Papa Francisko asema, Bara la Afrika lina kiu ya ustawi, amani na maendeleo fungamani ya binadamu. Papa Francisko asema, Bara la Afrika lina kiu ya ustawi, amani na maendeleo fungamani ya binadamu. 

Papa Francisko Bara la Afrika Lina Kiu ya Amani na Maendeleo!

Watu zaidi ya 160 wamefariki dunia na wengine wengi wamejeruhiwa vibaya sana. Baba Mtakatifu ameonesha uwepo wake wa karibu kwa familia na watu wa Mungu nchini Burkina Faso katika ujumla wao. Mashambulizi ya kigaidi yamekuwa yakisababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu anasema, Bara la Afrika linahitaji amani na wala si vita, kinzani wala vurugu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa linataka kuwa ni chombo cha matumaini kwa watu wa Mungu Barani Afrika kwa kujikita zaidi katika misingi ya haki; amani na ushirikiano wa udugu wa kibinadamu katika ukweli na uwazi. Vatican katika masuala ya diplomasia ya Kimataifa inataka kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Dhana hii inatekelezwa kwa kuwekeza katika sekta ya elimu, afya, uchumi pamoja na ustawi wa jamii. Lengo ni kutengeneza madaraja yanayowaunganisha watu na Mwenyezi Mungu ili hatimaye, kujenga umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Amani inafumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 6 Juni 2021, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Sherehe ya Mwili na Damu Azizi ya Bwana Wetu Yesu Kristo, “Corpus Domini” amependa kuwahakikishia watu wa Mungu nchini Burkina Faso walioathirika kutokana na vitendo vya kigaidi vilivyofanywa Ijumaa, usiku wa kuamkia Jumamosi tarehe 5 Juni 2021 kwenye Kijiji cha Solhan.

Watu zaidi ya 160 wamefariki dunia na wengine wengi wamejeruhiwa vibaya sana. Baba Mtakatifu ameonesha uwepo wake wa karibu kwa familia na watu wa Mungu nchini Burkina Faso katika ujumla wao. Mashambulizi ya kigaidi yamekuwa yakisababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu anasema, Bara la Afrika linahitaji amani na wala si vita, kinzani, vurugu na mipasuko. Mama Kanisa anatambua kwamba, amani inafumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Haya ni mambo yanayosimikwa katika kanuni maadili, uhuru wa kujieleza pamoja na mchakato mzima wa maamuzi yanayotolewa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Haki na amani ni sawa na chanda na pete, vinakumbatiana na kukamilishana. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanahimiza ushirikiano wa Kimataifa katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya amani na udugu wa kibinadamu. Kanisa halina budi kuwafunda watoto wake kujenga dhamiri nyofu, ili kukuza majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kuweza kuwa na uwajibikaji wa pamoja. Rej. GS. 90.

Ni katika mazingira kama haya, Mtakatifu Paulo VI kunako tarehe 6 Januari 1967 alianzisha Tume ya Kipapa ya Haki na Amani na leo hii, kuna Baraza la Maendeleo Fungamani ya Binadamu linalojikita zaidi katika utekelezaji wa haki jamii sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kanisa ni daraja linalounganisha dhana ya amani na mshikamano unaoongozwa na kanuni auni kwa ajili ya maboresho ya maisha ya watu wa Mungu. Kanisa Barani Afrika linataka kuendelea kuwa ni Sakramenti ya Wokovu, kwa kujielekeza zaidi katika misingi ya: haki, maridhiano na ushirikiano wa kweli. Linapenda kuona maendeleo fungamani ya binadamu yanagusa mahitaji msingi ya binadamu kama ushuhuda wa haki katika maisha ya watu wa Mungu. Falsafa, sera na siasa ya Kanisa Barani Afrika inapania kujenga daraja la dhana ya amani na mshikamano wa dhati, ili kukidhi mahitaji msingi ya binadamu; kwa kukazia: haki, amani ya kudumu na ushirikiano wa kweli. Haki ya kweli inafumbatwa katika mshikamano unaothamini tunu msingi, utu na heshima ya binadamu. Ikumbukwe kwamba, haki ni fadhila adilifu iliyo na utashi wa kudumu na thabiti wa kumpa Mungu na jirani iliyo haki yao.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, amani ni safari ya matumaini: Majadiliano, Upatanisho na Wongofu wa kiikolojia. Amani na utulivu wa Jumuiya ya Kimataifa, hauwezi kamwe kujengeka katika msingi wa vitisho na hofu ya maangamizi, kumbe, kuna haja ya kuvunjilia mbali mawazo ya vitisho na hofu. Baba Mtakatifu katika ujumbe huo wa Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2019 alipembua kwa kina na mapana amani, kama safari ya matumaini inayokabiliana na vizingiti pamoja na majaribu. Amani ni safari ya ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza unaosimikwa katika kumbukumbu, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Amani ni safari ya upatanisho katika umoja wa kidugu. Amani ni safari ya wongofu wa kiikolojia na kwamba, watu wataweza kupata yale yote wanayotumainia. Hii ni changamoto kwa watu wa Mungu kujikita katika mchakato wa ujenzi wa haki, amani na upatanisho. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanahimiza ushirikiano wa Kimataifa katika mambo ya kiuchumi, kwa kuwapatia raia elimu bora zaidi, ili waweze kushika majukumu katika sekta mbalimbali za maisha. Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni dhana inayohitaji ushiriki mkubwa wa Jumuiya ya Kimataifa, utu, heshima na haki msingi za binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza.

Lengo ni kupambana na umaskini, ujinga na maradhi yanayoendelea kupekenya utu wa binadamu. Mahitaji msingi ya binadamu yanapaswa kuwa ni kitovu cha maendeleo na ustawi wa binadamu. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika hija yake ya kitume hivi karibuni Barani Afrik alisema, Kanisa limekwisha kuchangia sana kuhusu dhana ya amani inayomwilishwa katika haki. Pengine, kwa sasa unakosekana utashi wa kunafsisha dhana hii katika hali halisi ya watu wa Mungu, kwa kukazia utashi wa kimaadili na kiutu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Diplomasia ya Vatican inasimikwa katika misingi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Maana mambo ya kidunia na yale ya kiimani, asili yake ni katika Mungu yule yule. Utu wa binadamu hauna budi kulindwa na kuheshimiwa. Mchakato wa ujenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu unapania kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi ili kuvunjilia mbali vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kidini na kisiasa. Ni mwaliko wa kusimama kidete kupambana na ujinga, umaskini na maradhi.

Papa Amani Afrika

 

08 June 2021, 15:46