2021.05.23 Regina Coeli 2021.05.23 Regina Coeli 

Papa Francisko:Katika Kanisa kuna vikundi vidogo visivyo vya kiroho

Roho Mtakatifu anatufanya kuwa viumbe vipya.Mitume mara baada ya kupokea Roho Mtakatifu hawakuwa na hofu tena.Walitoka nje na kushuhudia kuwa Bwana amefufuka.Kanisa ni la kila mtu,kwa kila mtu kama vile Roho Mtakatifu alivyooneesha siku ya Pentekoste.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Katika Siku Kuu ya Pentekoste Jumapili 23 Mei 2021, Papa Francisko ametoa tafakari yake wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, kwa kuongozwa na somo la siku amesema  “Kitabu cha Matendo ya mitume kinasimulia kilichotokea huko Yerusalemu mara baada ya siku hamsini za Pasaka ya Yesu. Mitume walikuwa pamoja wameunganika katika karamu kuu wakiwa na Bikira Maria. Bwana mfufuka alikuwa amewambia wabaki katika mji hadi atakapokuwa amewatumia kutoka juu zawadi ya Roho.  Hii ilijionesha wazi kwa ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Huu ni zoefu wa kweli lakini pia wa ishara”.

Wenyewe unaonesha kuwa  Roho Mtakatifu ni kama upepo wa nguvu na ulio huru. Huwezi kuuthibiti, kuusimamisha, na wala kuupima;  wala kuutazama mwelekeo wake. Hatabiriki katika mahitaji ya kibinadamu na katika mifumo yetu na hukumu zetu. Roho anayetoka kwa Mungu Baba  na Mwanaye Yesu Kristo na kuvuvia juu ya Kanisa, juu ya kila mmoja kwa kutoa maisha katika akili zetu na katika mioyo yetu. Kama  sala ya kanuni ya imani: “Ni Bwana na mleta uzima”.

Katika Siku ya Pentekoste, wanafunzi wa Yesu walikuwa bado na wasi wasi na wanaogopa. Hawakuwa bado na ujasiri wa kutoka nje. Hata sisi, wakati mwingine, tunapendelea kubaki kati ya kuta za ulinzi wa mazingira yetu. Lakini Bwana anajua jinsi gani ya kutufikia na kufungua milango ya mioyo yetu. Yeye anatutumia  Roho Mtakatifu juu yetu na kutukumbatia na kushinda hofu zetu, kuangusha vizingiti vyetu, anaibua  usalama wetu wa uongo. Roho anatufanya kuwa viumbe wapya na kama alivyo fanya siku ile kwa Mitume.

Wao baada ya kupokea Roho Mtakatifu hawakuwa kama mwanzo, bali walitoka nje na kuanza kuhubiri kuwa Yesu amefufuka. Ni Bwana kweli kiasi kwamba kila mmoja alikuwa anaelewa kwa lugha yake. Roho anabadili moyo, anapanua mtazamo wa mitume. Anawafanya kuwa na uwezo wa kuwasiliana na wote matendo makuu ya Mungu bila kizingiti, kutoka katika mipaka ya utamaduni na kidini ambayo walikuwa wamezoea kufikiria na kuishi. Anawaweka kwa namna ya kufikia wengi huku wakiheshimu uwezekano wao wa kusikiliza na kuelewa katika utamaduni na lugha ya kila mmoja. Kwa mananeo mengine, Roho Mtakatifu anawaweka katika mawasiliano watu tofauti kwa kutumiza umoja na ulimwengu wa Kanisa.

Papa Francisko ametoa ushauri wa kufunguliaa hata leo hii mioyo kwa zawadi ya Roho ambaye anafanya kusikia uzuri wote na ukweli wa upendo wa Mungu katika Kristo aliyekufa na kufufuka. Na anatusukuma kutoka nje kwenda kushuhudia upendo huo ambao daima unatutangulia na huruma yake.  Dunia inahitaji ujasiri, wa matumaini, na imani ya wafuasi wa Kristo. Kwa kuhitimisha Papa Francisko amesema tuombe Bikira Maria Mama wa Kanisa atuoombee ili Roho Mtakatifu ashuke kwa wingi na kujaza mioyo ya waamini na kuwasha moto wa pendo kwa wote.

23 May 2021, 12:22

Sala ya Malkia wa Mbingu ni nini?
 

Utenzi wa Malkia wa Mbingu ni kati ya tenzi nne za Bikira Maria (nyingine ni:Tunakimbilia Ulinzi wako,  Salam Malkia wa Mbingu, Salam Malkia). Kunako mwaka 1742, Papa Benedikto XIV alipoandika kwamba, waamini wasali Sala ya Malkia wa Mbingu wakiwa wamesimama, kama alama ya ushindi dhidi ya kifo, wakati wa Kipindi cha Pasaka, yaani kuanzia Domenika ya Ufufuko wa Bwana hadi Sherehe ya Pentekoste. Hii ni Sala ambayo husaliwa mara tatu kwa siku kama ilivyo pia Sala ya Malaika wa Bwana: Asubuhi, Mchana na Jioni ili kuweka wakfu Siku kwa Mwenyezi Mungu na Bikira Maria.

Utenzi huu kadiri ya Mapokeo ulianza kutumika kunako karne ya VI au Karne X, lakini kuenea kwake kunaanza kujitokeza katika nyaraka mbali mbali kati kati ya Karne ya XIII, ilipoingizwa kwenye Kitabu cha Sala za Kanisa cha Wafranciskani. Hii ni Sala inayoundwa na maneno mafupi manne yanayohitimishwa na Alleluiya na sala ya waamini wanaomwelekea Bikira Maria, Malkia wa mbingu, ili kufurahia pamoja naye kuhusu Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu.

Papa Francisko tarehe 6 Aprili 2015 wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, siku moja baada ya Sherehe ya Pasaka, aliwashauri waamini kuwa na moyo wa furaha wanaposali sala hii. “Tunamwendea Bikira Maria, tukimwomba afurahi, kwa sababu yule Mwanaye mpendwa aliyekuwa amemchukua mimba amefufuka kweli kweli kama alivyosema; tunajiaminisha kwa sala na maombezi ya Bikira Maria. Kimsingi furaha yetu ni mwangi wa furaha ya Bikira Maria kwani ndiye aliyetunza na anaendelea kutunza matukio mbali mbali ya maisha ya Yesu. “Tusali sala hii kwa furaha ya kuwa waana wa Mungu ambao wanafurahi kwa sababu Mama yao anafurahi”

 

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >