Papa Francisko Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala: Muhtasari wake. Papa Francisko Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala: Muhtasari wake. 

Papa Francisko: Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala: Muhtasari Wake!

Mchakato wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu unafumbatwa katika unyenyekevu na udugu wa kibinadamu! Hakuna sababu ya wongofu wa shuruti kwani, kimsingi wongofu wa shuruti unakinzana na ari na mwamko wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Ushuhuda wenye mvuto na mashiko ndiyo njia muafaka ya uinjilishaji mpya katika ulimwengu mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Mzunguko Mpya wa Katekesi Kuhusu Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia, Jumatano tarehe 23 Juni 2021 kwenye Uwanja wa Mtakatifu Damas mjini Vatican, amewakumbusha waamini kwamba, mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu unafumbatwa katika unyenyekevu na udugu wa kibinadamu! Hakuna sababu ya wongofu wa shuruti kwani, kimsingi wongofu wa shuruti unakinzana na ari na mwamko wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Ushuhuda wenye mvuto na mashiko ndiyo njia muafaka ya uinjilishaji mpya katika ulimwengu mamboleo. Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa anaendelea kuwaonesha waamini njia mpya ya wokovu unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kuwa inafumbatwa katika imani, utii na unyenyekevu sanjari na kutambua kwamba, Roho Mtakatifu katika nyakati zote ameendelea kutenda kazi ndani ya Kanisa. Ari na mwamko wa kimisionari kutoka kwa Mtakatifu Paulo iwe ni changamoto kwa waamini kutangaza, kushuhudia na kuishi kwa furaha ukweli wa Kiinjili. Roho Mtakatifu, Bwana na Mleta Uzima aendelee kuwaunganisha Wakristo wote, ili hatimaye, waweze kuwa ni watumishi waaminifu wa Mafumbo ya Kanisa.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 16 Juni 2021 alihitimisha Mzunguko wa Katekesi kuhusu Fumbo la Sala. Amekwisha tafakari kwa kina kuhusu: Sala na Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa kujielekeza zaidi kwa Roho Mtakatifu anayewafunulia waamini kumhusu Kristo Yesu. Roho Mtakatifu anao uwezo wa kuchunguza hata Mafumbo ya Mungu. Ni Mungu peke yake anayemjua Mungu kabisa. Kanisa linamsadiki Roho Mtakatifu kwa sababu ni Mungu na kamwe haliachi kutangaza imani kwa Mungu mmoja: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Kanisa ni Mama, Mwalimu na Shule ya Sala. Imani inapyaishwa kwa njia ya sala. Baba Mtakatifu ameelezea mitindo mbalimbali ya sala inayomwezesha mwamini kuzungumza mubashara na Mwenyezi Mungu. Anasema kuna Sala ya Sauti, Sala ya Fikara au Tafakari na Taamuli. Amepembua kwa kina na mapana kuhusu: umuhimu wa utume wa sala na changamoto zake katika maisha ya waamini. Amekumbusha kwamba, Kanisa lina dhamana ya kusali na kufundisha namna ya kusali vizuri zaidi. Kanisa ni shule kuu ya sala. Amefafanua kuhusu Sala ya Taamuli na Mapambano katika Sala ya Kikristo” na kwamba, Sala si lelemama yataka nguvu ya ndani. Amegusia kuhusu fadhaa, uzembe na ukavu katika maisha ya sala!

Tumaini, Udumifu na Ujasiri katika sala ni mambo muhimu sana katika maisha ya sala! Baba Mtakatifu amesisitizia kuhusu udumifu katika upendo na sala. Sehemu hii ya Katekesi ilinogeshwa na Waraka wa kwanza wa Mtakatifu Paulo kwa Wathesalonike 5: 15-20 “Angalieni mtu awaye yote asimlipe mwenziwe mabaya kwa mabaya; bali siku zote lifuateni lililo jema, ninyi kwa ninyi na kwa watu wote. Furahini siku zote; Ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu. Msimzimishe Roho; msitweze unabii.” Udumifu katika upendo na sala ni mchakato unaokita mizizi yake katika sala ya moyo inayomkiri Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu na hivyo kuomba huruma na msamaha kwa kutambua kwamba, binadamu ni mdhambi, daima anahitaji msamaha na huruma ya Mungu katika maisha yake. Hii ni sala inayopaswa kunogesha siku ya mwamini, kwa sababu sala hii ni sehemu ya vinasaba vya maisha yake!

Kama muhtasari wa hitimisho la mzunguko wa Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala, Jumatano tarehe 16 Juni 2021, Kwenye Uwanja wa Mtakatifu Damas mjini Vatican, Baba Mtakatifu alifafanua kuhusu Sala ya Saa ya Yesu inayokita ujumbe wake katika Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Hii ni Sala ambayo Kristo Yesu aliisali alipokuwa Bustanini Gethsemane. “Kisha wakaja mpaka bustani iitwayo Gethsemane; akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa muda niombapo. Akamtwaa Petro na Yakobo na Yohane pamoja naye, akaanza kufadhaika sana na kuhangaika. Akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa mkeshe. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akiomba ya kuwa, ikiwezekana, saa hiyo imwepuke. Akasema, Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.” Mk 14:32-36.

Papa Sala
23 June 2021, 14:42