Dr. Jose Gregorio Hernandez Cisneros ametangazwa na Mama Kanisa kuwa Mwenyeheri, mfano bora wa kuigwa katika huduma kwa wagonjwa na maskini! Dr. Jose Gregorio Hernandez Cisneros ametangazwa na Mama Kanisa kuwa Mwenyeheri, mfano bora wa kuigwa katika huduma kwa wagonjwa na maskini! 

Dr. Josè G. Hermàndez: Injili ya Huduma ya Upendo Kwa Maskini

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake katika Ibada ya Misa Takatifu anataja sifa kuu za Mwenyeheri Dr. José Gregorio Hernández; Umuhimu wa kudumisha Injili ya Upendo na Upatanisho; Changamoto ya UVIKO-19; pamoja na kunafsisha fadhila za Kikristo kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kitaifa na udugu wa kibinadamu! Amri za Mungu zikawa dira ya maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Askofu mkuu Aldo Giordano, Balozi wa Vatican nchini Venezuela, tarehe 30 Aprili 2021, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko amemtangaza Mtumishi wa Mungu Dr. José Gregorio Hernández Cisneros kuwa Mwenyeheri. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video, anapenda kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya Mwenyeheri Dr. José Gregorio Hernández, ambaye kwa sasa yuko mbinguni pamoja na Bikira Maria wa Coromoto, ili wawe ni waombezi wa familia ya Mungu nchini Venezuela pamoja na watu wote katika ujumla wao! Hili ni tukio ambalo lilikuwa limehifadhiwa katika sakafu ya maisha ya watu wa Mungu nchini Venezuela na sasa Mwenyezi Mungu amedhihirisha wema, ukuu na utukufu wake kwa kumtangaza kuwa Mwenyeheri. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, anataja sifa kuu za Mwenyeheri Dr. José Gregorio Hernández; Umuhimu wa kudumisha Injili ya Upendo na Upatanisho; Changamoto ya UVIKO-19; pamoja na kunafsisha fadhila za Kikristo kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kitaifa na udugu wa kibinadamu!

Mwenyeheri Dr. José Gregorio Hernández, mfuasi amini wa Kristo Yesu ni mfano bora wa kuigwa na watu wote wa Mungu katika maisha, wito na utume wake. Ni mwamini aliyetoa kipaumbele cha kwanza kwa Habari Njema ya Wokovu; katika maisha, wito na utume wake, akaziweka Amri za Mungu kuwa dira na mwongozo wake wa maisha. Mwenyeheri Dr. José Gregorio Hernández, alitenga muda wa kutosha kwa ajili ya kusoma, kutafakari Neno la Mungu na kusali; akaguswa na mateso na mahangaiko ya wagonjwa nchini Venezuela. Akajisadaka bila ya kujibakiza kuhakikisha kwamba, anatumia ujuzi na weledi wake kwa unyenyekevu mkuu katika huduma kwa wagonjwa na maskini. Ni mwamini aliyependa sana kujisomea ili kupata pia hekima ya mambo ya duniani, akazama katika tafiti za kisayansi na kuendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa pamoja na kuwarithisha vijana wa kizazi kipya elimu makini. Ni mwamini aliyejipambanua katika huduma ya kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, akasimama kidete kupambana na changamoto zilizokuwa zinaibuliwa kwa wakati wake na sasa ni Msamaria mwema kwa ajili ya huduma ya walimwengu wote.

Mwenyeheri Dr. José Gregorio Hernández anakumbukwa sana kwa ushuhuda wa huduma kwa raia wa Venezuela, mfano wa Kristo Yesu aliyewaachia Mitume wake kielelezo cha huduma ya upendo kwa kuwaosha wanafunzi wake miguu na kuipangusa kwa kile kitambaa alichojifungia. Aliwapenda wanafunzi wake upeo, na hata Yuda Iskariote alimpenda ingawa alifahamu kwamba, angemsaliti! Hakulipiza kisasi, bali alionesha upendo kwa wote! Huu ni mwaliko wa kuendeleza Injili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu; huduma inayomwilishwa katika fadhila ya unyenyekevu, kama njia ya kusherehekea kutangazwa kwa Mwenyeheri Dr. José Gregorio Hernández. Ni muhimu kuzingatia misingi ya haki, usawa, utu na heshima ya binadamu, kwa kujaliana na kusaidiana. Mwenyeheri Dr. José Gregorio Hernández ni shuhuda na chombo cha upatanisho, mwaliko kwa waamini kujipatanisha wao kwa wao na kunogesha upatanisho huu kwa Mungu, Kanisa na jamii, kwa kutambua kwamba, kukosa na kukoseana ni ubinadamu, kusamehee na kusahau ni mwanzo wa mchakato wa utakatifu wa maisha. Msamaha upate chimbuko lake kutoka katika sakafu ya maisha ya familia!

Mwenyeheri Dr. José Gregorio Hernández ametangazwa wakati ambapo watu wa Mungu nchini Venezuela wanapambana kufa na kupona na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kuna watu wengi wamefariki dunia, bado kuna maambukizi makubwa ya UVIKO-19 na kwamba, hali bado ni tete sana ndiyo maana hata maadhimisho haya yamefanyika kwa kuzingatia itifaki dhidi ya UVIKO-19. Ili kulinda usalama na kupunguza uwezekano wa kusambaza maambukizi kwa haraka, ndiyo maana watu wameambiwa kukaa karantini kwani hili ni gonjwa la hatari sana. Mbele ya macho yake ya imani, Baba Mtakatifu anasema, kuna maelfu ya watu waliokimbia Venezuela ili kutafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Watu hawa wanatindikiwa na uhuru pamoja na mahitaji yao msingi. Lakini ikumbukwe kwamba, wote hawa ni ndugu wamoja wenye haki na wajibu sawa.

Mwenyeheri Dr. José Gregorio Hernández alitambua mateso na mahangaiko ya ndugu zake, akawa ni chemchemi ya imani na matumaini ya watu wa Mungu nchini Venezuela. Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani. Lengo likiwa ni kujenga na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili wote waweze kujikita katika uzalishaji na huduma bora kama sehemu ya mchakato wa kupyaisha tena Venezuela baada ya kutumbukia katika janga na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Moyo wa upatanisho unahitajika katika medani mbalimbali za maisha, kwani hiki ni kitega uchumi kikuu cha hakijamii. Iwe ni fursa ya kujisadaka katika huduma bila ya kujibakiza. Kila mwananchi awe ni chombo na shuhuda wa ujenzi wa umoja wa Kitaifa. Licha ya tofauti zao msingi, wananchi wa Venezuela watambuane kuwa ni ndugu wamoja. Waoneshe unyenyekevu katika kuhudumiana.

Upatanisho na amani ni kati ya sala za Baba Mtakatifu Francisko kwa familia ya Mungu nchini Venezuela anayo tamani kuitembelea mapema iwezekanavyo hali itakavyoruhusu. Serikali na taasisi zake, ziwahakikishie wananchi ulinzi, usalama na imani, kama nyenzo msingi katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, haki na amani. Watu wote wa Mungu nchini Venezuela wanapaswa kujizatiti katika ujenzi wa umoja wa Kitaifa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Haya ni mambo msingi katika kukuza misingi ya demokrasia, ulinzi na usalama; haki, amani na matumaini ya kweli. Umoja wa Kitaifa ndiyo sala kuu ya Baba Mtakatifu Francisko.

Mwenyeheri Dr
01 May 2021, 16:14