Tafuta

Mama Kanisa tarehe 13 Mei 2021 anaadhimisha kumbukumbu ya Bikira Maria wa Fatima sanjari na kumbukizi la miaka 40 tangu jaribio la kutaka kumuua Mt. Yohane Paulo II liliponyika 13 Mei 1981. Mama Kanisa tarehe 13 Mei 2021 anaadhimisha kumbukumbu ya Bikira Maria wa Fatima sanjari na kumbukizi la miaka 40 tangu jaribio la kutaka kumuua Mt. Yohane Paulo II liliponyika 13 Mei 1981. 

Kumbukumbu Miaka 40 Jaribio la Mauaji ya Mt. Yohane Paulo II

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake kuhusu Fumbo la Sala, amewakumbusha waamini kwamba, katika kumbukumbu ya Bikira Maria wa Fatima, Mtakatifu Yohane Paulo II alikiri kwa imani kwamba, Bikira Maria wa Fatima ndiye aliyeokoa maisha yake wakati wa jaribio la kutaka “kumfyekelea mbali” kutoka katika uso wa dunia lililofanywa na Mehmet Ali Ağca. Imani Thabiti!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mama Kanisa tarehe 13 Mei ya kila mwaka anaadhimisha Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Fatima. Kwa mwaka 2021, Kanisa linafanya kumbu kumbu ya Miaka 40 tangu Jaribio la kutaka Kumuua Mtakatifu Yohane Paulo II lilipofanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ilikuwa ni tarehe 13 Mei 1981, siku ambayo Mtakatifu Yohane Paulo II alipouona mkono wa nguvu wa Bikira Maria ukitenda kazi katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake kuhusu Fumbo la Sala, amewakumbusha waamini kwamba, katika kumbukumbu ya Bikira Maria wa Fatima, Mtakatifu Yohane Paulo II alikiri kwa imani kwamba, Bikira Maria wa Fatima ndiye aliyeokoa maisha yake wakati wa jaribio la kutaka “kumfyekelea mbali” kutoka katika uso wa dunia lililofanywa na Mehmet Ali Ağca. Hili ni tukio anasema Baba Mtakatifu Francisko ambalo linawakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutambua kwamba, maisha na historia ya kila mwanadamu iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuungana pamoja naye, ili kulikabidhi Kanisa, ulimwengu na waamini katika ujumla wao, chini ya ulinzi na tunza ya Moyo Safi wa Bikira Maria.

Katika sala na sadaka zao, waendelee kumwomba Bikira Maria, aweze kuwaombea walimwengu amani na hatimaye, mwisho wa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Waamini waendelee kujikita katika toba na wongofu wa ndani. Katika hali ya kukata tamaa na mahangaiko katika sala, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumkimbilia Bikira Maria kwa ulinzi na tunza yake ya kimama! Sala ni silaha madhubuti katika mapambano ya maisha ya kiroho! Bila sala, hakuna ushindi dhidi ya dhambi na ubaya wa moyo! Rozari Takatifu ni muhtasari wa historia nzima ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Mwezi Mei ni muda muafaka wa kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, silaha za mapambano dhidi ya dhambi na ubaya wa moyo ni: Tafakari ya Neno la Mungu, Sala, Sakramenti ya Upatanisho pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Haya ni mambo msingi yanayomwezesha mwamini kuendelea katika safari ya maisha yake ya kiroho sanjari na ushuhuda wa Kikristo, kielelezo makini cha imani tendaji!

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Poland katika kumbukumbu ya Miaka 40 tangu jaribio la kutaka kumuua Mtakatifu Yohane Paulo II litokee, linaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama alama ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu. Kutakuwa na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na huo pia utakuwa ni mwanzo wa Ibada ya Rozari Takatifu itakayofanywa kwa kutembea kilometa 30, kielelezo cha maisha ya Kristo Yesu hapa duniani. Matukio yote haya yanapania kuchochea fadhila ya imani ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Leo hii, watu wengi wanakosa imani thabiti katika hija ya maisha yao hapa duniani!

Baba Mtakatifu Francisko aliwahi kusema, Kanisa katika ulimwengu mamboleo ni Kanisa la mashuhuda ambalo linaendelea kujengwa kutokana na damu ya watoto wake inayomwagika sehemu mbali mbali za dunia. Kuna watu wanauwawa, wanayanyaswa na kudhulumiwa kutokana na chuki za kidini. Huu ndio ukweli uliokuwa umefumbatwa katika ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima, yaani Francis, Lucia na Yacinta. Ni Siri inayogusa matukio ya kihistoria, maisha na utume wa Kanisa. Hata leo hii, Kanisa linaendelea kujaribiwa, kwa baadhi ya watu kutaka kujenga hisia za chuki na uhasama dhidi ya Kanisa pamoja na kupandikiza utamaduni wa kifo!

Bikira Maria alipowatokea watoto wa Fatima, aliwapatia Siri kuu tatu ambazo zote zimekwisha fafanuliwa na viongozi wa Kanisa kwa nyakati tofauti. Ni siri ambazo zimejikita katika mwono wa vita, majanga asilia, kinzani na migawanyiko kati ya watu. Siri zote hizi ziliandikwa na Sr. Lucia. Siri ya tatu hakikuweza kufunuliwa kutokana na amri iliyotolewa na Askofu mahalia. Mtakatifu Yohane Paulo II baada ya jaribio la kutaka kumuua kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican hapo tarehe 13 Mei 1981 aliamuru kwamba, siri ya tatu ifunuliwe na kuwekwa hadharani. Tafsiri ya siri hii ilitolewa na Kardinali Joseph Ratzinger, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la mafundisho tanzu ya Kanisa na alisema kwamba, siri ya tatu ya Fatima ilikuwa ni mwaliko kwa Wakristo kusoma alama za nyakati na kutoa majibu muafaka kwa njia ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Mtakatifu Yohane Paulo II anakiri kwamba, ni mkono na kinga ya Bikira Maria iliyomwezesha kusalimika katika jaribio la kutaka kumuua hapo tarehe 13 Mei 1981. Sala ni nguzo muhimu sana katika maisha dhidi ya wasi wasi wa kifo anasema Mtakatifu Yohane Paulo II.

Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa ni mwamini hodari na shupavu katika maisha na utume wake. Taa ya imani ilikuwa ni dira na mwongozo wa maisha yake, hata pale alipoonekana yupo kwenye mahangaiko ya kuugua kwa muda mrefu, lakini bado aliendelea kuwa ni mtu mwenye amani, furaha na utulivu wa ndani. Ni mwamini ambaye alikuwa safarini kuelekea kwenye maisha na uzima wa milele. Hiyo ni changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujiandaa kikamilifu ili kuweza kukabiliana na fumbo la kifo katika maisha yao. Ni mwaliko wa kuondokana na uchoyo na ubinafsi; kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hata baada ya jaribio la kutaka kumuua kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mnamo Mei 13 mwaka 1981, Mtakatifu Yohane Paulo II aliendelea na maisha na utume wake katika hali ya utulivu na amani ya ndani.

Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa na ibada ya pekee kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Kristo Yesu, kabla ya kukata roho, alipenda kuwakabidhi wanafunzi wake chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Ndiyo maana Mama huyu alikuwa na nafasi ya pekee sana katika maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II. Katika maisha kila mtu amekabidhiwa Msalaba wake, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Msalaba huu unakuwa ni chemchemi ya: msamaha, huruma, upendo na mwanga angavu wa maisha! Katika maisha na utume wake, Mtakatifu Yohane Paulo II, aligusa medani mbali mbali za maisha ya binadamu; akaimarisha mafundisho msingi ya Kanisa yanayofumbatwa katika huruma ya Mungu, Roho Mtakatifu, Uhusiano kati ya imani na akili; Ari na mwamko wa kimisionari ndani ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II, hata katika dakika zake za mwisho katika udhaifu wa mwili na magonjwa, aliendelea kuwa ni: Shuhuda, Nabii na Chombo cha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Akafanikiwa kuonesha ukuu, utakatifu, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Mt. Yohane Paulo II
12 May 2021, 15:23