Jukwaa la Vyama vya Kifamilia Nchini Italia linasema kwamba, kupungua kwa idadi ya watoto wanaozaliwa nchini Italia ni janga la kitaifa na kimataifa na hatari kwa siku za usoni! Jukwaa la Vyama vya Kifamilia Nchini Italia linasema kwamba, kupungua kwa idadi ya watoto wanaozaliwa nchini Italia ni janga la kitaifa na kimataifa na hatari kwa siku za usoni! 

Jukwaa la Vyama Vya Kifamilia Italia: Ukosefu wa Watoto ni Janga

Jukwaa la Vyama vya Kifamilia Nchini Italia limepembua: kuhusu hali ya jumla ya uzazi nchini Italia kwa kujielekeza zaidi katika mada zilizogusia kuhusu: kiwango cha uzazi chenye mvuto; vizazi vipya ni chanzo kizuri cha uwekezaji na kwamba, watoto ni uzuri unaopaswa kusimuliwa! Mkutano huu umefunguliwa na Papa Francisko pamoja na Prof. Mario Draghi, Waziri mkuu wa Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Jukwaa la Vyama vya Kifamilia Nchini Italia “Forum delle Associazioni Familiari” lilianzishwa kunako mwaka 1992 ili kuragibisha tunu msingi za maisha ya kifamilia nchini Italia, kama nguzo msingi ya jamii sanjari na kuendelea kujizatiti katika kulinda, kudumisha na kutegemeza familia. Jukwaa hili linaundwa na vyama 47 pamoja na majukwaa ya kimkoa 18 na hivyo kulifanya Jukwaa zima kuwa na jumla ya vyama 582. Kuna jumla ya familia milioni 4 ambazo ni wanachama na hivyo zinaunda ya watu milioni 12. Pamoja na mambo mengine, Jukwaa la Vyama vya Kifamilia Nchini Italia linapania maboresho ya maisha ya kifamilia, ili kuhakikisha kwamba, shughuli za kifamilia katika medani mbalimbali za maisha zinatekelezwa kikamilifu kwa kuzingatia sera makini za kifamilia. Jukwaa la Vyama vya Kifamilia Nchini Italia, Ijumaa tarehe 14 Mei 2021 limefanya mkutano wa siku moja ili kupembua kuhusu hali ya jumla ya uzazi nchini Italia kwa kujielekeza zaidi katika mada zilizogusia kuhusu: kiwango cha uzazi chenye mvuto; vizazi vipya ni chanzo kizuri cha uwekezaji na kwamba, watoto ni uzuri unaopaswa kusimuliwa!

Mkutano huu umefunguliwa na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Prof. Mario Draghi, Waziri mkuu wa Italia. Mkutano umeratibiwa na Bwana Gigi de Palo, Rais wa Jukwaa la Vyama vya Kifamilia Nchini Italia “Forum delle Associazioni Familiari” na viongozi mbalimbali wa Italia, wamechagia mawazo yao. Bwana Gigi de Palo, katika hotuba yake elekezi amebainisha kwamba, idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa nchini Italia ni janga la kitaifa na kimataifa linalosigana na mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Sera zinazopania kukuza na kudumisha tunu msingi za familia ni sehemu ya mchakato wa uwekezaji. Leo hii vijana wengi nchini Italia hawana mpango wa kupata watoto na wale waliotia nia hii, inaonekana kana kwamba, ni jambo linaloleta karaha kwenye familia na wala si jambo la kujivunia na watoto si tena amana na utajiri wa familia kama ilivyokuwa hapo awali. Ikumbukwe kwamba, watoto ni amana na utajiri wa jamii husika kwani hawa ndio watakaoendeleza uchumi wa kijani na maendeleo fungamani ya binadamu na wala hakuna mageuzi katika sekta mbalimbali za maisha bila ya uwepo wa vijana wa kizazi kipya.

Italia inakabiliwa na idadi kubwa ya wafanyakazi wanaokula pensheni, ikilinganishwa na vijana wanaozalisha na kutoa huduma. Watoto ni matumaini ya jamii kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, kumbe, inalipa kuwekeza kwa watoto. Umefika wakati kwa Italia kuwekeza katika sera bora za familia, ili kupata watoto zaidi. Jambo la msingi kwa wakati huu ni kufanya mabadiliko makubwa katika: miundombinu ya familia, kwa kuwekeza katika uzazi na kupandikiza mbegu ya matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Hakuna sababu ya kukata tamaa kutokana na hali ngumu ya uchumi. Kwa upande wake, Prof. Mario Draghi, Waziri mkuu wa Italia amesema idadi ya watoto wanaozaliwa ni muhimu kama ulivyo umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na usawa kati ya watu unaosimikwa katika kanuni maadili na utu wema. Inasikitisha kuona kwamba, kwa wanawake kuchukua na kulea mimba ni jambo la fedheha sana na matokeo yake uchoyo na ubinafsi ukatawala. Tafiti nyingi zinaonesha kwamba, familia nyingi zaidi zingependa kupata watoto, lakini mazingira ya sasa hayana mvuto. Kumbe, kuna haja kwanza kabisa kuboresha hali ya maisha ya wanawake, kukuza ukuaji wa uchumi pamoja na kuwa uhakika wa hali ya usalama na utulivu wa kijamii. Nia hii njema, halina budi kwenda sanjari na vijana kupata fursa ya ajira, makazi pamoja na huduma bora kwa watoto wao wadogo.

Hii ni changamoto kubwa kwa vijana wengi nchini Italia. Idadi ya watoto wanaozaliwa nchini Italia katika kipindi cha miaka kumi iliyopita imeshuka kwa asilimia 30% na idadi ya watu waliopoteza maisha katika kipindi cha mwaka 2020 ni watu 340, 000. Umri wa wastani watu nchini Italia ni miaka 47, kumbe, ni nchi ambayo watu wake wanaendelea kuzeeka kwa kasi na kuna hatari kwamba, Italia ikatoweka katika ramani ya dunia. Serikali chini ya uongozi wa Prof. Mario Draghi imeanza kuwekeza zaidi katika sera za familia pamoja na kutoa ruzuku kwa familia zenye idadi kubwa ya watoto ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza. Kumbe, kuna haja kwa Serikali ya Italia kuwekeza kwa vijana na wanawake, ili kuwajengea imani na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Jukwaa la familia
14 May 2021, 16:13