulia waamini kumhusu Kristo Yesu. Roho Mtakatifu anao uwezo wa kuchunguza hata Mafumbo ya Mungu. Ni Mungu peke yake anayemjua Mungu kabisa. Kanisa linamsadiki Roho Mtakatifu kwa sababu ni Mungu na kamwe haliachi kutangaza imani kwa Mungu mmoja: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Kanisa ni Mama, Mwalimu na Shule ya Sala. Imani inapyaishwa kwa njia ya sala. Kuna mitindo mbalimbali ya sala inayomwezesha mwamini kuzungumza na Mwenyezi Mungu. Kuna Sala ya Sauti, Sala Fikara au Tafakari na Taamuli. Katika Katekesi kuhusu Fumbo la Sala, Baba Mtakatifu amepembua kwa kina na mapana kuhusu: umuhimu wa utume wa sala na changamoto zake. Kanisa lina dhamana ya kusali na kufundisha namna ya kusali vizuri zaidi. Kanisa ni shule kuu ya sala. Baba Mtakatifu amefafanua kuhusu Sala ya Taamuli na Mapambano katika Sala ya Kikristo” na kwamba, Sala si lelemama yataka nguvu ya ndani. Amegusia kuhusu fadhaa, uzembe na ukavu katika maisha ya sala! Tumaini, Udumifu na Ujasiri katika sala ndiyo mada iliyonogesha Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kwa mara ya mwisho!

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 9 Juni 2021 kwenye Uwanja wa Mtakatifu Damasi mjini Vatican, katika Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala, amekazia kuhusu udumifu katika upendo na sala. Sehemu hii ya Katekesi imenogeshwa na Waraka wa kwanza wa Mtakatifu Paulo kwa Wathesalonike 5: 15-20 “Angalieni mtu awaye yote asimlipe mwenziwe mabaya kwa mabaya; bali siku zote lifuateni lililo jema, ninyi kwa ninyi na kwa watu wote. Furahini siku zote; Ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu. Msimzimishe Roho; msitweze unabii.” Udumifu katika upendo na sala ni mchakato unaokita mizizi yake katika sala ya moyo inayomkiri Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu na hivyo kuomba huruma na msamaha kwa kutambua kwamba, binadamu ni mdhambi, daima anahitaji msamaha na huruma ya Mungu katika maisha yake. Hii ni sala inayopaswa kupamba siku ya mwamini, kwa sababu sala hii ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya mwamini.

Mababa wa Kanisa wanawahimiza waamini kusali sala zote na maombi kila wakati katika Roho, huku wakikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote. Kukesha na kufunga daima ni sehemu ya utaratibu wa maisha ya mwamini, lakini kusali bila kukoma ni sheria. Hii ni bidii inayobubujika kutoka katika mapendo. Ni kinyume kabisa cha uzito wa uvivu na kwamba, pambano kamili la sala ni lile la mapendo ya unyenyekevu, matumaini na ya kudumu. Haya ni mapendo yanayofungulia nyoyo za waamini mambo makuu matatu yanayotoa uhai wa imani juu ya sala. Daima inawezekana kusali. Sala ni hitaji la lazima kwa maisha. Sala na maisha ya Kikristo ni sawa na chanda na pete, vinategemeana na kukamilishana. Rej. KKK 2742 – 2745. Baba Mtakatifu Francisko anasema Mapadre wanawajibu wa kuwasaidia waamini kuhakikisha kwamba, “wanawasha moto wa sala katika maisha yao ya kila siku”. Mtakatifu Yohane Chrysostom anasema, inawezekana kusali kwa motomoto hata wakati wa kutembea hadharani au ukiketi dukani kwako, ukinunua au ukiuza au hata akina mama wanapopika. Sala ni mahali ambapo mwamini anaweza kutunga wimbo wake kadiri anavyopenda na wala hakuna ukinzani na majukumu, utaratibu na mpango wa siku. Sala ni mahali ambapo kila kazi inapata maana na uwepo wake kwa sababu ni kiini cha amani na utulivu wa ndani.

Baba Mtakatifu kwa unyenyekevu mkubwa anakiri kwamba, si rahisi sana kuweza kumwilisha katika uhalisia wa maisha sheria, taratibu na kanuni za Fumbo la Sala katika maisha. Lakini licha ya “patashika nguo kuchanika” kutokana na pilika pilika za maisha hapa duniani, waamini wakumbuke kwamba, Mwenyezi Mungu anamkumbuka kila mmoja wao. Waamini wakuze utamaduni wa sala za mishale: “Bwana Unihurumie”, Bwana Unisaidie hima! “Yesu, Maria na Yosefu mnisaidie”. Ni kutokana na muktadha huu, waamini nao wanapaswa kumkumbuka Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala! Katika maisha ya Wamonaki, Kazi imekuwa ikipewa heshima kubwa si tu kwa sababu ya kanuni maadili na utu wema, bali inamwezesha mwamini kuwa na uwiano mzuri katika maisha, na kwa kukita miguu yake katika uhalisia wa maisha yenyewe. Hakuna kinacholingana na sala kwani inakifanya kiwezekane kile kisichowezekana, rahisi kile kilicho kigumu. Haiwezekani kabisa mtu anaye sali kwa makini kutenda dhambi. Sala na Kazi ni chanda na pete!

“Ikawa katika kuenenda kwao aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake. Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake. Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie. Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa. Lk 10: 38-42. Katika sehemu hii ya Injili, Kristo Yesu anakazia umuhimu wa kusikiliza Neno la Mungu, lakini si kwamba, anadharau kazi iliyokuwa ikitendwa na Mariamu. Kumbe, kuna umuhimu wa kuweka uwiano mzuri kati ya kazi na sala. Husali bila kukoma mwamini anayeunganisha sala na kazi; na kazi na sala. Ni kwa namna hii tu, waamini wanaweza kufikiri jinsi ya kanuni ya kusali bila kukoma inavyoweza kutekelezwa. Rej. KKK 2745.

Baba Mtakatifu Francisko anatoa angalisho kwamba, si vyema kutupilia mbali nafasi ya sala katika maisha ya mwamini. Kristo Yesu baada ya kuonesha utukufu na ukuu wake alipong’ara Uso mbele ya wanafunzi wake na wakataka waendelee kubaki katika mng’ao ule, aliwarejesha tena katika maisha ya kawaida. Ule mng’ao wa Sura yake ulitakiwa ubaki ndani mwao kama mwanga na nguvu ya kuimarisha imani, ili hatimaye, waweze kuipokea “Kashfa ya Fumbo la Msalaba, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa imani, matumaini na mapendo thabiti. Imani inarutubisha na kuenzi maisha ya Fumbo la Sala. Kumbe, maisha na sala na sala na maisha ni mzunguko unalomwezesha mwamini kudumu katika upendo wa Mungu.

Udumifu Katika Sala
09 June 2021, 15:30

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >