Tafuta

Vatican News
Papa Francisko Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala: Tumaini, Udumifu na Ujasiri katika maisha ya sala! Papa Francisko Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala: Tumaini, Udumifu na Ujasiri katika maisha ya sala!  (Vatican Media)

Papa: Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala: Tumaini, Udumifu na Ujasiri

Tumaini, Udumifu na Ujasiri katika sala ndiyo mada iliyonogesha Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 26 Mei 2021 kwenye Uwanja wa Mtakatifu Damasi mjini Vatican. Tafakari hii imeongozwa na Neno la Mungu, jinsi ambavyo Kristo Yesu alivyomfufua Binti wa Yairo, hata baada ya yule mkuu wa Sinagogi kuambiwa kwamba yule binti amekwisha kufa! “Usiogope, amini”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko bado anaendelea na Katekesi kuhusu Fumbo la Sala. Ameendelea kujikita katika: Sala na Utatu Mtakatifu kwa kujielekeza zaidi kwa Roho Mtakatifu anayewafunulia watu kumhusu Kristo Yesu. Roho Mtakatifu anao uwezo wa kuchunguza hata Mafumbo ya Mungu. Ni Mungu peke yake anayemjua Mungu kabisa. Kanisa linamsadiki Roho Mtakatifu kwa sababu ni Mungu na kamwe haliachi kutangaza imani kwa Mungu mmoja: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Kanisa ni Mama, Mwalimu na Shule ya Sala. Imani inapyaishwa kwa njia ya sala na kwamba, kuna mitindo mbalimbali ya sala, ili kuweza kuzungumza na Mwenyezi Mungu kuna: Sala ya Sauti, Sala Fikara au Tafakari na Taamuli. Baba Mtakatifu amekwisha kupembua kuhusu: umuhimu wa utume wa sala na changamoto zake. Kanisa lina dhamana ya kusali na kufundisha namna ya kusali vizuri zaidi. Kanisa ni shule kuu ya sala. Amefafanua kuhusu Sala ya Taamuli na Mapambano katika Sala ya Kikristo” na kwamba, Sala si lelemama yataka “kifua kweli kweli”. Mwishoni, alitafakari kuhusu fadhaa, uzembe na ukavu katika maisha ya sala! Tumaini, Udumifu na Ujasiri katika sala ndiyo mada iliyonogesha Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 26 Mei 2021 kwenye Uwanja wa Mtakatifu Damasi mjini Vatican.

Tafakari hii imeongozwa na Neno la Mungu, jinsi ambavyo Kristo Yesu alivyomfufua Binti wa Yairo, hata baada ya yule mkuu wa Sinagogi kuambiwa kwamba yule binti amekwisha kufa! Neno la Yesu lilikuwa “Usiogope, amini”. Rej. Mk 5:22-24. 35-36. Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kuwa na tumaini na udumifu katika sala na hasa wakati ambapo waamini wanahisi kwamba, sala zao hazisikilizwi hata kidogo na huo unakuwa ni mwanzo wa makwazo katika sala! Baba Mtakatifu anasema, mwamini anasali kumwombea ndugu yake afya njema, badala ya kupona anafariki dunia! Waamini wamesali sana kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kusitisha vita huko Yemen na Siria, lakini hadi leo hii, bado vita inaendelea kurindima na watu kupoteza maisha sehemu mbalimbali za dunia! Ni katika muktadha kama huu, baadhi ya waamini wanasitisha na kukoma kusali. Mababa wa Kanisa wanasema, tumaini la kimwana hujaribiwa, hujithibitisha katika taabu. Ugumu wa kwanza wahusu sala ya maombi kwa ajili ya mtu mwenyewe au kwa ajili ya wengine katika maombezi. Wengine huacha kusali kwa sababu wanafikiri sala na maombi yao hayasikilizwi. Rej. KKK 2734.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kujiuliza maswali msingi: Kwanini wanafikiri kwamba, maombi yao hayakusikilizwa? Namna gani sala yao inasikilizwa, namna gani ni sala ya kufaa? Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatoa muhtasari wa maswali haya msingi kwa kusema kwamba, hiki ni kielelezo cha ukosefu wa mang’amuzi ya imani yanayotaka kugeuza mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu kuwa kama “mazingaombwe” kwa kumtaka Mwenyezi Mungu atende kama wanavyotaka wao! Sala ni majadiliano kati ya mwamini na Mwenyezi Mungu. Waamini wanapomsifu na kumshukuru Mungu kwa wema na ukarimu wake, hawajihangaishi kwa namna ya pekee kujua ikiwa kama sala yao imempendeza Mungu au la! Wanataka kumlazimisha Mwenyezi Mungu awatendee kama wanavyotaka na kukidhi matakwa ya nyoyo zao. Kristo Yesu kwa hekima na busara yake, amewafundisha wafuasi wake Sala ya Baba Yetu, muhtasari wa mafundisho makuu yaliyotolewa na Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, sehemu ya kwanza ya Sala ya Baba Yetu ni maombi yanayotolewa kwa Mwenyezi Mungu na hatimaye, waamini wanajiaminisha kwa Mungu ili mapenzi yake yaweze kufanyika. “Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.” Mt. 6:9-10. Kadhalika Roho Mtakatifu anawasaidia katika udhaifu wao kwa maana hawajui kuomba jinsi iwapasavyo. Kumbe, hapa kuna haja ya kuwa na unyenyekevu na kujiweka katika mazingira ya kusali vizuri zaidi, kwa kuchagua maneno na hatimaye kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu kwa kutambua uwepo wake kati yao. Waamini wamwachie Mwenyezi Mungu awapatie nafasi ya toba na wongofu wa ndani, ili mwisho wa siku, waweze kusali vyema zaidi kadiri ya mapenzi ya Mungu kwa ajili ya ustawi na mafao ya roho zao. Licha ya juhudi zote hizi, bado kashfa ya waamini kutosikilizwa na Mwenyezi Mungu inaendelea kutawala katika akili na nyoyo zao! Ili kuondokana na kashfa ya kudhani kwamba, Mwenyezi Mungu amewageuzia kisogo waja wake, kuna haja ya kutafakari kwa kina Injili Takatifu, ili kuona jinsi ambavyo kimsingi maisha ya Kristo Yesu yalivyosheheni sana kwa ajili ya watu waliojeruhiwa kiroho na kimwili; wanaoomba huruma na neema ya Mungu katika maisha yao. Kuna watu wanaosali kwa ajili ya walemavu, watoto wao; watu wanaosali kutokana na shida na mahangaiko yao, wote hawa wanamkimbilia na kumlilia Kristo Yesu wakisema, “Bwana Utuhumie”.

Baba Mtakatifu anasema, kuna wakati ambapo waamini wanadhani kwamba, Mwenyezi Mungu kamwe hasikilizi sala zao. Mfano dhahiri ni imani ya yule Mwanamke Mkananayo aliyeamua kudumu katika kuomba, huku akijibizana na Kristo Yesu, kiasi hata cha kumwambia “hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao”. Ndipo Yesu alipoiona imani ya Mwanamke Mkananayo na hatimaye, kumponya binti yake “Mama imani yako ni kubwa! Na iwe kwako kama utakavyo.” Akapona binti yake tangu saa ile! Huu ni ujasiri na udumifu katika sala. Kristo Yesu alimsamehe dhambi na kumponya mwenye kupooza kule Kapernaumu, kielelezo cha muda wa Mungu kutenda anavyotaka! Rej. Mk. 2:1-12. Uponywaji wa Binti wa Yairo ni kielelezo cha matumaini katika sala inayomwilishwa katika imani thabiti! Katika giza la maisha, imani na matumaini, waamini wawe na ujasiri wa kumwomba Mwenyezi Mungu awasaidie kuimarisha imani na kusikiliza sala na maombi yao. Baada ya Njia ya Msalaba, Jumamosi Kuu kuna Pasaka ya Bwana, yaani Ufufuko wa Kristo Yesu. Wema daima utashinda ubaya na mwanadamu atakirimiwa wokovu. Waamini wajifunze kuwa na unyenyekevu wanaposubiri neema na baraka ya Mungu katika maisha yao! Mwisho wa siku, Kristo Yesu atashinda yote!

Sala: Tumaini na Udumifu
26 May 2021, 16:03