Baba Mtakatifu Francisko tarehe 16 Mei 2021 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Myanmar: Amekazia umuhimu wa kutunza imani, umoja na ukweli! Baba Mtakatifu Francisko tarehe 16 Mei 2021 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Myanmar: Amekazia umuhimu wa kutunza imani, umoja na ukweli! 

Papa Francisko: Tunzeni: Imani, Umoja na Ukweli Katika Maisha!

Papa Francisko amekazia:Uumuhimu wa kutunza imani, umoja na ukweli, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Mambo haya msingi ni wosia uliotolewa na Yesu kabla ya kupaa na kurejea mbinguni kwa Baba yake wa milele. Wosia huu ni kielelezo cha: urafiki, upendo na nguvu ya kukabiliana na matatizo na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Siku arobaini baada ya Ufufuko wa Kristo Yesu, Mama Kanisa huadhimisha Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni ambayo kwa mwaka huu hapa mjini Vatican imeadhimishwa tarehe 13 Mei 2021. Lakini kutokana na sababu za kichungaji Sherehe hii sehemu mbalimbali za dunia imeadhimishwa rasmi Jumapili tarehe 16 Mei 2021 sanjari na Siku ya 55 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2021 inayonogeshwa na kauli mbiu “Njoo uone”, Yn 1:46. Huu ni wakati kwa waamini kuwa na ujasiri wa kuangalia mambo ya juu na kamwe wasiridhike na mambo ya dunia, kwani haya yanapita kama “upepo wa kisulisuli”. Waamini watambue wito na utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia kwa njia ya maisha yao adili na matakatifu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 16 Mei 2021 ameadhimisha Jumapili ya Saba ya Kipindi cha Pasaka, kwa ajili ya kuombea haki, amani na utulivu nchini Myanmar. Ibada hii imehudhuriwa na watu wa Mungu kutoka nchini Myanmar. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kutunza imani, umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na ukweli, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia!

Baba Mtakatifu anasema, mambo haya msingi ni wosia uliotolewa na Kristo Yesu kabla ya kuondoka na kurejea mbinguni kwa Baba yake wa milele. Wosia huu ni kielelezo cha: urafiki, upendo na nguvu ya kuweza kukabiliana na matatizo na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika maisha. Katika kipindi hiki kigumu katika historia ya maisha ya watu wa Mungu nchini Myanmar wanahimizwa kutunza imani, umoja na ukweli. Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu akainua macho yake kuelekea mbinguni, huku akiwaombea Mitume wake. Hizi zilikuwa ni nyakati za mwisho kabla ya kupambana na Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu. Aliuona usiku wa giza machoni pake, akahisi usaliti na hata kukimbiwa na wale aliowapenda. Aliyainua macho yake mbinguni, bila kukata tamaa wala kutawaliwa na machungu ya moyo. Huu ni wosia aliokuwa amewapatia hata Mitume wake akiwaambia kwamba, hata watakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo watambue ya kwamba, uharibifu wake umekaribia. “Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia.” Lk 21:28.

Hii ni changamoto ya kutunza imani kwa kuyaelekeza macho mbinguni, kwa sababu hapa duniani kuna mapambano ya vita na damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumwagika. Kutunza imani maana yake ni kukataa katukatu kutumbukia katika dimbwi la chuki na uhasama na badala yake, kujielekeza zaidi katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu kwa kutambua kwamba, kimsingi wao ni ndugu wamoja! Hata katika nyakati za shida na mahangaiko makubwa, waamini wanapaswa kujiaminisha mbele ya Mungu, ili kuendelea kuwa na matumaini hata mahali ambapo hakuna matumaini hata kidogo. Imani kwa Mwenyezi Mungu ni silaha madhubuti inayoendelea kupyaisha mapendo na matumaini dhidi ya utamaduni wa kifo. Hii ni changamoto kubwa ya imani kwani kishawishi kikubwa ni kujifungia katika ubinafsi na kuanza kutamani kulipiza kisasi, kama kielelezo cha kujihami na kumlilia Mungu. Hata pale waamini wanapolalama na kumlilia Mungu, machozi yao yanageuka kuwa ni chemchemi ya sala!

Pengine kilio ni sala inayosikilizwa zaidi na Mwenyezi Mungu kuliko aina nyigine yoyote ya sala, kwani sala hii inabubujika kutoka katika moyo uliovunjika na kupondeka. Na mara nyingi, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, hupangusa macho ya watoto wake, ndiyo maana inalipa kutunza imani! Baba Mtakatifu Francisko anawataka watu wa Mungu nchini Myanmar kutunza umoja, kama ambavyo Kristo Yesu alivyowaombea Mitume wake ili wote wawe na umoja, kama familia moja ambamo upendo wa kidugu unatawala. Kristo Yesu aliwafahamu fika Mitume waliokuwa wanagombea madaraka, wakifikiri ni nani ambaye angekuwa wa kwanza, yaani kiongozi wao. Hii ndiyo saratani ya utengano, migawanyiko na mipasuko, kielelezo makini cha yale yanayotendeka katika undani wa maisha ya binadamu, katika: familia, jamii na hata wakati mwingine ndani ya Kanisa. Dhambi ya utengano inajikita katika: wivu, uchoyo, mafao binafsi badala ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Tabia ya kuwahukumu wengine, uchu wa mali na madaraka ni mambo yanayochochea kinzani, mipasuko na hatimaye, vita!

Kristo Yesu katika wosia wake, anawataka Wafuasi wake kulinda umoja kwani kinzani na utengano ni kazi ya Shetani, Ibilisi. Watu wa Mungu waendelee kujikita katika ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu kama familia, kwa kuwa na ujasiri wa kuishi kirafiki katika upendo na udugu! Katika changamoto mamboleo zinazojitokeza katika masuala ya kisiasa na kijamii, udugu wa kibinadamu unapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Kanisa kwa upande wake, liwe ni chambo cha kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja sanjari na kusaidiana, lengo ni kuimarisha umoja na mshikamano wa kidugu. Baba Mtakatifu anawataka watu wa Mungu nchini Myanmar kutunza ukweli, ili kuendeleza mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Watambue kwamba Ukweli huu ni Kristo Yesu mwenyewe, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kadiri ya Mwinjili Yohane.

Huu ni mwaliko wa kuendelea kushikamana na kufungamana na Kristo Yesu katika ukweli na kamwe wasiruhusu kumezwa na malimwengu. Wawe ni manabii na mashuhuda wa ukweli hata kama itawagharimu maisha. Kamwe wasikubali kukengeuka na kumezwa na malimwengu. Waamini wajizatiti katika ukweli kwa ajili ya ukweli wenyewe, ili kujisadaka kwa ajili ya jirani zao. Katika vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, waamini wawe waaminifu kwa tunu msingi za Kiinjili na watetezi na walinzi wa amani, ili kuleta mabadiliko yanayokusudiwa. Waamini wajiweke wakfu kwa ukweli na uzuri wa Injili, ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Ufalme wa Mungu hata katika giza nene, machungu ya moyo na hata pale ambapo Shetani, Ibilisi anaonekana kana kwamba, “amewashinda kwa bao la kisigino”. Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko amesema kwamba, ameitolea Sadaka ya Misa Takatifu kwa ajili ya mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu nchini Myanmar, ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kuziongoa nyoyo zote na kuzielekeza katika amani. Waendelee kutunza imani, wajizatiti katika ujenzi wa umoja na kuishi katika ukweli wa Injili. Kamwe wasikate tamaa kwa sababu Kristo Yesu, anawaombea waja wake wote, ili Mwenyezi Mungu awaweke mbali na mwovu na kuwaokoa dhidi ya nguvu za Shetani, Ibilisi.

Papa Myanmar

 

 

16 May 2021, 16:00