Baba Mtakatifu Francisko kwa barua yake binafsi "Motu Proprio" Antiquum ministerium" ameanzisha huduma ya Katekista ndani ya Kanisa, lakini kimsinhi hii ni huduma kale! Baba Mtakatifu Francisko kwa barua yake binafsi "Motu Proprio" Antiquum ministerium" ameanzisha huduma ya Katekista ndani ya Kanisa, lakini kimsinhi hii ni huduma kale! 

Papa: Barua Binafsi: Antiquum Ministerium: Utume wa Katekista

Changamoto za uinjilishaji wa kina katika ulimwengu wa utandawazi zimepelekea hata Baba Mtakatifu tarehe 11 Mei 2021 kuchapisha Barua Binafsi "Motu Proprio" ujulikanao kama "Antiquum ministerium" yaani "Huduma Kale". Lakini ikumbukwe kwamba, hii si huduma mpya kabisa kwa watu wa Mungu kwani huduma ya makekista imekuwepo tangu kale. Hawa ni mashuhuda wa imani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kwa Barua yake Binafsi "Motu Proprio", "Antiquum ministerium" yaani “Huduma kale” ameanzisha Huduma ya Katekista ambayo kimsingi ni huduma kale. Maandiko Matakatifu yanataja huduma mbalimbali zinazotolewa na Mama Kanisa. Mwenyezi Mungu katika Kanisa ameweka: Mitume, Manabii, Walimu, watenda miujiza pamoja na watu waliokirimiwa karama mbalimbali za Roho Mtakatifu. Rej. 1Kor. 12:28-31. Mwinjili Luka katika utangulizi wa Kitabu cha Matendo ya Mitume anaelezea umuhimu wa mafundisho yake kwa Wakristo na kwamba, kuna haja ya kushirikishana tunu msingi za maisha kama alama na matunda ya Katekesi ya kweli. Karama mbalimbali ndani ya Kanisa zilipania kutoa huduma kwa ajili ya Jumuiya yaani “Diakonia”. Mtakatifu Paulo Mtume, anatambua Karama za Roho Mtakatifu na tofauti zake, lakini zote zinapata chanzo na asili yake kutoka kwa Roho Mtakatifu anayemgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye! Rej. 1Kor. 12: 4-11.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakiri kwamba, kuna mafundisho ambayo Mitume waliwarithisha baadhi ya waamini na kuwasihi kuyahifadhi Mapokeo waliyopokea, wapiganie imani, ili Kanisa liweze kuishi katika utakatifu na kukuza imani. Mama Kanisa anakiri kwa dhati kabisa kwamba, huduma hii imesaidia katika utume wa uinjilishaji na kwamba, Kanisa katika ulimwengu mamboleo linapongeza njia mbalimbali zinazoendelea kujitokeza ili kuliwezesha Kanisa lenyewe liendelee kuwa aminifu kwa Neno la Mungu, ili kwamba, Injili Takatifu iweze kuhubiriwa kwa kila kiumbe. Katika kipindi cha miaka elfu mbili iliyopita, wameonesha ufanisi mkubwa katika utume wao. Wakleri na watawa wameendelea kujisadaka kwa ajili ya kufundisha Katekesi, ili kwamba imani iweze kuwa ni chombo madhubuti cha kuimarisha imani kwa watu wote. Kuna baadhi ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ambayo yameendelea kujipambanua kwa ajili ya kufundisha Katekesi.

Mama Kanisa anawakumbuka kwa heshima na taadhima waamini walei waliojisadaka usiku na mchana kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu kwa njia ya mafundisho ya Katekesi. Hawa ni watu waliokuwa na imani thabiti na mashuhuda wa utakatifu wa maisha, baadhi yao wakaanzisha Makanisa na wengine kuitupa mkono dunia kwa njia ya ushuhuda wa kifodini. Hata leo hii, kuna Makatekista mashuhuri ambao ni viongozi wa Jumuiya zao na wanasaidia pia kurithisha na ukuzaji wa imani. Kuna jeshi kubwa la wenyeheri, watakatifu na mashuhuda ambao ni Makatekista waliolisongesha mbele Kanisa na kwa hakika wanahitaji kutambuliwa, kwa sababu wao ni utajiri mkubwa na amana ya Katekesi pamoja na historia nzima ya tasaufi ya Kikristo.

Tangu baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Mama Kanisa ameendelea kupyaisha shukrani zake kutokana na kuwahusisha watu wengi zaidi katika mchakato wa uinjilishaji, wengi wao wakiwa ni waamini walei. Hawa wamejitahidi kutumia karama na mapaji yao, kiasi kwamba, wanaweza kuitwa kuwa ni “Plantatio Ecclesiae” yaani “shamba la Kanisa” pamoja na ustawi wa Kanisa. Kanisa linawashukuru na kulipongeza Jeshi la Makatekista ambalo limekuwa mstari wa mbele kutangaza, kushuhudia na kurithisha imani ya Kanisa kwa njia ya kazi zao kubwa. Katika nyakati hizi, ambapo wakleri ni wachache sana wa kuhubiri Habari Njema ya Wokovu kwa watu wengi hivi pamoja na kuendelea na shughuli za kichungaji, wajibu na dhamana ya Makatekista ni kubwa zaidi. Rej. AG 17.

Mama Kanisa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, ameendelea kupyaisha Katekesi na hasa zaidi kwa kuchapisha Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki: muhtasari wa Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala. Wosia wa Kitume wa “Cateches Tradendae, na Miongozo ya Katekesi ni kielelezo makini kuonesha umuhimu wa Katekesi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa elimu na majiundo endelevu kwa waamini. Ikumbukwe kwamba, Askofu mahalia kimsingi ndiye Katekista wa kwanza, akisaidiwa na wakleri wake pamoja na waamini walei wanaoshiriki utume huu kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Jitihada zote hizi zinazoonesha umuhimu wa mchakato wa uinjilishaji katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, ili kuleta mabadiliko yanayokusudiwa. Uaminifu kwa mambo ya kale na uwajibikaji kwa mambosasa ni masharti muhimu kwa Kanisa kuweza kuendeleza utume wake katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Roho Mtakatifu anaendelea kuita na kuwatuma watu ili waweze kukutana na watu wa Mungu wanaosubiri kugundua: uzuri, wema na ukweli wa imani ya Kikristo.

Ni jukumu la wachungaji wa Kanisa kuwaunga mkono katika mchakato huu, kwa kutajirisha maisha ya Jumuiya ya Kikristo kwa kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa, ili waweze kupenyeza tunu msingi za maisha ya Kikristo katika jamii, siasa na sekta ya uchumi. Ikumbukwe kwamba, waamini walei hapa ni wale waamini wote isipokuwa wale wenye Daraja Takatifu, na wenye hali ya kitawa iliyokubaliwa na Kanisa. Tabia ya kidunia ndiyo tabia halisi na pekee kwa waamini walei. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, ni juu ya walei, kutokana na wito wao, kuutafuta ufalme wa Mungu wakiyashughulikia mambo ya dunia na kuyaelekeza kadiri ya Mungu, wakijitahidi kuyatakatifuza malimwengu kama kutoka ndani, mithili ya chachu, katika kuyatimiza majukumu yao wenyewe, wakiongozwa na roho ya kiinjili, hivyo wamshuhudie Kristo kwa wengine, waking’aa hasa kwa ushuhuda wa maisha yao, imani, matumaini na mapendo. Waamini walei wanaweza kushirikishwa zaidi katika maisha na utume wa Kanisa kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mtume.

Makatekista wanaitwa kuwa ni wataalamu na wahudumu wa jumuiya ya waamini katika kutangaza, kushuhudia na kurithisha imani katika hatua mbalimbali. Waanzie hatua ya kwanza ya kutangaza Injili, “Kerygma”, kufundisha maisha mapya katika Kristo Yesu sanjari na kuwandaa waamini kwa ajili ya kupokea Sakramenti za Kanisa na hatimaye, kuendelea na majiundo endelevu ili kila mwamini aweze kuwa tayari siku zote kumjibu kila mtu anayemuuliza habari za tumaini lililo ndani mwake; lakini kwa upole na kwa hofu. Rej. 1Pet.3:15. Makatekista wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa imani, waalimu, wandani wa imani na walimu wanaofundisha kwa niaba ya Kanisa. Yote haya yanaweza kutekelezwa kwa njia ya sala, masomo na ushiriki wa moja kwa moja katika maisha ya jumuiya yanayoweza kukuza utambulisho na uwajibikaji wake wote.

Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake Binafsi "Motu Proprio" "Antiquum ministerium" yaani “Huduma kale” anaendelea kukazia mabadiliko yaliyofanywa na Mtakatifu Paulo VI katika Waraka wake wa Kitume “Ministeria Quaedam” akifanya rejea katika huduma hii kwa Kanisa Katoliki, aliyaita madaraja haya kuwa ni “Madaraja madogo” na kufafanua shughuli na malengo yake. Madaraja ya Huduma ya Neno na Utumishi Altareni. Huduma zote hizi lazima zilenge katika kujenga na kukuza umoja wa Kanisa kwa kuishi kiliturujia, huduma kwa maskini, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, daima wakiwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake binafsi, Motu Proprio “Spiritus Domini” yaani “Roho wa Bwana”: Utume wa Waamini Walei kutoka katika Ubatizo”, amefanya mabadiliko katika kanuni namba 230 kifungu cha 1 cha Mkusanyiko wa Sheria za Kanisa na hivyo kutoa ruhusa kwa wanawake kuweza kushiriki katika huduma ya usomaji na utumishi Altareni.

Huduma nyingine zinazoweza kutolewa na waamini walei ni pamoja na kuanzisha ofisi za: Wahudumu, Wapunga Pepo na Makatekista. Huduma zote hizi zinapaswa kupata chimbuko lake katika Mapokeo hai ya Kanisa. Hadhi na utume wa waamini walei vimekuwa vinaendelea kutambuliwa zaidi katika Kanisa. Kanisa linaweza kuwategemea waamini walei wengi japokuwa bado idadi hii bado si ya kutosha sana; walei wanaotambua umuhimu wa jumuiya na uaminifu mkubwa kwa shughuli za mapendo, katekesi na maadhimisho ya mafumbo ya imani. Lakini, daima wanapaswa kukumbuka kwamba, wao ni waamini walei. Huduma hii ina mwelekeo wa wito maalum na madhehebu yake ya kuingizwa, kumbe, Askofu mahalia anapaswa kufanya mang’amuzi ya dhati kadiri mahitaji msingi ya Kanisa mahalia. Watu wanaoitwa na kusimikwa kuwa Makatekista wanapaswa kuwa ni watu wenye imani thabiti, ukomavu wa hali ya juu, washiriki wakamilifu katika maadhimisho ya mafumbo ya Kanisa. Wawe ni wakarimu na wenye uwezo wa kujenga na kudumisha mahusiano ya umoja na udugu wa kibinadamu.

Ili Makatekista waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu wanapaswa kupewa mafundisho ya: Maandiko Matakatifu, Taalimungu, Shughuli za Kichungaji, kozi ya ualimu na ufundishaji, ili hatimaye, wawe ni watangazaji mahiri wa kweli za kiimani na wawe wamejipatia mafundisho ya awali ya Katekesi. Makatekista watarajiwa wawe ni wahudumu waaminifu na wanaoweza kushirikiana kwa karibu zaidi na mapadre pamoja na mashemasi, tayari kutekeleza dhamana na wajibu wao, mahali popote pale watakapotakiwa kwenda, huku wakichangamotishwa na ukweli wa hali ya kitume! Na kwa maneno haya, Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha rasmi Huduma ya Makatekista na madhehebu ya kuingizwa kwao yataandaliwa na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Mabaraza ya Maaskofu Katoliki yataanzisha mchakato wa majiundo makini, sheria na kanuni zitakazotakiwa kufuatwa mintarafu Barua Binafsi "Motu Proprio" "Antiquum ministerium" yaani “Huduma kale”.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanawakumbusha Maaskofu kwamba, “Maana wachungaji wanajua kwamba hawakuasisiwa na Kristo ili wajitwalie peke yao utume wote wenye wokovu ambao Kanisa liliupokea kwa ajili ya ulimwengu, bali kwamba huduma yao tukufu ndiyo kuwachunga waamini na kutambua huduma zao na karama zao, ili wote, kila mmoja kadiri ya kipaji chake, wasaidiane kwa pamoja katika kazi moja” LG 30. Mwishoni kabisa, Baba Mtakatifu Francisko anawasihi Maaskofu kutekeleza wosia huu katika shughuli zao za kichungaji, ili huduma ya Makatekista iweze kupata ufanisi na kukua katika jumuiya zao. Utekelezaji wa Barua Binafsi "Motu Proprio" "Antiquum ministerium" yaani “Huduma kale” unaanza mara moja baada ya kuchapishwa kwenye Gazeti la L’Osservatore Romano na hatimaye kwenye “Acta Apostolicae Sedis”.

Papa Huduma Kale
11 May 2021, 15:09