Baba Mtakatifu anawaalika waamini kushikamana na Kristo Yesu ili waweze kuzaa matunda ya upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa Mungu na jirani mhitaji zaidi. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kushikamana na Kristo Yesu ili waweze kuzaa matunda ya upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa Mungu na jirani mhitaji zaidi. 

Papa Francisko: Tangazeni na Kushuhudia Injili ya Upendo!

Kumbe, wanadamu wanapaswa kupendana wao kwa wao kwa kutumia kipimo cha Kristo Yesu. Huu ni upendo wenye nguvu kiasi hata cha kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine. Huu ni upendo kamili, usiokuwa na hila ndani yake, ni upendo usiokuwa na masharti ya “nipe nikupe”, hii ni zawadi ya Mungu kwa binadamu. Upendo unapaswa kumwilishwa katika huduma kwa wahitaji zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mwinjili Yohane, Jumapili ya VI ya Kipindi cha Pasaka ya Bwana, Mwaka B wa Kanisa, anapembua upendo na kuuweka katika ngazi kuu tatu: Upendo wa Mungu kwa Mwanaye Kristo Yesu. Pili ni Upendo wa Kristo Yesu kwa binadamu wote. Tatu ni upendo wa Baba na Mwana unaomwilishwa katika upendo kwa watu wote bila ubaguzi. “Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu.” Yn. 15:19. Hiki ndicho kipimo cha upendo wa Kristo, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu. Kukaa katika pendo la Kristo Yesu maana yake ni kuwa waaminifu katika Sheria na Amri zake, ambazo amezipatia muhtasari kwa kuzikita katika upendo kwa Mungu na jirani. Hiki ndicho kiini cha Amri Mpya ya upendo kwa Mungu na jirani. Huu ni upendo unaobubujika kutoka kwa Mungu kwa sababu Mungu ni upendo. Asiyejua kupenda anabaki katika kifo. Rej. 1Yn. 3:14.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 9 Mei 2021 wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ametafakari kuhusu umuhimu wa waamini kubaki wakiwa wameungana na Kristo Yesu ambaye amejitambulisha kuwa ni Mzababu wa kweli. Wakibaki wakiwa wameungana na Kristo Yesu watazaa matunda ya toba na wongofu wa ndani, kielelezo cha upendo kamili. Yesu anasema, “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe.” Yn. 15: 10 – 11. Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya furaha na upendo kamili kwa sababu Mungu ni upendo. Mto wa upendo unatiririka kutoka kwa Mungu Baba Mwenyezi kupitia kwa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu hadi kuvifikia viumbe vyote. Kumbe, wanadamu wanapaswa kupendana wao kwa wao kwa kutumia kipimo cha Kristo Yesu. Huu ni upendo wenye nguvu kiasi hata cha kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine. Huu ni upendo kamili, usiokuwa na hila ndani yake, ni upendo usiokuwa na masharti ya “nipe nikupe”, hii ni zawadi ya Mungu kwa binadamu.

Upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, umewawezesha wanadamu kuwa ni rafiki wa Kristo na hivyo kupata uwezo wa kumfahamu Baba na hatimaye, kushirikishwa katika utume wake kwa ajili ya maisha ulimwenguni. Waamini wanaweza kubaki huku wakiwa wameshikamana na kufungamana na Kristo Yesu kwa kushika Amri na maagizo yake sanjari na wao wenyewe kupendana kama kielelezo cha ushuhuda wa wafuasi wa Kristo. Kupenda kama anavyopenda Kristo Yesu, maana yake ni kumwilisha upendo huu katika huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii ni huduma inayonafsishwa katika matendo kama Kristo Yesu mwenyewe, siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, alipowaosha wanafunzi wake miguu na kuwataka kuoshana miguu wao kwa wao kama alivyowafanyia. Kwa kupendana wao kwa wao, wafuasi wa Kristo wanaendeleza utume wa huduma ambayo Mwana wa Mungu alikuja kuitekeleza hapa duniani, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake ili yaweze kuwa ni fidia ya wengi, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wake kwa binadamu.

Upendo wa Kristo unawawajibisha wafuasi wake kutoka katika ubinafsi wao, usalama wa mambo ya kidunia pamoja na starehe, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wahitaji zaidi. Ni hali ya kujiweka tayari, kwa kile ambacho Mwenyezi Mungu amewakirimia na kuwajalia jinsi walivyo! Huu ni upendo unaoshuhudiwa kwa matendo na wala si kwa maneno matupu ambayo kamwe hayawezi kuvunja mfupa! Upendo wa Kristo unawataka waja wake kuondokana na uchu wa mali, fedha na madaraka, kwani aina hii ya upendo, inawapeleka mbali zaidi na upendo halisi unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Matokeo yake wanajikuta wakiwa wachoyo, wabinafsi na “watu wa kutaka kujimwambafai”. Upendo unaochechemea matokeo yake ni mipasuko ya kijamii, ghasia na vita. Waathirika wakuu kila kukicha ni wanawake na watoto. Kupenda kama Kristo Yesu anavyopenda maana yake ni kuwaheshimu na kuwathamini jirani zako jinsi walivyo, bila kudai ziada. Kristo Yesu anawataka wafuasi wake kuishi katika upendo anaoutaka Yeye na wala si kadiri ya vionjo vyao binafsi, wala ibada za watu kujiabudu wao wenyewe; kwa kutaka kuwatawala na kuwamiliki wengine.

Upendo wa kweli ni kujiaminisha na kujisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa jirani! Kristo Yesu anasema, “Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe” Jn. 15:11. Baba Mtakatifu Francisko anasema, maana yake ni kuhakikisha kwamba, furaha inayobubujika kutoka kwa Baba na Mwana, inaimarisha umoja na mafungamano kati yao wenyewe, huku wakiwa wameungana na Fumbo la Utatu Mtakatifu. Furaha ya kutambua kwamba, wanapendwa na Mwenyezi Mungu, licha ya mapungufu yao ya kibinadamu inawawezesha kuwa na imani thabiti, kiasi hata cha kupambana na changamoto za maisha kwa ushujaa zaidi. Ni furaha na upendo unaowawezesha waamini kuvuka shida na changamoto za maisha wakiwa wameimarika zaidi. Ni katika muktadha wa kuishi na kumwilisha furaha na upendo huu, unageuka na kuwa ni utambulisho wao kama wafuasi amini wa Kristo Yesu. Bikira Maria awasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kubaki katika upendo wa Kristo Yesu na hivyo kuendelea kukua na kukomaa katika pendo hili, tayari kujisadaka kwa ajili ya jirani, huku wakishuhudia furaha ya Kristo Yesu Mfufuka!

Papa Upendo

 

 

09 May 2021, 15:29

Sala ya Malkia wa Mbingu ni nini?
 

Utenzi wa Malkia wa Mbingu ni kati ya tenzi nne za Bikira Maria (nyingine ni:Tunakimbilia Ulinzi wako,  Salam Malkia wa Mbingu, Salam Malkia). Kunako mwaka 1742, Papa Benedikto XIV alipoandika kwamba, waamini wasali Sala ya Malkia wa Mbingu wakiwa wamesimama, kama alama ya ushindi dhidi ya kifo, wakati wa Kipindi cha Pasaka, yaani kuanzia Domenika ya Ufufuko wa Bwana hadi Sherehe ya Pentekoste. Hii ni Sala ambayo husaliwa mara tatu kwa siku kama ilivyo pia Sala ya Malaika wa Bwana: Asubuhi, Mchana na Jioni ili kuweka wakfu Siku kwa Mwenyezi Mungu na Bikira Maria.

Utenzi huu kadiri ya Mapokeo ulianza kutumika kunako karne ya VI au Karne X, lakini kuenea kwake kunaanza kujitokeza katika nyaraka mbali mbali kati kati ya Karne ya XIII, ilipoingizwa kwenye Kitabu cha Sala za Kanisa cha Wafranciskani. Hii ni Sala inayoundwa na maneno mafupi manne yanayohitimishwa na Alleluiya na sala ya waamini wanaomwelekea Bikira Maria, Malkia wa mbingu, ili kufurahia pamoja naye kuhusu Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu.

Papa Francisko tarehe 6 Aprili 2015 wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, siku moja baada ya Sherehe ya Pasaka, aliwashauri waamini kuwa na moyo wa furaha wanaposali sala hii. “Tunamwendea Bikira Maria, tukimwomba afurahi, kwa sababu yule Mwanaye mpendwa aliyekuwa amemchukua mimba amefufuka kweli kweli kama alivyosema; tunajiaminisha kwa sala na maombezi ya Bikira Maria. Kimsingi furaha yetu ni mwangi wa furaha ya Bikira Maria kwani ndiye aliyetunza na anaendelea kutunza matukio mbali mbali ya maisha ya Yesu. “Tusali sala hii kwa furaha ya kuwa waana wa Mungu ambao wanafurahi kwa sababu Mama yao anafurahi”

 

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >