Wenyeheri Maria Pilar Gullòn Yturriaga na wenzake ni mashuhuda wa Injili ya huduma ya upendo Wenyeheri Maria Pilar Gullòn Yturriaga na wenzake ni mashuhuda wa Injili ya huduma ya upendo  

Mwenyeheri Maria Pilar G. Y. na Wenzake Mashuhuda wa Injili

Wenyeheri wapya: Maria Pilar Gullón Yturriaga, Octavia Iglesias Blanco na Olga Pérez-Monteserín Núñez, ni waamini walei, wanawake wa shoka, waliojisadaka kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema. Waliwahudumia majeruhi wa vita na kuwasaidia kupambana na maisha wakati wa hatari bila kuwatelekeza. Kanisa linamshukuru Mungu kwa ushuhuda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican. 

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, katika maadhimisho ya Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, Jumapili tarehe 30 Mei 2021 amesema kwamba, Wenyeheri wapya: Maria Pilar Gullón Yturriaga, Octavia Iglesias Blanco na Olga Pérez-Monteserín Núñez, ni waamini walei, wanawake wa shoka, waliojisadaka kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema. Waliwahudumia majeruhi wa vita na kuwasaidia kupambana na maisha wakati wa hatari bila kuwatelekeza. Walihatarisha sana maisha yao, lakini hatimaye, wakauwawa kikatili kutokana na chuki za kidini “Odium Fidei”. Mama Kanisa anamshukuru Mungu kwa kulijalia mashuhuda wa Injili ya huduma ya upendo!

Watumishi wa Mungu: María Pilar Gullón Yturriaga (1911-1936), alitekeleza utume wake kama dada wa nyumbani, akiwahudumia wazazi wake waliokuwa ni wazee. Alijisadaka bila ya kujibakiza katika shughuli mbalimbali za kitume Parokiani kwake, kwa ajili ya ustawi wa jamii, akauwawa kutokana na chuki ya dini “Odium Fidei” akiwa na umri wa miaka 25. Mtumishi wa Mungu Octavia Iglesias Blanco (1894-1936) alizaliwa na kulelewa kwenye familia ya Kikristo, akajisadaka kwa ajili ya huduma kwa wazazi wake. Na kwa ridhaa ya Mama yake mzazi, alipata kibali kwenda mstari wa mbele wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe ili kuwahudumia wagonjwa na majeruhi wa vita, akauwawa kikatili kwa sababu za chuki za kidini, akiwa na umri wa miaka 41.

Mtumishi wa Mungu Olga Pérez-Monteserín Núñez (1913-1936), alijitosa kwa ajili ya kazi za nyumbani, alikuwa msanii na mchoraji wa picha, aliuwawa kikatili akiwa na umri wa miaka 23. Hawa waamini walei na wauguzi wa Chama cha Msalaba Mwekundu waliouwawa kikatili wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Hispania, tarehe 29 Mei 2021 wametangazwa kuwa ni Wenyeheri. Ibada hii ya Misa Takatifu kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, imeadhimishwa na Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu Jimboni Astorga nchini Hispania na wanajulikana kama Wenyeheri wa Mashahidi wa Astorga kwani wamevikwa taji la maisha ya uzima wa milele, kwa sababu wenyeheri hawa wapya wamepewa uwezo wa kufanyika kuwa ni watoto wa Mungu, kwa kuliamini jina lake. Rej. Yn 1:12.

Kardinali Marcello Semeraro, katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa waamini kujivika fadhila ya ujasiri ili kuondokana na woga sanjari na kuendelea kuwasha moto wa upendo katika huduma makini. Kamwe woga na hofu visiwe ni vigezo katika maisha ya waamini, bali wawe na ujasiri na kusimama kidete kulinda na kutetea kile wanacho amini, kama sehemu ya mchakato wa kukuza mahusiano na mafungamano kati ya waamini na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao. Mashuhuda wa imani, daima waliweza kushinda woga kwa kuwasha moto wa upendo. Katika kipindi hiki cha janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO -19, waamini wanahamasishwa kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu kwa njia ya huduma makini, sala na majitoleo. Hii inatokana na ukweli kwamba, Mwenyezi Mungu yuko karibu, kati pamoja nao, amana, urithi na utajiri walioarithi kama waamini kutoka kwa Kristo Yesu.

Wenyeheri María Pilar Gullón Yturriaga, Octavia Iglesias Blanco pamoja na Olga Pérez-Monteserín Núñez, licha ya mateso, madhulumu na ubaya wa moyo, lakini waliendelea kuwasha moto wa upendo uliopenyeza na hata kuwafikia majeruhi wa vita. Hawa walikuwa ni wauguzi wa Chama cha Msalaba Mwekundu mjini Astorga, wakaonesha ushuhuda wa utimilifu wa upendo kiasi cha kumwaga damu yao kwa ajili ya upendo wa dhati kwa Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake. Ushuhuda wa maisha ni sehemu muhimu sana kwa Wakristo. Wenyeheri wapya, walikuwa na ujasiri sana kiasi cha kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa na majeruhi wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Hispania. Mababa wa Kanisa wanakumbusha kwamba, mwili wa mtu umepewa hadhi ya kushiriki “sura ya Mungu” ni mwili wa mtu hasa kwa kuwa unahuishwa na mtima wa kiroho, na ni nafsi yote kabisa ya mtu iliyonuiwa kuwa hekalu la Roho Mtakatifu ndani ya mwili wa Kristo. Rej. KKK 364. Wenyeheri wapya walijisadaka kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, kiasi hata cha wao wenyewe kuhatarisha maisha yao; kwa kunyanyaswa, kudhulumiwa na hatimaye, kuuwawa kikatili kwa sababu ya kutenda mema. Waliitupa mkono dunia, huku wakimtukuza Kristo Yesu Mfalme wa ulimwengu, kiri ya imani ambayo imewastahilisha kutangazwa kuwa ni Wenyeheri!

Wenyeheri Hispania

 

30 May 2021, 15:40