Papa:Tusali kwa ajili ya wanaohatarisha maisha wakitetea haki msingi

Katika Video yenye nia za maombi kwa mwezi Aprili,Papa Francisko anakazia umakini wa hadhi ya kila mtu.Mawazo yake yanawaendea wale wote wanaoitetea katika udikteta,katika tawala za kimabavu na hata katika demokrasia yenye mgogoro.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

“Ni juu ya haki msingi ambayo kila mwanadamu anapaswa kukuza katika ufungamani na ambayo haiwezi kukataliwa na nchi yoyote ambayo  Papa Francisko katika nia zake kwa Mwezi Aprili 2021 amekazia na ambazo zimetolewa kwa njia ya Video  ambayo inayoandaliwa kila mwezi na Mtandao wa Maombi Kimataifa. Papa anseama: “Katika maeneo mengine kutetea hadhi ya watu kunaweza kumaanisha kwenda gerezani hata bila mchakato wa kesi” au “kashfa”. Katika kurejea hili  ni ukweli wa kupinga kwa dhati umaskini, ukosefu wa usawa, ukosefu wa kazi, ardhi na makazi, haki za kijamii, anaelezea, akibainisha, kwamba kutetea haki msingi za binadamu kunahitaji ujasiri na uamuzi. “Tuwaombee wale ambao wanahatarisha maisha yao wanapigania haki msingi katika udikteta, tawala za kimabavu na hata katika demokrasia zenye mzozo, na ili waweze kuona kwamba sadaka zao na kazi zao zinazaa matunda mengi.”

Papa Francisko pia anaelezea ufahamu kwamba: “mara nyingi haki msingi za kibinadamu hazilingani kwa kila mtu”, kwa maana kwamba, “kuna watu wa daraja  la kwanza, la pili, la tatu, na watu wanaochukuliwa kuwa taka”. “Hapana”, anasema tena mbele ya ukweli huu: “Lazima ziwe sawa kwa kila mtu”. Katika Video hiyo inaingiliana na picha za Papa uku akiongea na mikono ya watu wanaofanya kazi au kusoma au wanaoishi katika hali mbaya.  Kwa mujibu wa taarifa kutoka Mtandao wa Maombi ya sala Kimataifa ya nia za Papa anasema Video hiyo inasadiwa na Utume wa Kudumu wa Vatican katika Shirika la Umoja wa Mataifa

Na katika taarifa hiyo pia inataka kupyaisha Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu, lililopitishwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mnamo 1948, ambalo lilikuwa na hati ya kwanza ya kisheria ya kuanzisha ulinzi wa ulimwengu wa haki msingi za binadamu. Hata Kanisani, kuanzia na Papa Yohane XXIII mnamo mwaka 1960, haki za binadamu zimekuwa na umuhimu mkubwa katika mafundisho ya Kikatoliki na mazoezi ya kijamii”. Taarifa hiyo inakumbuusha pia hata na makala ya hivi karibuni ambayo Kardinali Michael Czerny alibainisha kuwa “Mtakatifu Yohane XXIII aliorodhesha haki msingi katika Waraka wake wa  Pacem in terris, mnamo 1963 na kuanza na zile ambazo leo hii zinachukuliwa kuwa haki za kiuchumi.

“Kila binadamu ana haki ya kuishi, anasema, kwa uadilifu wa mwili, zana za lazima na za kutosha kwa ajili ya kiwango cha maisha chenye hadhi hasa kuhusu chakula, mavazi, nyumba, kupumzika, huduma ya matibabu, huduma muhimu za kijamii”. Leo hii,  Papa Francisko anaweka mkazo huo huo, akisisitiza hasa haki za kufanya kazi, nyumba, ardhi na usalama na uhakika wa chakula”. Mwaliko wa Papa Francisko  kwenye video hiyo, anasema Padre Frédéric Fornos, mkurugenzi wa kimataifa wa Mtandao wa Maombi Duniani wa Papa, ni kuwaombea wale ambao wanahatarisha maisha yao wakipigania haki imsingi, “kwa kuwakumbuka wanaume na wanawake hawa, katika nchi nyingi za ulimwengu, ambao wako gerezani au katika hali ya  hatari, au ambao wamepoteza maisha yao, wengi kwa jina la imani yao kwa Yesu Kristo. Tusiwasahau, tuwaombee”.

Padre Fornos anasema “Sio mara ya kwanza kwamba Papa Francisko anasisitiza juu ya umuhimu wa haki msingi za watu. Katika Waraka wake wa hivi karibuni wa Fratelli tutti yaani Wote ni ndugu, alishutumu kwamba 'wakati sehemu moja ya wanadamu inaishi kwa utajiri, sehemu nyingine inaona hadhi yake ikidharauliwa, au kukanyagwa na haki zake msingi kupuuzwa au kukiukwa”. Tukumbuke kuwa Video ya Papa ni mpango rasmi wa ulimwengu wa kusambaza nia za sala za kila mwezi za Baba Mtakatifu. Imetengenezwa na Mtandao wa Maombi Kimataifa kwa ajili ya mambo ya Papa (Utume wa Maombi). Tangu 2016, Video za Papa zimekuwa zikitazamwa zaidi ya mara milioni 152 kwenye mitandao yake yote ya kijamii. Inatafsiriwa kwa zaidi ya lugha 23, na ina habari za waandishi wa habari katika nchi 114.

07 April 2021, 15:41