Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema katika maadhimisho ya Juma la Laudato si kuanzia tarehe 16-25 Mei 2021: Kazi ya Uumbaji! Papa Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema katika maadhimisho ya Juma la Laudato si kuanzia tarehe 16-25 Mei 2021: Kazi ya Uumbaji! 

Papa Francisko: Juma la Laudato Si: 16-25 Mei 2021: Kazi ya Uumbaji

Papa Francisko: Jumapili tarehe 16 Mei 2021 amewaambia waamini kwamba, huo ulikuwa ni mwanzo wa maadhimisho ya Juma la “Laudato si” litakalofikia kilele chake tarehe 25 Mei 2021 sanjari na kufunga rasmi “Mwaka wa Laudato si.”. Ni muda muafaka kwa Kanisa kupima mafanikio yaliyopatikana katika Maadhimisho ya Mwaka wa Laudato si katika mchakato wa wongofu wa kiekolojia

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayokita mizizi yake katika misingi ya haki, amani, ustawi, maendeleo, mafao ya wengi na wongofu wa kiekolojia, kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” uliozinduliwa hapo tarehe 18 Juni 2015 mjini Vatican. Baba Mtakatifu anapenda kukazia umuhimu wa kutunza mazingira, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki, kwani uharibifu wa mazingira unalinganishwa na umaskini; anaihimiza jamii pamoja na kuendelea kutunza furaha, amani na utulivu wa ndani; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete na kamwe hayawezi kutenganishwa. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume wa “Laudato si”, anapembua kwa kina na mapana kuhusu: Mambo yanayotokea katika mazingira; Umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Uumbaji. Anabainisha vyanzo vya mgogoro wa ekolojia vinavyohusiana na watu, baadaye anazama zaidi kufafanua maana ya ekolojia katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Anatoa ushauri kuhusu njia za kupanga na kutekeleza na mwishoni anajiekeza zaidi katika elimu ya ekolojia na maisha ya Kikristo!

Baba Mtakatifu wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, Jumapili tarehe 16 Mei 2021 amewaambia waamini kwamba, huo ulikuwa ni mwanzo wa maadhimisho ya Juma la “Laudato si” litakalofikia kilele chake tarehe 25 Mei 2021 sanjari na kufunga rasmi “Mwaka wa Laudato si.”. Ni muda muafaka wa kupima mafanikio yaliyopatikana katika Maadhimisho ya Mwaka wa Laudato si katika mchakato wa wongofu wa kiekolojia. Ni kipindi maalum cha kufanya upembeuzi yakinifu kuhusu madhara yaliyosababishwa na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ili kujiandaa vyema kuweza kukabiliana na majanga kwa siku za usoni Huu ni muda uliokubaliwa wa kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini, wanaohitaji msaada na uwajibikaji ili hatimaye, kuleta mageuzi makubwa yanayofumbatwa katika wongofu wa kiekolojia, kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya dunia ambayo inaendelea kuchakaa kama “jani la mgomba”. Wanasayansi wanasema, tabia ya ulaji wa kupindukia, matumizi mabaya ya rasilimali za dunia na uchafuzi wa mazingira umevuka kiwango cha dunia kuweza kustahimili, kiasi kwamba, kwa sasa kinachofuatia ni majanga asilia kama yanavyoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia. Kuna hatari kubwa ya kukiachia kizazi kijacho: mashimo, jangwa na lundo kubwa la takataka.

Baba Mtakatifu analishukuru Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu, Wanaharakati wa Mazingira Wakatoliki Duniani, Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis; wadau na watetezi wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya. Katika kipindi hiki chote, washiriki wanaendelea kujielekeza zaidi katika majadiliano kuhusu utunzaji wa mazingira nyumba ya wote katika elimu na nishati mbadala ili kupandikiza matumaini pamoja na kueneza Sala ya Injili ya Kazi ya Uumbaji. Kuna nyimbo kuhusu Kazi ya Uumbaji. Katika maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste, wadau watakutana kusali kwa ajili ya kuhitimisha Mwaka wa Laudato si, tayari kutumwa kwenda kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Tarehe 24 Mei 2021 kutakuwepo na majadiliano kuhusu haki ya maji na huduma bora ya afya. Tarehe 25 Mei 2021 kutakuwa na uzinduzi wa Jukwaa la “Laudato si”.

laudato si

 

 

17 May 2021, 16:06