Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya kumbukumbu ya Miaka 40 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II atembelee kwenye kiwanda cha kufua chuma cha Terni, anakazia dhana na wito wa kazi kama urithi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya kumbukumbu ya Miaka 40 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II atembelee kwenye kiwanda cha kufua chuma cha Terni, anakazia dhana na wito wa kazi kama urithi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. 

Dhana na Wito wa Kazi ni Amana ya Mafundisho Jamii ya Kanisa!

Dhana na wito wa kazi ni sehemu ya urithi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. Mama Kanisa angependa kuona maboresho ya mazingira ya kazi na maisha ya wafanyakazi sehemu mbalimbali za dunia kwa kutambua kwamba, kimsingi kazi ni wito kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Tangu mwanzo Mwenyezi Mungu alimtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kazi ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu ambaye ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, kazi ni wito wa mwanadamu. Kazi ni utimilifu wa mtu binafsi, kijamii na kiekolojia. Hapa ni mahali pa kubadilishana mawazo, mang’amuzi na uzoefu wa maisha. Ni mahali pa kujenga mahusiano kwa kukutana na watu wengine, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na ujenzi wa utamaduni wa upendo. Wito wa kazi una uhusiano wa pekee na mazingira nyumba ya wote, ambayo mwanadamu amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu kuyalinda, kuyatunza na kuyaendeleza kama sehemu ya ekolojia fungamani ya maisha ya mtu binafsi, jamii na dunia katika ujumla wake. Ilikuwa ni tarehe 19 Machi 1981, Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mchumba wake Bikira Maria, Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea kiwanda kikubwa cha kufua chuma pamoja na mji wa Terni, nchini Italia katika ujumla wake. Imegota miaka 40 tangu tukio hili la kihistoria lilipotekea. Imekuwa ni fursa pia kwa Askofu Giuseppe Piemontese, OFM, Conv. wa Jimbo Katoliki la Terni-Narni-Amelia kuadhimisha kumbukizi hili kama sehemu ya tafakari ya kina kuhusu: dhana na wito wa kazi katika maisha ya mwanadamu.

Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limesababisha vifo vya watu wengi duniani, mateso na mahangaiko makubwa kwa watu. UVIKO-19 limezalisha kundi kubwa la watu wasiokuwa na fursa za ajira pamoja na umaskini. Yote haya yanapelekea watu kukosa dira, mwelekeo na matumaini kwa siku za usoni. Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea kiwandani hapo aligusia umuhimu wa maisha ya binadamu; utu na heshima ya kazi; haki jamii na kanuni maadili kama msingi wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika amani na uhuru kamili. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Askofu Giuseppe Piemontese, OFM, Conv. wa Jimbo Katoliki la Terni-Narni-Amelia anazungumzia kuhusu: mtikisiko wa uchumi Kitaifa na Kimataifa ulioharibiwa zaidi na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kanisa ni mtetezi wa maskini na wanyonge katika jamii. Wadau wote wanapaswa kusimama kidete ili kuendeleza fursa za ajira.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwahakikishia watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Terni-Narni-Amelia, uwepo wake wa karibu kiroho, kwa njia ya sala pamoja na kuwatia shime, ili kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu.  Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limechangia kwa kiasi kikubwa mtikisiko wa uchumi Kitaifa na Kimataifa, kiasi cha kuvuruga matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Huu ni wakati wa kupyaisha uwajibikaji, ujenzi wa umoja na mshikamano wa kidugu pamoja na kushirikishana rasilimali na utajiri wa dunia hii. Jambo la msingi katika hali na mazingira kama haya ni kujikita katika utawala wa sheria unaozingatia; kanuni maadili na utu wema; utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. Dhana na wito wa kazi ni sehemu ya amana na urithi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. Mama Kanisa angependa kuona maboresho makubwa ya mazingira ya kazi na maisha ya wafanyakazi sehemu mbalimbali za dunia kwa kutambua kwamba, kimsingi kazi ni wito kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Tangu mwanzo Mwenyezi Mungu alimtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza. Rej. Mwa 2:15. Kazi ni wito wa kwanza wa mwanadamu unaomkirimia mwanadamu utu na heshima yake. Wadau wote wanahamasishwa na Mama Kanisa ili kuhakikisha fursa za ajira, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinalindwa na kuendelezwa. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wadau wote katika ulimwengu wa kazi kujizatiti ili kuhakikisha kwamba watu wanapata fursa za ajira mintarafu ujuzi na maarifa yao; kwa kuzingatia wajibu na dhamana ya wafanyakazi kwa ajili ya familia zao na jamii katika ujumla wake. Ni katika muktadha huu, kuna haja ya kuendeleza miradi inayonogesha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, hasa kwa maskini na wanyonge ndani ya jamii. Mama Kanisa anapenda kuonesha uwepo wake endelevu na mshikamano wa dhati na wale wote wanaokabiliwa na ukosefu na wasi wasi wa fursa za ajira kutokana na kuyumba kwa uchumi Kitaifa na Kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha ujumbe wake kwa kuwaweka wafanyakazi wote chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi.

Kwa upande wake, Askofu Giuseppe Piemontese, OFM, Conv. wa Jimbo Katoliki la Terni-Narni-Amelia, Italia, amekazia kuhusu Injili ya matumaini kwa wale wote waliopondeka na kuvunjika moyo. Janga la UVIKO-19 iwe ni fursa ya kupyaisha maendeleo jamii na maisha ya kiroho. Maeneo ya kazi, wafanyakazi na viongozi katika ngazi mbalimbali, majadiliano katika ukweli na uwazi yapewe kipaumbele cha pekee ili kuondokana na migogoro kazini. Wafanyakazi waboreshe maisha yao kwa sala na maadhimisho ya Sakramenti mbalimbali za Kanisa, huku wakiendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki jamii, utu na heshima ya binadamu.

40 Yrs Terni

 

17 May 2021, 14:39