Papa Francisko: Maadhimisho ya Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ni kielelezo cha ufuo wa upendo wa Mungu. Papa Francisko: Maadhimisho ya Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ni kielelezo cha ufuo wa upendo wa Mungu. 

Papa Francisko: Utatu Mtakatifu Ni Fumbo la Upendo wa Mungu

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, Papa Francisko anasema, hili ni Fumbo ambalo limefunuliwa na Kristo Yesu, ambaye amewawesha waamini kuufahamu Uso wa Mungu mwenye upendo; akajitambulisha kuwa ni Mwana na Neno wa Mungu na Roho Mtakatifu atokaye kwa Baba na Mwana, Roho Mfariji na Mtetezi wa watu wake. Mungu ni upendo

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Neema ya Bwana wetu Kristo Yesu, na pendo la Mungu na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote! Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, msingi wa Mafumbo yote yanayosherehekewa na Kanisa kwa nyakati mbalimbali. Hili ni Fumbo la imani na la maisha ya Kikristo. Ni Fumbo la Mungu ndani yake Mwenyewe. Mwenyezi Mungu katika historia na Mpango ukombozi amejifunua kuwa ni Mungu mmoja katika Nafsi Tatu. Baba Mungu Mwenyezi Mwumba mbingu na nchi, na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Kanisa linasadiki kwa Kristo Yesu, Mwana wa pekee, wa Mungu aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Ni Mungu aliyetoka kwa Mungu, Mwanga kwa mwanga. Mungu kweli kwa Mungu kweli. Aliyezaliwa bil kuumbwa, Mwenye umungu mmoja na Baba. Ndiye aliyeshuka kutoka mbinguni kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kanisa linasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana na mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa na Baba na Mwana: Aliyenena kwa vinywa vya Manabii.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 30 Mei 2021, Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu amesema hili ni Fumbo kuu linalopita uelewa wa binadamu. Mwenyezi Mungu amejifunua mwenyewe na anabaki ni Fumbo lisiloelezeka katika ukamilifu wake. Amejifunua mwenyewe kama “Yeye aliye”, amejijulisha kama mwingi wa huruma na fadhila; ukweli na upendo! Kwa ufupi kabisa, “Mungu ni upendo”. 1Yoh. 4:8.16. Uwepo wenyewe wa Mungu ni upendo. Kwa kumpeleka Mwanawe pekee na Roho wa Upendo, nyakati zilipotimia, Mwenyezi Mungu akafunua siri yake ya ndani kabisa; Mungu mwenyewe ni ushirikiano wa milele wa upendo. Fumbo la Utatu Mtakatifu limefunuliwa na Kristo Yesu, ambaye amewawesha waamini kuufahamu Uso wa Mungu mwenye huruma na mapendo; akajitambulisha kuwa ni Mwana na Neno wa Mungu na Roho Mtakatifu atokaye kwa Baba na Mwana, Roho Mfariji na Mtetezi wa watu wake.

Yesu Kristo Mfufuka alipowatokea wafuasi wake aliwatuma kwenda kutangaza na kushuhudia Injili kwa Mataifa yote, ili waweze kuwa ni wanafunzi wake, kwa kuwabatiza “kwa jina la Baba, na la Mwana, na Roho Mtakatifu”. Mt. 28:19. Utume wa Mama Kanisa na wafuasi wake katika ujumla wao, ni kuhakikisha kwamba, wote wanazamishwa katika pendo la Mungu, ili waweze kupokea wokovu na maisha ya uzima wa milele! Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ni mwaliko kwa waamini kuadhimisha Fumbo la Upendo asili, dira na mwelekeo wa safari ya maisha yao hapa duniani. Ni mwaliko wa kuimarisha umoja na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao, huku wakijichotea nguvu hii kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Huu ndio utashi na wosia wa kiroho unaobubujika kutoka katika Sala ya Kikuhani aliyosali Kristo Yesu kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu: “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.” Yn. 17:21.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu lazima kukite mizizi yake katika umoja, kielelezo makini cha uzuri wa Injili, changamoto kubwa ni kumwilisha umoja huu na kuutolea ushuhuda katika maisha kama waamini licha ya mipasuko na migawanyiko iliyopo hadi wakati huu. Hata katika tofauti zao msingi, lakini Wakristo wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa upendo wa Mungu, kwa kuheshimiana na kupendana kama ndugu wamoja katika Kristo Yesu. Wakristo wawe ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa wale wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao huku bondeni kwenye machozi kama: wageni “watu wa kuja, vyasaka na wanyamahanga”. Waoneshe huruma na mapendo kwa watu waliojeruhiwa katika maisha na utu wao; watu wanaobezwa na kusumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Upendo ni kielelezo cha Mungu aliye hai, mwaliko kwa kushirikiana na kushikamana na wengine katika huduma. Wawe na ujasiri pamoja na fadhila ya unyenyekevu, ili kutoa na kupokea msamaha.

Ni wajibu wa waamini wote kuthamini karama na mapaji ambayo Roho Mtakatifu amewakirimia kadiri ya ujenzi wa umoja na mshikamano wa kidugu. Kwa njia hii, waamini wataweza kusongesha mbele mchakato wa ukuaji na ukomavu wa jumuiya ya waamini inayoinjilisha kwa nguvu ya upendo wa Mungu anayeishi ndani mwao kwa njia ya karama ya Roho Mtakatifu. Mwishoni mwa tafakari yake kuhusu Fumbo la Utatu Mtakatifu, Baba Mtakatifu Francisko amewaambia waamini kwamba, Bikira Maria katika unyenyekevu wake analitafakari Fumbo la Utatu Mtakatifu, Mungu mmoja katika Nafsi tatu, akalipokea Fumbo hili katika maisha yake. Awasaidie waamini kuimarisha imani yao, ili waweze kumwabudu Mwenyezi Mungu sanjari na kutoa huduma kwa jirani zao!

Fumbo la Upendo
30 May 2021, 15:25

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >