Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amezindua rasmi Jukwaa la kazi la Laudato si, safari ya miaka ya saba ya mafungamano na ushirikishwaji kwa ajili ya kutunza mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko amezindua rasmi Jukwaa la kazi la Laudato si, safari ya miaka ya saba ya mafungamano na ushirikishwaji kwa ajili ya kutunza mazingira nyumba ya wote. 

Mwaka wa Laudato si: Jukwaa la Kazi la Laudato si! Mpango Mkakati

Jukwaa la Kazi la Laudato si ni Safari ya Miaka Saba inayojikita katika: mwono wa ekolojia fungamani, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini; kwa kujielekeza katika uchumi unaosimikwa katika ekolojia; kwa kujikita katika mtindo wa maisha ya kawaida sanjari na kuendelea kukazia elimu na tasaufi ya ekolojia pamoja na ushirikishwaji wa jumuiya! Matumaini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki na amani kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Uliozinduliwa tarehe 18 Juni 2015 mjini Vatican. Baba Mtakatifu anapembua kuhusu madhara ya uharibifu wa mazingira, umuhimu wa wongofu wa kiekolojia na teknolojia rafiki kwa mazingira. Anazungumzia kuhusu haki ya maji safi na salama. Mazingira ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, urithi unaopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Utunzaji wa mazingira hauna budi kwenda sanjari na uwajibikaji na wala maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yasitumike kama nguvu ya kiuchumi kwa ajili ya kunyonya Mataifa mengine wala kuyatumbukiza katika utamaduni wa kifo. Nguvu ya fedha iwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jumuiya ya Kimataifa ijenge utamaduni wa kujadiliana, kuamua na kutenda kwa pamoja. Mapambano ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma ni muhimu, ili kujenga mtandao wa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Utunzaji wa mazingira nyumba ya wote ni mchakato unaokita mizizi yake katika uhalisia wa maisha ya kila siku.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kama sehemu ya kumbukizi la Miaka Mitano tangu alipochapisha Waraka wake wa Kitume, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” sanjari na uzinduzi wa Jukwaa la Kazi “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, anapenda kukazia yafuatayo: Kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha Maskini, Utunzaji bora wa mazingira na Jukwaa la kazi ili kutekeleza sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote katika kipindi cha miaka saba kuanzia sasa! Baba Mtakatifu anasema, kunako mwaka 2015 aliwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwa kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema rasilimali na utajiri wa dunia. Leo hii kuna uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote. Janga kubwa la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ni changamoto ya kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini. Kuna mwingiliano mkubwa kati ya afya bora na mazingira anamoishi binadamu. Hapa kuna haja ya kujikita katika wongofu wa kiekolojia kwa kubadili mtindo wa maisha kwa ajili ya ekolojia ya binadamu, tayari kujikita katika ujenzi wa jamii mpya!

Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya Kimataifa inao wajibu mkubwa kwa vizazi vijavyo, kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Huu ni mwaliko wa kuondokana na ubinafsi unaopelekea matumizi mabaya ya rasilimali na mali ya dunia. Ni wakati wa kujenga utamaduni wa kuheshimu zawadi ya kazi ya uumbaji, kwa kuwa na mtindo mpya wa maisha, unaothamini ekolojia, ili kuwaandaliwa vijana leo na kesho bora zaidi, ili kuwaachia bustani inayostawi na wala si jangwa linalokatisha tamaa. Baba Mtakatifu anawashukuru wadau mbalimbali walionogesha maadhimisho ya “Mwaka wa Laudato si” uliozinduliwa tarehe 24 Mei 2020 na kuratibiwa na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu. Kama sehemu ya mchakato wa kufunga rasmi maadhimisho ya “Mwaka wa Laudato si”, Baba Mtakatifu ametangaza kuzinduliwa kwa Jukwaa la Kazi la Laudato si “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, safari shirikishi ya miaka saba, kama sehemu ya mchakato wa kujizatiti kikamilifu katika maendeleo na ekolojia fungamani.

Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuzialika familia, parokia na majimbo; shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu, hospitali, maeneo ya biashara na mashamba makubwa; makundi na wanaharakati pamoja na taasisi za kidini kushirikiana na kushikamana, ili kufanya kazi kwa pamoja, ili kujenga jamii inayokita mizizi yake katika: udugu wa kibinadamu, amani na ulimwengu fungamani. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Safari ya Miaka Saba itaongozwa na: mwono wa ekolojia fungamani, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini; kwa kujielekeza katika uchumi unaosimikwa katika ekolojia; kwa kujikita katika mtindo wa maisha ya kawaida sanjari na kuendelea kukazia elimu na tasaufi ya ekolojia pamoja na ushirikishwaji wa jumuiya! Kuna matumaini makubwa na kama wengi watashiriki na kila upande kuchangia tamaduni, uwezo, uzoefu na mang’amuzi yake, dunia inaweza kubadilika na kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi kadiri ya mpango wa Mungu.

Papa Laudato si

 

 

25 May 2021, 15:16