UNHCR: Sikilizeni na kujibu kilio cha wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum kama kielelezo cha umoja na udugu wa kibinadamu. UNHCR: Sikilizeni na kujibu kilio cha wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum kama kielelezo cha umoja na udugu wa kibinadamu. 

UNHCR: Sikilizeni na Kujibu Kilio cha Wakimbizi na Wahamiaji!

Papa amekutana na kuzungumza na Dr. Fillipo Grandi pamoja na ujumbe wake. Wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi duniani, baa la njaa, umaskini na magonjwa, lakini kwa namna ya pekee janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona ni kati ya tema tete zilizojadiliwa na Baba Mtakatifu pamoja na Dr. Fillipo Grandi katika mazungumzo yao. Kuna haja ya kusikiliza na kujibu kilio cha maskini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna watu wanaokimbia nchi na makazi yao kwa sababu ya baa la njaa, vita, umaskini, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na hatari mbali mbali za maisha na hivyo wanatafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Kristo Yesu yuko kati pamoja na watu wote hawa kama hata ilivyo kwa wale wote wanaoteseka kwa kiu; walio uchi, wagonjwa, wafungwa na wageni. Waamini wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanauona Uso wa Kristo Yesu anayeteseka kati pamoja na watu wote hawa. Waamini waoneshe ujasiri wa kuwaendea ili kukutana nao, kuwapenda na kuwahudumia kwa niaba ya Kristo Yesu. Watu wasiokuwa na makazi maalum ni fursa nyingine tena ya kukutana na Kristo Yesu, tayari kuwakaribisha, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha katika maisha ya jumuiya inayowapatia ukarimu. Hii ndiyo sera na mkakati wa Kanisa katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji sehemu mbalimbali za dunia. Kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Emau waliweza kumtambua Kristo Yesu kwa kumega mkate. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 liwasaidie waamini kufahamu changamoto wanazokabiliana nazo wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Jambo la msingi ni kuwa karibu nao, ili kuwahudumia kwa huruma na mapendo kama ilivyokuwa kwa yule Msamaria mwema.

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 16 Aprili 2021 amekutana na kuzungumza na Dr. Fillipo Grandi Kamishna mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, pamoja na ujumbe wake. Wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi duniani, baa la njaa, umaskini na magonjwa, lakini kwa namna ya pekee janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ni kati ya tema tete zilizojadiliwa na Baba Mtakatifu pamoja na Dr. Fillipo Grandi katika mazungumzo yao. Katika mahojiano maalum na Vatican News, Dr. Fillipo Grandi anakiri kwamba, ni vigumu sana kwa wakati huu kufanya majadiliano kuhusu huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum hasa katika kipindi hiki ambapo kuna maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 sehemu mbalimbali za dunia na kila nchi inataka kujihami dhidi ya maambukizi mapya. Katika muktadha huu, waathirika ni maskini, wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Sera za kuwapokea na kuwahudumia watu hawa zimegeuzwa kuwa ni ajenda za kujitafutia umaarufu wa kisiasa, ingawa kimsingi, huduma hii ilipaswa kuwa ni sehemu ya utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Wimbi kubwa la wakimbizi huko Amerika ya Kati, Kusini na Kaskazini ni changamoto kubwa hasa kutokana pia na machafuzo ya kisiasa na kijamii kama yanayovyojidhihirisha huko nchini Venezuela. Umoja wa Jumuiya ya Ulaya UE, unapaswa kuwa na sera makini kwa ajili ya kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, linaunga mkono sera na mbinu mkakati wa Kanisa katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji. Hawa ni watu wanaokimbia, vita, dhuluma, nyanyaso, majanga asilia pamoja athari za mabadiliko ya tabianchi. UVIKO-19 kwa sasa nalo ni janga linalotishia usalama na maisha ya watu wengi. Kuna baadhi ya wanasiasa sehemu mbalimbali za dunia wanaotumia wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kama sehemu ya kujijenga kisiasa kwa kujimwambafai, ili kushinda chaguzi mbalimbali, jambo ambalo ni kinyume kabisa cha maadili na utu wema.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwa ni sauti ya maskini na wanyonge; wakimbizi na wahamiaji, ili Jumuya ya Kimataifa iweze kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika mshikamano wa umoja na upendo. Wakimbizi na wahamiaji kwa sasa wanaishi katika maeneo na mazingira magumu sana, kiasi cha kukosa ulinzi na usalama pamoja na mahitaji yao msingi. Haya ndiyo yaliyojidhihirisha huko Lesvos, nchini Ugiriki na Libya. Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji pia kuna mkono wa wafanyabiashara ya binadamu na viungo vyake. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, lililoanzishwa kunako mwaka 1950 lilipaswa kudumu kwa muda wa miaka mitatu tu. Lakini hadi mwaka 2021 linaadhimisha kumbukizi la miaka 70 tangu kuanzishwa kwake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni sehemu ya changamoto tete za Jumuiya ya Kimataifa kwa wakati huu.

Wakimbizi na Wahamiaji

 

 

17 April 2021, 15:41