Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amesema Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni ni hitimisho la Fumbo la Umwilisho! Kristo Yesu sasa ametukuka mbinguni lakini anaendelea kuwa na wafuasi wake katika kutangaza na kushuhudia Injili. Baba Mtakatifu Francisko amesema Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni ni hitimisho la Fumbo la Umwilisho! Kristo Yesu sasa ametukuka mbinguni lakini anaendelea kuwa na wafuasi wake katika kutangaza na kushuhudia Injili.  (Vatican Media)

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Tangazeni Injili ya Kristo

Kristo Yesu alishuka kutoka mbinguni kwa uwezo wa Roho Mtakatifu akafanyika mwili na sasa anapaa kwenda kwa Baba yake, baada ya kukamilisha kazi nzima ya ukombozi. Ni Mtu kweli na Mungu kweli. Ubinadamu wake umetukuka mbinguni, mwaliko kwa waamini kutafakari Fumbo la Kupaa mbinguni, kwa imani na matumaini. Kristo Yesu bado anaendelea kukaa kati pamoja nao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kwa muda wa siku arobaini, baada ya mateso, kifo na ufufuko wake, Kristo Yesu aliwatokea na kuzungumza na wafuasi wake, akala na kunywa nao, akawaimarisha katika misingi ya imani, matumaini na mapendo thabiti. Wakati wote huo, utukufu wake ulikuwa bado umefunikwa na alama za ubinadamu wa kawaida. Kanisa linakiri na kufundisha kwamba, Kristo Yesu alipaa mbinguni, amekaa kuume kwa Baba. Mwinjili Marko katika Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, Mk. 16:15-20, anamwonesha Kristo Yesu akiwa na Mitume wake kabla ya Kupaa kwenda mbinguni na kukaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi. Hiki ni kipindi cha kuagana, kimsingi kinasheheni simanzi, hali ya kupondeka na kuvunjika moyo, kwa kudhani kwamba, sasa Mitume wa Yesu wamebaki yatima na kama ilivyo kawaida kwa mtoto yatima kamwe hadeki!

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, Jumapili tarehe 16 Mei 2021, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Mitume wanaanza kujipanga kikamilifu, huku wakiwa wamesheheni furaha kubwa nyoyoni mwao, tayari “kuchanja mbuga” kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kwa Kristo Yesu Kupaa Mbinguni, anahitimisha utume wa kukaa pamoja nao hapa duniani. Huyu ndiye Kristo Yesu aliyeshuka kutoka mbinguni kwa uwezo wa Roho Mtakatifu akafanyika mwili na sasa anapaa kwenda kwa Baba yake, baada ya kukamilisha kazi nzima ya ukombozi. Ni Mtu kweli na Mungu kweli. Ubinadamu wake umetukuka mbinguni, mwaliko kwa waamini kutafakari Fumbo la Kupaa mbinguni, kwa imani na matumaini. Kristo Yesu bado anaendelea kukaa kati pamoja na waja wake kwa mtindo mwingine wa maisha.

Kristo Yesu aliwaagiza wafuasi wake kwenda ulimwenguni kote kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kumbe, bado yuko pamoja na wafuasi wake, wanapotangaza na kushuhudia Injili, baada ya kushukiwa na Roho Mtakatifu. Kwa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, Wakristo wote wamepewa dhamana na wajibu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu tangu baada ya ufufuko wake hadi pale atakapokuja tena kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Hii ni dhamana na utume ambao Kristo Yesu amewadhaminisha wafuasi wake, licha ya nguvu, uwezo, dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu. Jambo la msingi ni kutambua kwamba, Kristo Yesu bado anatenda kazi pamoja nao na hata katika sala. Amepaa kwenda mbinguni na sasa ameketi kuume kwa Baba yake wa milele akiwaombea waja wake. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, mchakato wa uinjilishaji utaweza kufanikiwa ikiwa kama kila mwamini atamwachia nafasi Roho Mtakatifu aweze kutenda kazi ndani mwake. Kwa njia hii, waamini wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Kristo!

Kwa njia ya ushuhuda wao, wanageuka kuwa ni: Jicho la Kristo Yesu ili kuona mahitaji msingi ya maskini na wale wote waliosahaulika au kutengwa na jamii. Waamini wanakuwa ni mikono ya Kristo Yesu ili kugusa, kuganga na kuponya wale waliojeruhiwa. Ni sikio la kusikiliza kilio cha watu wasiokuwa na sauti na hatimaye, wanakuwa ni ulimi wa kusimulia wema na huruma ya Mungu sanjari na kuwashirikisha wengine matumaini; kwa kusikiliza na hatimaye kuguzwa manukato ya utakatifu wa maisha badala ya kuzungukwa na uvundo wa dhambi! Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika maadhimisho ya Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, wamwombe Bikira Maria, Malkia wa Mbingu, awasaidie ili waweze kuwa mashuhuda hodari wa Kristo Yesu Mfufuka katika uhalisia wa maisha yao!

Papa Uinjilishaji

 

 

 

16 May 2021, 15:20