Patriaki Gregory Peter XX Gabroyan amefariki dunia tarehe 25 Mei 2021 na kuzikwa tarehe 29 Mei 2021 Patriaki Gregory Peter XX Gabroyan amefariki dunia tarehe 25 Mei 2021 na kuzikwa tarehe 29 Mei 2021 

Patriaki Gregory P. XX Gabroyan: Mtetezi wa Maskini na Wanyonge!

Papa Francisko amepokea taarifa ya Msiba wa Patriaki Gregory Peter XX Gabroyan wa Kanisa Katoliki la Waarmenia kwa masikitiko makubwa. Anamkumbuka vyema kwani kunako mwaka 2015 kabla ya kukubali kupokea dhamana ya kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu nchini Lebanon, aliomba baraka ili aweze kutekeleza majukumu haya kwa ufanisi mkubwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Patriaki Gregory Peter XX Gabroyan wa Kanisa Katoliki la Waarmenia amefariki dunia tarehe 25 Mei 2021 akiwa na umri wa miaka 86 tangu alipozaliwa. Ibada ya mazishi imeadhimishwa na Askofu mkuu Boutros Marayati, Kanisa Katoliki la Waarmenia, Jumamosi tarehe 29 Mei 2021 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Gregory mwangaza na Eliasi na kuzikwa huko Bzommar-Keserwan, nchini Lebanon. Kardinali Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Siria amesoma salam za rambirambi kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Itakumbukwa kwamba, Patriaki Gregory Peter XX Gabroyan wa Kanisa Katoliki la Waarmenia alizaliwa tarehe 15 Novemba 1934 huko Aleppo nchini Siria. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 28 Machi 1959. Tangu wakati huo amefanya utume wake nchini Lebanon na Ufaransa. Patriaki Gregory Peter XX Gabroyan alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Amekuwa ni faraja na kimbilio kwa watu wa Mungu nchini Lebanon hasa katika miaka ya hivi karibuni kutokana na mtikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa. Hata katika hali ya ugonjwa, akiwa kitandani, bado aliendelea kujishughulisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Lebanon

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika salam za rambirambi alizomwandikia Askofu mkuu Boutros Marayati, Msimamizi wa Kanisa Katoliki la Waarmenia anasema, amepokea taarifa ya Msiba wa Patriaki Gregory Peter XX Gabroyan wa Kanisa Katoliki la Waarmenia kwa masikitiko makubwa. Anamkumbuka vyema kwani kunako mwaka 2015 kabla ya kukubali kupokea dhamana ya kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu nchini Lebanon, aliomba baraka ya pekee, ili aweze kutekeleza majukumu haya kwa ufanisi mkubwa. Tarehe 7 Septemba 2015 wakaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu pamoja, kama kielelezo cha Umoja katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, huduma muhimu kwa Kanisa na sehemu ya mchakato wa majiundo, ili kufanana na hatimaye, kumwambata Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Baba Mtakatifu anasema, wakati wa hija yake ya kitume nchini Armenia, mwaka 2016 waliambatana pamoja. Na Mwaka 2018 wakati wa uzinduzi wa Sanamu ya Mtakatifu Gregory wa Narek kwenye Bustani za Vatican alikuwepo na kushuhudia tukio hili.

Ni katika matukio haya makuu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, amebahatika kuwa karibu zaidi na Patriaki Gregory Peter XX Gabroyan. Ni kiongozi aliyependwa sana na watu wa Mungu nchini Armenia, kiasi cha kuvumilia mateso, mahangaiko na madhulumu katika maisha yake. Pamoja na yote hayo, lakini aliendelea kubaki akiwa mwaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Alikuwa ni mhamasishaji mkuu wa upendo na mshikamano kati ya watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kwa ajili ya Siria na Lebanon. Tayari alikuwa ameanzisha mchakato wa kumtangaza kuwa Mwenyeheri na hatimaye Mtakatifu, Kardinali Gregory Peter XV Agagianian. Mwishoni mwa maisha yake hapa duniani, anasema Baba Mtakatifu Francisko, Hayati Patriaki Gregory Peter XX Gabroyan alipambana sana na maisha, akawajibika na kujiuliza kama bado angeweza kuendelea kuwaongoza waamini wa Kanisa Katoliki la Armenia, lakini Mwenyezi Mungu amemwita ili akapumzike kwenye makazo ya uzima wa milele. Baba Mtakatifu anapenda kuiweka roho ya Patriaki Gregory Peter XX Gabroyan wa Kanisa Katoliki la Waarmenia kwa huruma na upendo wa Mungu, akisindikizwa na sala na maombezi ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa pamoja na watakatifu wa mbinguni, ili hatimaye, aweze kupokelewa huko mbinguni na kuungana na watakatifu pamoja na mashuhuda wa imani kutoka Armenia.

Kwa upande wake, Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki ambaye pia ni Makamu wa Dekano wa Baraza la Makardinali, amempongeza Patriaki Gregory Peter XX Gabroyan kwa miaka mingi ya huduma kwa watu wa Mungu. Ni kiongozi ambaye walifahamiana na mara kwa mara waliadhimisha pamoja Mafumbo ya Kanisa. Sasa anasali na kumwombea ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kumpokea na kumkirimia maisha ya uzima wa milele.

Rambirambi Armenia
29 May 2021, 15:26