Katika maadhimisho ya Sikukuu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeti, tarehe 31 Mei 2021, Baba Mtakifu ataongoza Sala ya Rozari Takatifu. Katika maadhimisho ya Sikukuu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeti, tarehe 31 Mei 2021, Baba Mtakifu ataongoza Sala ya Rozari Takatifu. 

Sikukuu ya B. Maria Kumtembelea Elizabeti: Mapendo kwa Jirani

Jumatatu jioni tarehe 31 Mei 2021, Baba Mtakatifu Francisko atafunga Mwezi wa Rozari Takatifu kwa kusali Rozari takatifu na waamini kwenye Bustani za Vatican. Kwa muda wa Mwezi mzima, waamini wameungana na Baba Mtakatifu Francisko kusali Rozari sehemu mbalimbali za dunia, huku wakiomba ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa dhidi ya UVIKO-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Rozari takatifu ni muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi wa mwanadamu na ni sehemu ya maisha ya Kristo Yesu. Ni sala inayowawezesha waamini kukimbilia chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, kwa ajili ya kuombea haki, amani na maridhiano kati ya watu, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Rozari ni sala ya waamini wa kawaida inayowahakikishia uwepo endelevu wa Bikira Maria katika safari ya maisha yao huku bondeni kwenye machozi. Waamini wanakumbushwa umuhimu wa kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kuombea: toba na wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha; haki na amani; umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kama Bikira Maria alivyowataka Watoto wa Fatima, yaani Francis, Yacinta Marto na Lucia dos Santos. Mwezi Mei ni muda muafaka wa kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, silaha za pambano dhidi ya dhambi na ubaya wa moyo ni: Tafakari ya Neno la Mungu, Sala, Sakramenti ya Upatanisho pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Waamini wajenge na kukuza utamaduni wa kusali Rozari takatifu. Mwezi Mei 2021 umetengwa kwa namna ya pekee na Mama Kanisa ili kuendelea kumlilia Mwenyezi Mungu ili aweze kusitisha janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambalo limesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Tarehe 31 Mei ya Kila Mwaka, Kanisa linaadhimisha Sikukuu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeth. Huu ni ushuhuda wa fadhila; ni mkutano kati ya Agano la Kale na Agano Jipya; huruma na upendo wa Mungu unaookoa na kuponya. Huu ni ushuhuda wa Injili ya matumaini, kwa watu wa Agano la Kale na kama ilivyo kwa watu wa ulimwengu mamboleo! Huu mwendelezo wa utenzi wa sifa, shukrani na furaha ya ujio wa Masiha, Mkombozi wa Ulimwengu unaotambuliwa na Yohane Mbatizaji. Bikira Maria ni Sanduku la Agano Jipya na la Milele. Ni Mama wa Mkombozi anayekwenda kumtembelea Elizabeth. Hapa wanawake wawili wanaohifadhi ndani mwao Injili ya uhai wanakutana. Bikira Maria ni mtumishi wa Bwana na Elizabeth ni kielelezo cha matumaini mapya kwa Waisraeli. Bikira Maria anakwenda kwa haraka kumsalimia Elizabeth, kielelezo makini cha huduma ya upendo kwa jirani na mfano wa kuigwa hasa katika ulimwengu mamboleo unaogubikwa na ubinafsi na uchoyo wa kutisha!

Ni katika muktadha huu, Jumatatu jioni tarehe 31 Mei 2021, Baba Mtakatifu Francisko atafunga Mwezi wa Rozari Takatifu kwa kusali Rozari takatifu na waamini kwenye Bustani za Vatican. Kwa muda wa Mwezi mzima, waamini wameungana na Baba Mtakatifu Francisko kusali Rozari sehemu mbalimbali za dunia, huku wakiomba ulinzi na tunza ya Bikira Maria dhidi ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Uinjilishaji Mpya linasema, kumekuwepo na shuhuda kutoka sehemu mbalimbali za dunia, kuonesha ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu katika Ibada hii. Baba Mtakatifu anatarajiwa kupokea zawadi ya picha ya Bikira Maria Mfungua Mafundo kutoka Augsburg, Ujeruman. Mafundo hapa yaeleweke kuwa ni shida na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo waamini hasa katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambalo limesababisha madhara makubwa katika sekta ya afya, uchumi, kisaikolojia na hata katika mafungamano ya watu.

Waamini wanamwomba Bikira Maria afungue mafundo yanayokwamisha mahusiano na mafungamano ya kijamii; mafundo ya upweke hasi yanayowafanya watu kuchungulia kaburi. Afungue mafundo ya watu kutowajali jirani zao. Bikira Maria afungue mafundo ya ukosefu wa fursa za ajira; kinzani, vipigo na ukatili wa kijinsia ndani ya familia. Bikira Maria asaidie kufungua fundo la umaskini; sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, ili watu waweze kuwa na ari na mwamko mpya wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ibada hii itatangazwa mubashara na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican.

Rozari Takatifu

 

28 May 2021, 16:27