Mwenyeheri Padre Francis maria wa Msalaba: Muasisi wa Shirika la Mungu Mwokozi maarufu kama Waslvatoriani anakumbukwa kwa: Kukazia: Maandiko Matakatifu, Wokovu kwa Wote na Umoja wa Kitume! Mwenyeheri Padre Francis maria wa Msalaba: Muasisi wa Shirika la Mungu Mwokozi maarufu kama Waslvatoriani anakumbukwa kwa: Kukazia: Maandiko Matakatifu, Wokovu kwa Wote na Umoja wa Kitume! 

Mwenyeheri Francis Maria wa Msalaba Jordan: Neno, Wokovu na Umoja

Mwenyeheri Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan katika maisha na utume wake alikazia mambo yafuatayo: Tafakari ya kina ya Maandiko Matakatifu; Kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa ajili ya wokovu wa watu wote; Wakristo wote wanaitwa na kuhimizwa kujenga umoja na mshikamano wa kitume ili kutangaza na kushuhudia matendo makuu katika maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kardinali Angelo Di Donatis, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 15 Mei 2021 amemtangaza Mtumishi wa Mungu Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan kuwa ni Mwenyeheri. Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Lateran. Akichochewa na bidii na ari ya maisha ya kitume na kiu ya kumfanya Yesu Kristo ajulikane na kupendwa na watu wote kama Mwokozi wa ulimwengu, alianzisha Shirika Fundishi la Kitume mnamo 1881 mjini Roma. Mnamo mwaka 1883 alibadilisha kazi yake ya kitume na kuifanya kuwa ni taasisi ya kidini na yeye mwenyewe kuchukua jina la kitawa Francis Maria wa Msalaba Jordan. Kutoka Shirika Fundishi la Kitume kulianzishwa Shirika la Mungu Mwokozi yaani Wasalvatorian kunako mwaka 1881. Na Shirika la Masista wa Mungu Mwokozi yaani Masista Wasalvatorian kunako mwaka 1888, wakifuatana na vikundi vilivyoandaliwa vya waamini walei. Lengo lilikuwa ili katika kuyatimiza majukumu yao wenyewe, wakiongozwa na roho ya Kiinjili, na hivyo wamdhihirishe Kristo Yesu kwa wengine, waking’aa hasa kwa ushuhuda wa maisha yao, imani, matumaini na mapendo.

Mwenyeheri Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan alifariki dunia tarehe 8 Septemba 1918 huko Tafers, Uswiss. Alitangazwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Mtumishi wa Mungu, tarehe 14 Januari 2011. Na kaburi lake liko kwenye Makao makuu ya Shirika, hatua chache tu, kutoka kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Mama Kanisa anamtambua kwamba, kwa njia ya neema ya Mwenyezi Mungu, amekufa, akazikwa na kufufuka na Kristo Yesu na sasa anaishi naye miongoni mwa wenyeheri na watakatifu wa Mungu. Kardinali Angelo Di Donatis katika mahubiri yake amekazia mambo makuu matatu yaliyojitokeza katika maisha na utume wa Mwenyeheri Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan kuwa ni: Tafakari ya kina ya Maandiko Matakatifu; Kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa ajili ya wokovu wa watu wote; Wakristo wote wanaitwa na kuhimizwa kujenga umoja na mshikamano wa kitume ili kutangaza na kushuhudia matendo makuu katika maisha yao. Mwenyeheri Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan aliwahimiza wanashirika wake, kujikita katika tafakari ya kina ya Neno la Mungu, kama mwanga unaoyaangazia mapito ya maisha yao.

Tafakari ya kina ya Neno la Mungu ni msingi thabiti wa mchakato wa uinjilishaji. Huu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu unaodhihirisha kazi ya ukombozi. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, msingi wote wa uinjilishaji ni Neno la Mungu ambalo watu hulisikiliza, hulitafakari, huliishi, huliadhimisha na hulitolea ushuhuda. Maandiko Matakatifu ni chanzo hasa cha uinjilishaji. Na kwa njia hii, Kanisa linainjilisha na kuinjilishwa. Hiki ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu unarutubishwa kwa tafakari ya kina ya Neno la Mungu. Mwenyeheri Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan, alitamani kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu ili watu wote waweze kuokoka. Kwa njia ya uinjilishaji unaofumbatwa katika Neno la Mungu sanjari na malezi na majiundo makini ya Kikristo. Huu ndio utume na dhamana ya familia ya Wasalvatoriani hata katika ulimwengu mamboleo. Alitamani kuona watu wote duniani wanakombolewa, na kama alivyojitahidi kutekeleza Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Huu ni uinjilishaji unaokita mizizi yake katika huduma ya upendo wa dhati. Huu ni mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Ni mwaliko wa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kutenda kama anavyotaka. Neno la Mungu liguse undani wa maisha ya watu ili kuwaondolea utupu unaomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Watu wa Mungu wanapaswa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda upeo na anawataka wote waokoke na hatimaye, kuingia mbinguni. Ili kuweza kufikia lengo hili kuna haja kwa waamini kujazwa na upendo wa Mungu unaoshuhudiwa kwa maneno, lakini zaidi kwa matendo! Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka, huku wakiyaelekeza macho yao mbinguni. Mama Kanisa katika Sala ya Mageuzo anaomba kwa unyenyekevu, Roho Mtakatifu, ili awafanye kuwa ni jamaa moja, wale wote wanaoshiriki Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu. Kardinali Angelo Di Donatis anasema, Wakristo wote wanaitwa na kuhimizwa kujenga umoja na mshikamano wa kitume ili kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha yao, huku wakiongozwa na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, ili wote waweze kuwa wamoja katika Kristo Yesu.

Mwenyeheri Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan, alitaka wafuasi wake waunganishwe na kuwa wamoja katika utume, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kristo Yesu ni ufunuo wa Mungu Mwokozi. Karama ya Shirika ilipaswa kuwa ni kiungo muhimu cha shughuli zote za kitume zilizotekelezwa na kushuhudiwa na Wasalvatoriani. Leo hii, Wasalvatorian wameenea sehemu mbalimbali za dunia, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Mwinjilishaji mkuu ni Roho Mtakatifu anayewaunganisha na kuwakirimia ari na moyo wa umoja na mshikamano kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Mwanga wa Mwenyeheri Padre Francis Maria wa Msalaba Jordan na upendo wake, vitangazwe na kushuhudiwa sehemu mbalimbali za dunia, ili watu wengi zaidi waweze kuuona mwanga wa Kristo Yesu Mfufuka!

Katika Ibada hii ya Misa Takatifu, ameshiriki pia Kardinali Stanisław Dziwisz, Katibu muhtasi wa Mtakatifu Yohane Paulo II kwa muda wa zaidi ya miaka 40. Wameshiriki viongozi wakuu, mapadre, watawa na waamini walei wa matawi yote ya Wasalvatorian. Wameshiriki pia Waseminari wa Wasalvatorian. Ni kwa bahati mbaya sana, Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake, hakuweza kuhudhuria tukio hili muhimu sana katika historia na maisha ya Wasalvatorian, ambao amefanya nao kazi za kitume kwa miaka mingi!

Mwenyeheri Padre Francis
15 May 2021, 15:23