Papa Francisko: Dumuni katika sala kwa ajili ya toba, wongofu na wokovu wa walimwengu! Papa Francisko: Dumuni katika sala kwa ajili ya toba, wongofu na wokovu wa walimwengu! 

Dumisheni Sala Kwa Ajili ya Toba, Wongofu na Wokovu wa Watu!

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuunganika pamoja na Kristo Yesu, ili waweze kudumu katika sala, kwa ajili ya toba, wongofu na ukombozi wa walimwengu. Hii ni changamoto kwa waamini kuendelea kukua na kukomaa katika mahusiano na Kristo Yesu kwa njia ya sala. Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya wokovu wetu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Sala ya Saa ya Yesu inahitimisha kazi yake ya ukombozi kama Mwana mpendwa wa Mungu na Kuhani wa Milele. Hii ni sala inayotekeleza maombi makuu yanayofumbatwa katika Sala ya Baba Yetu yaani: Kushughulikia jina la Baba Mungu Mwenyezi, tamaa ya Ufalme na Utukufu wa Mungu; kutimizwa kwa mapenzi ya Mungu, mpango wa wokovu na ukombozi dhidi ya Shetani, Ibilisi. Hatimaye katika sala hii, Kristo Yesu anawafunulia waja wake ujuzi usiotenganishwa na Fumbo la Utatu Mtakatifu ambalo kimsingi ndilo Fumbo la Maisha ya Sala! Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 16 Juni 2021 amehitimisha Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuunganika pamoja na Kristo Yesu, ili waweze kudumu katika sala, kwa ajili ya toba, wongofu na ukombozi wa walimwengu. Hii ni changamoto kwa waamini kuendelea kukua na kukomaa katika mahusiano na Kristo Yesu kwa njia ya sala.

Waamini wakumbuke kwamba, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, Kristo Yesu amewakomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Waamini wamwachie nafasi Kristo Yesu, ili aweze kuwaongoza katika namna nzuri zaidi ya kusali, bila ya kuogopa jinsi gani wanasali au wanamwomba Mwenyezi Mungu kitu gani katika maisha yao. Katika hija ya maisha yao hapa duniani, waamini wajitahidi kuwa ni nuru na mwanga wa Injili kwa watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu katika salam zake kwa mahujaji na wageni, amekazia umuhimu wa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali na kuombeana mema. Waguswe na mateso, mahangaiko na mahitaji msingi ya jirani zao, na hivyo wawe tayari kuwaunga mkono kwa njia ya sala na maombi. Sala inawaunganisha watu kwa sababu ni kiungo cha upendo kwa wote. Kristo Yesu ni Kuhani mkuu anayeomba kwa ajili ya waja wake na pia anasali ndani mwao na Mwenyezi Mungu anayesikia sala zao. Rej. KKK 2749.

Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wale wote waliojihimu na hatimaye, kufanikiwa kuhudhuria katika katekesi yake kuhusu Fumbo la Sala. Lakini, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanaendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini katika maisha ya watu: kiroho na kimwili; wawe ni mashuhuda wa Injili ya furaha na amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni kwa njia ya sala, waamini wanatambua na kugundua kwamba, wao ni watoto wapendwa wa Mungu; walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kukombolewa kwa Damu Azizi ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu na kwamba, wanaendelea kutakatifuzwa na Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima. Katika furaha na mafanikio ya maisha; katika huzuni na ugumu wa mioyo, daima waamini wajiaminishe mbele ya Mwenyezi Mungu. Waamini wajenge utamaduni wa kudumu katika sala kwa sababu sala ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwamini kwa sababu kimsingi sala ni maisha.

Sala ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa waamini katika mchakato wa ujenzi wa mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake. Kwa njia ya sala waamini wanakuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu katika maisha yao, tayari kuwajibu kwa wakati muafaka, wanapokimbilia ulinzi na tunza yake ya daima.

Sala ya Saa ya Yesu
16 June 2021, 15:05