Papa Francisko: Sherehe ya Kupaa Bwana Yesu Mbinguni: Changamoto kwa waamini kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya maisha adili na matakatifu. Papa Francisko: Sherehe ya Kupaa Bwana Yesu Mbinguni: Changamoto kwa waamini kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya maisha adili na matakatifu. 

Papa Francisko: Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Ushuhuda Amini

Waamini wawe na ujasiri wa kuangalia mambo ya juu na kamwe wasiridhike na mambo ya dunia, kwani haya yanapita. Watambue wito na utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia kwa njia ya maisha yao adili na matakatifu. Daima Roho Mtakatifu atawaongoza katika mapambano ya maisha ya kiroho, jambo la msingi ni kujiaminisha kwake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Katika Kanuni ya Imani Mama Kanisa anasadiki na kufundisha kwamba, “Akapaa mbinguni; amekaa kuume kwa Baba. Atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu; nao ufalme wake hautakuwa na mwisho.” Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni mwa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 12 Mei 2021 kwenye Uwanja wa Mtakatifu Damas mjini Vatican amewakumbusha waamini kwamba, Kanisa, tarehe 13 Mei 2021 linaadhimisha Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, ingawa kutokana na sababu za kichungaji, Sherehe hii itaadhimishwa rasmi, Jumapili tarehe 16 Mei 2021 sanjari na Siku ya 55 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2021 inayonogeshwa na kauli mbiu “Njoo uone”, Yn 1:46. Ni wakati muafaka kwa waamini kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho haya na kwamba, anawaombea amani na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu Mfufuka. Waamini wawe na ujasiri wa kuangalia mambo ya juu na kamwe wasiridhike na mambo ya dunia, kwani haya yanapita kama “upepo wa kisulisuli”.

Waamini watambue wito na utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia kwa njia ya maisha yao adili na matakatifu. Daima Roho Mtakatifu atawaongoza katika mapambano ya maisha ya kiroho, jambo la msingi ni kujiaminisha kwake! Baba Mtakatifu anakaza kusema, Yesu kabla ya kupaa kwenda mbinguni aliwaambia wafuasi wake kwamba, atawapelekea Roho Mtakatifu na kamwe hatawaacha yatima; atakuja kwao! Haya ni maneno ya faraja ambayo hata leo hii, Kristo Yesu anataka kuwaambia wafuasi wake. Watakuwa ni marafiki zake, ikiwa kama watafikiri na kutenda katika maisha yao kama anavyotaka! Daima ataonesha na kudhihirisha uwepo wake endelevu na kamwe hawatajisikia kuwa yatima! Baba Mtakatifu amewataka waamini kufuata mfano wa Bikira Maria na Mitume wa Yesu waliokuwa wakidumu katika moyo mmoja katika kusali, ili waweze kuwa imara katika kufuata nyayo za Kristo Yesu.

Kwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria, awawezeshe wafuasi wa Kristo kuwa wanyenyekevu, huku wakiendelea kusali na kungoja ujio wa Roho Mtakatifu. Wakristo wakuze na kudumisha ndani mwao sanaa ya ujenzi wa umoja wa Kanisa; wawe ni mashuhuda wa imani na vyombo vya Injili ya upendo. Wakristo wajitahidi katika maisha na utume wao, kuwa kweli ni washiriki na mashuhuda wa kazi ya ukombozi, kwa kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza. Wajitahidi kumfungulia Roho Mtakatifu ili aweze kuwakirimia mapaji na karama zake; ili hatua kwa hatua, aendelee kuwafunda katika mantiki ya Injili, upendo na ukarimu; kwa kuwafundisha na kuwakumbusha yale yote ambayo Kristo Yesu aliyasema katika maisha na utume wake hapa duniani!

Kupaa Bwana Mbinguni
12 May 2021, 14:50