Mwenyeheri Rosario angelo Livatino ni shuhuda wa haki na imani iliyomsukuma kutenda kwa ushupavu bila kuogopa vitisho vya makundi ya kigaidi ya Mafia. Mwenyeheri Rosario angelo Livatino ni shuhuda wa haki na imani iliyomsukuma kutenda kwa ushupavu bila kuogopa vitisho vya makundi ya kigaidi ya Mafia. 

Mwenyeheri Rosario A. Livatino: Shuhuda wa Haki na Imani

Mwenyeheri Rosario A. Livatino ni shuhuda aliyeyamimina maisha yake kwa ajili ya haki na imani. Katika huduma yake kwa watu wa Mungu alijikita zaidi katika kutoa haki kama Hakimu na kamwe hakuruhusu rushwa na ufisadi vimtawale. Alijielekeza kutoa hukumu bila kulaani, ili kumpatia mkosaji nafasi ya kumwongokea Mungu kwa kuacha njia zake mbaya. Haki na Imani Poa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, Jumapili tarehe 9 Mei 2021 kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko amemtangaza Mtumishi wa Mungu Rosario Angelo Livatino kuwa ni Mwenyeheri. Ibada ya Misa Takatifiu imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Agrigento nchini Italia. Mwenyeheri Rosario Angelo Livatino, aliuwawa kikatili na Kikundi cha Mafia huko Stidda tarehe 21 Septemba 1990, akiwa na umri wa miaka 38 tu ya kuzaliwa. Atakuwa anaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo 29 Oktoba. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Jumapili tarehe 9 Mei 2021 amemtaja Hakimu Rosario Angelo Livatino kuwa ni shuhuda aliyeyamimina maisha yake kwa ajili ya haki na imani. Katika huduma yake kwa watu wa Mungu katika ujumla wao, lakini alijikita zaidi katika kutoa haki kama Hakimu na kamwe hakuruhusu rushwa na ufisadi vitawale maisha yake. Alijielekeza zaidi katika kutoa hukumu bila kulaani, ili kumpatia mwamini nafasi ya kutubu na kumwongokea Mungu kwa kuacha njia zake mbaya. Daima alijiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu.

Ni katika muktadha huu, Mwenyeheri Rosario Angelo Livatino, akabahatika kuwa ni shuhuda wa Injili ya Kristo hadi mauti ya kishujaa yalipomfika! Mwenyeheri Rosario Angelo Livatino ni mfano bora wa kuigwa na waamini wote lakini zaidi na Mahakimu pamoja na wafanyakazi wote wa Mahakama, ili waweze kusimama kidete kulinda na kudumisha utawala wa sheria na uhuru wa kweli. Kutokana na maambukizi makubwa ya Virusi vya Ugonjwa wa Korona, UVIKO-19, idadi kubwa ya waamini kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Agrigento wameifuatilia kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Katika mahubiri yake, Kardinali Marcello Semeraro, amesema kwamba, Mwenyeheri Rosario Angelo Livatino alifariki dunia huku akiwasamehe watesi na wauaji wake. Haki na imani ilikuwa ndiyo dira ya maisha yake. Alipenda kuona kwamba, haki inatekelezwa kwanza kwa njia ya ushuhuda wa wale waliokuwa wamepewa dhamana ya kuhakikisha kwamba, haki inatendeka.

Mwenyeheri Livatino alipenda sana kuandika katika nyaraka zake, “STD na kirefu chake “Sub Tutela Dei” yaani “Chini ya Ulinzi Safi wa Mungu na wakati mwingine, mambo yalipomzidia aliweka alama ya Msalaba. Alisikitika kuona kwamba, licha ya sadaka kubwa aliyokuwa anaitoa katika Mahakama, lakini bado watu walimgeuzia kisogo. Ni Hakimu ambaye hakupenda kulaani, bali alitoa nafasi kwa watuhumiwa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Ni kweli watu wengi waliweza kuongoka kutokana na mfano bora wa maisha yake yaliyokuwa yanamwilishwa katika matendo mema. Huu ndio ushuhuda wenye mvuto na mashiko kama ambavyo aliwahi kusema Mtakatifu Paul VI. Mwenyeheri Rosario Angelo Livatino mwaminifu wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Haya ni mauaji ya kikatili dhidi ya mfanyakazi wa Serikali, lakini zaidi ni mauaji ya Hakimu Mkatoliki aliyejipambanua katika kulinda na kutetea utawala wa sheria, maadili na utu wema. Ni mwamini aliyesimamia tunu za Kiinjili na kamwe hakuruhusu rushwa na ufisadi viguse na kutawala maisha yake. Ameshuhudia kwamba, Injili ya Kristo Yesu haichangamani hata kidogo na matendo ya kikatili yanayofanywa na vikundi vya Mafia.

Naye Kardinali Francesco Montenegro, Askofu mkuu wa Jimbo Katoliki la Agrigento, Italia anasema, ilikuwa ni tarehe 9 Mei 1993, kwenye uwanda wa bonde la Templi, Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, baada ya kukutana na kuzungumza kwa faragha na wazazi wa Mwenyeheri Rosario Angelo Livatino, akatamka wazi kwamba, wale wote wanaojihusisha na Mafia, watubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, kwani “Siku ya Mwisho, hakutakuwa na cha salia Mtume”! Kardinali Francesco Montenegro amewakumbuka na kuwaombea Mahakimu, wafanyakazi katika vikosi vya ulinzi na usalama, wanasiasa pamoja na raia wema waliopoteza maisha yao kutokana na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na makundi ya kigaidi. Italia bado inaendelea kuathirika kutokana na vitendo vya kigaidi vinavyofanya na Mafia.

Mwenyeheri Livatino
10 May 2021, 15:36