Baraza la Maaskofu Katoliki Italia tarehe 24 Mei 2021 litaanza mkutano wake mkuu wa 74 utakaofunguliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia tarehe 24 Mei 2021 litaanza mkutano wake mkuu wa 74 utakaofunguliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. 

Papa Francisko: Mkutano Mkuu wa 74 wa Maaskofu Italia, CEI: Sinodi

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 24 Mei 2021 anatarajia kufungua maadhimisho ya Mkutano mkuu 74 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, Jumanne, tarehe 25 Mei 2021 atatoa hotuba elekezi kama sehemu ya mbinu mkakati wa uinjilishaji mpya mintarafu dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Sinodi ya XVI ya Maaskofu itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba 2021-2023 itaongozwa na kauli mbiu “Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume” Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kuhusu umuhimu wa kumwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kukazia umuhimu wa watu wa Mungu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Juhudi za kichungaji na kitaalimungu zisaidie kuimarisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu majadiliano ya kidini na kiekumene, kwa kumpokea Roho Mtakatifu, ili kuweza kujifunza mengi kutoka kwa wengine, na kuvuna kile ambacho Roho Mtakatifu amepanda ndani yao, ambacho kimekusudiwa kuwa ni zawadi kwa jirani!

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi Mwezi Oktoba 2021: Mchakato wa Awamu ya Kwanza utayahusu Makanisa Mahalia na Taasisi zote za Kanisa: Oktoba 2021 hadi Aprili 2022. Makanisa mahalia yatatumiwa mada na maswaili dodoso yakufanyiwa kazi. Awamu ya Pili ni kuanzia Septemba 2022 hadi Machi 2023. Lengo kuu ni kuhamasisha majadiliano katika ngazi ya Mabara, ili hatimaye, kutengeneza Hati ya Kutendea Kazi: “Instrumentum Laboris”. Awamu ya Tatu, Kanisa la Kiulimwengu kuanzia mwezi Oktoba 2023 na wajumbe watakaokuwa wameteuliwa watashiriki katika Sinodi itakayoadhimishwa chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Lengo kubwa ni kuwashirikisha na kuwasikiliza watu wa Mungu, kujenga na kuimarisha urika wa Maaskofu pamoja na kumsikiliza Roho Mtakatifu, mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 24 Mei 2021 anatarajia kufungua maadhimisho ya Mkutano mkuu 74 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI. Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, Jumanne, tarehe 25 Mei 2021, majira ya asubuhi, atatoa hotuba elekezi ya mkutano huu, kama sehemu ya mbinu mkakati wa uinjilishaji mpya unaohitaji upyaisho wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu mintarafu “Dhana ya Sinodi” katika maisha na utume wa Kanisa. Askofu Franco Giulio Brambilla wa Jimbo Katoliki la Novara ambaye pia ni Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, atatoa mwelekeo wa jumla wa Kanisa Katoliki nchini Italia na baadaye, kutakuwa na kazi za vikundi ili kupembua mambo mazito na mbinu mkakati utakaotumika katika utekelezaji wa maazimio haya!

Papa na CEI 2021

 

 

 

22 May 2021, 14:32