Shirika la Wahubiri, Maarufu kama Wadominikani tarehe 6 Agosti 2021 linaadhimisha Kumbukizi la Miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Dominiko wa Guzmàn aliyejisadaka kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Shirika la Wahubiri, Maarufu kama Wadominikani tarehe 6 Agosti 2021 linaadhimisha Kumbukizi la Miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Dominiko wa Guzmàn aliyejisadaka kutangaza Habari Njema ya Wokovu. 

Kumbukizi la Miaka 800 Tangu Afariki Mt. Dominiko wa Guzmàn

Mtakatifu Dominiko wa Guzmán aliyepyaisha mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili. Alitangaza Injili iliyokita mizizi yake katika huruma ya upendo wa Mungu, ukweli unaokoa na kama chemchemi ya nguvu ya wokovu. Alikazia utume, umoja, maisha ya Kijumuiya na umisionari wa kitume.. Muda wa shukrani kwa mchango wa Wadominikani katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mtakatifu Dominiko wa Guzmán alizaliwa huko mjini Calarogo, ambao kwa sasa mji huu unajulikana kama Caleruega huko nchini Hispania tarehe 8 Agosti 1170. Alifariki dunia tarehe 6 Agosti 1221 na kuzikwa kwenye Kanisa kuu la “San Domenico Jimbo kuu la Bologna nchini Italia. Papa Gregori IX tarehe 2 Julai 1234 akamtangazwa kuwa ni Mtakatifu. Ni muasisi wa Shirika la Wahubiri, maarufu kama Wadominikani, “Order of Preacher, OP.” Ni katika muktadha huu, Mama Kanisa anapoadhimisha kumbukumbu ya Miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Dominiko wa Guzmán, Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia Barua, Padre Gerard Francisco Timoner, OP, Mkuu wa Shirika la Wadominikani. Katika barua hii, Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kulijalia Kanisa Mtakatifu Dominiko wa Guzmán aliyepyaisha mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili. Alitangaza Habari Njema ya Wokovu iliyokita mizizi yake katika huruma ya upendo wa Mungu, ukweli unaokoa na kama chemchemi ya nguvu ya wokovu. Alikazia utume, umoja, maisha ya Kijumuiya na umisionari wa kitume. Jubilei ya Miaka 800 tangu afariki dunia Mtakatifu Dominiko wa Guzmán ni muda wa shukrani kwa kwa mchango mkubwa unaoendelea kutolewa na Wadominikani katika maisha na utume wa Kanisa sehemu mbalimbali za dunia.

Mtakatifu Dominiko wa Guzmán anatambulika kuwa ni Mhubiri wa Neema ya Mungu inayokita mizizi yake katika karama na utume wa Shirika la Wadominikani: Mapadre, Watawa na Waamini Walei bila kuvisahau vyama vya vijana. Kila mtakatifu alikirimiwa utume maalum katika maisha yake kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Dominiko wa Guzmán aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili, utakatifu na kuendelea kukazia umoja na maisha ya kijumuiya kwa kuyaishi kikamilifu mashauri ya Kiinjili yaani: Ufukara, Utii na Useja kamili, chachu ya mageuzi makubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Hizi ni tunu msingi zilizowapambanua Wakristo wa Kanisa la Mwanzo. Mtakatifu Dominiko wa Guzmán alianzisha Jumuiya ya wahubiri, waliopenda kusoma na kuyatafakari Maandiko Matakatifu, wakajikita katika maisha matakatifu na adili na hivyo wakawa kweli ni mashuhuda wa chemchemi ya maisha na ukweli wa Neno la Mungu. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, Wadominikani wanaendelea kutoa changamoto kwa Wakristo kuwa kweli ni Mitume wamisionari, wanaokwenda pembezoni mwa jamii ili kutangaza na kushuhudia mwanga wa Injili na upendo wenye huruma kutoka kwa Kristo Yesu. Kiini cha Kanisa na ari na moto wa umisionari unaopaswa kuendelea kuwaka!

Mtakatifu Dominiko wa Guzmán alitangaza Habari Njema ya Wokovu iliyokita mizizi yake katika huruma ya upendo wa Mungu, ukweli unaokoa na kama chemchemi ya nguvu ya wokovu. Mtakatifu Dominiko wa Guzmán aliguswa na mateso na mahangaiko na vifo vya watu wa Mungu, akauza baadhi ya mali zake ili kujenga kituo cha huduma ya upendo, ili kushuhudia upendo wa Kristo Yesu unaoganga na kuponya. Alikazia umoja wa ukweli unaosimikwa katika upendo, nguzo ya haki msingi za binadamu, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa Kanisa kuendeleza urafiki na udugu wa kibinadamu, ili “kufyekelea” mbali mifumo tenge ya uchumi na siasa, tayari kujielekeza zaidi katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, haki na amani. Waamini wanahimizwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika utakatifu, haki na amani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mtakatifu Dominiko wa Guzmán katika maisha na utume wake, alikazia ujenzi wa jumuiya, ili kukuza na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu, kama kielelezo cha utawala bora. Ni utawala shirikishi uliofumbatwa katika mang’amuzi na maamuzi kadiri ya sheria, taratibu na kanuni za Shirika.

Kwa maneno mengine huu ni mchakato ambayo ulisimikwa katika msingi wa “dhana ya Sinodi”, ili kuwawezesha watu wengi wa Mungu kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa kama kielelezo cha umoja na udugu wa kibinadamu. Udugu wa Kiinjili ni ushuhuda wa unabii wa Mpango wa Mungu kama chombo cha umoja na upatanisho wa familia ya binadamu. Na huu ni utambulisho makini wa karama ya Wadominikani na kama sehemu ya mchakato wa kuragibisha upyaisho wa maisha ya Kikristo na utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu katika ulimwengu mamboleo! Mtakatifu Dominiko wa Guzmán na Mtakatifu Francisko wa Assisi walitambua kwamba, kutangaza Injili kunapaswa kwenda sanjari na ushuhuda wa ujenzi wa jumuiya ya kitawa inayosimikwa katika umoja wa kidugu na utume wa kimisionari. Watakatifu, wasanii na wasomi wa nyakati mbalimbali wametambua na kuthamini mchango wa Mtakatifu Dominiko wa Guzmán. Kifodini cha baadhi ya Wadominikani ni mahubiri ya nguvu, yenye mvuto na mashiko. Wamesimama kidete kutangaza Injili ya Kristo pembezoni mwa jamii, bila kusahau kuwashirikisha vijana ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ushiriki mkamilifu wa waamini walei katika utume wa uinjilishaji wa kina ni jambo linalopewa kipambele cha kwanza kwa nyakati hizi.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake mintarafu kumbukumbu ya Miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Dominiko wa Guzmán, kwa kuwashukuru Wadominikani waliojielekeza zaidi katika masomo ya taalimungu kwa kufafanua mafumbo ya imani kwenye vyuo mbalimbali vya taalimungu Barani Ulaya. Ni masomo, malezi na makuzi yanayokita mizizi yake katika: Maandiko Matakatifu, Taalimungu na Elimu dunia ili kusaidia mchakato wa majadiliano katika ukweli kwa ajili ya huduma ya Ufunuo wa Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. Wadominikani wamekuwa mstari wa mbele katika sekta ya elimu kwa kuanzisha taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu, ili kusaidia majadiliano kati ya akili na imani, ili kuendeleza maisha na utume wa Kanisa. Hiki ni kipindi cha kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa mchango mkubwa ambao umetolewa na Wadominikani kwa Vatican na Kanisa katika ujumla wake. Baba Mtakatifu anawaombea ili wadumu katika uaminifu wa karama ya Mwanzilishi wa Shirika lao, amana na urithi wa karama ya mwanzilishi wao, pamoja na ongezeko la miito mitakatifu ya kipadre na kitawa.

Mt. Dominiko 800 Yrs
25 May 2021, 08:02