Papa Francisko kama sehemua ya mshikamano wa upendo wa udugu wa kibinadamu ametoa zawadi ya dawa na vifaa tiba kwa familia ya Mungu nchini Armenia ili kupambana na UVIKO-19. Papa Francisko kama sehemua ya mshikamano wa upendo wa udugu wa kibinadamu ametoa zawadi ya dawa na vifaa tiba kwa familia ya Mungu nchini Armenia ili kupambana na UVIKO-19. 

Mshikamano wa Upendo kwa Waathirika wa UVIKO-19 Armenia

Askofu mkuu José A. Bettencourt, Balozi wa Vatican nchini Armenia amekabidhi dawa na vifaa tiba kwa Padre Mario Cuccarollo, Mkurugenzi mtendaji wa Hospitali ya “Redemptoris Mater” huko Ashotsk nchini Armenia. Tukio hili limehudhuriwa na baadhi ya wanajumuiya wa eneo hili. Dawa na vifaa tiba ni kwa ajili ya waathirika wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Mshikamano!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, katika kipindi cha miaka minanne ameendelea kujipambanua kwa kusimama kidete katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya na utamadunisho, unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Ameendelea kuhimiza utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na mapambano dhidi ya umaskini ili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano. Hata katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, Baba Mtakatifu anawaambia waamini kwamba Kristo Yesu anawajali na kuwasumbukia waja wake.  Ni muda muafaka wa kufanya toba na wongofu wa ndani, kwa kuzingatia na kuambata mambo msingi katika maisha. Ni wakati wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki zao msingi. Huu ni wakati wa kuwashukuru madaktari, wauguzi, wafanyakazi katika sekta ya afya, vikosi vya ulinzi na usalama, watu wa kujitolea, mapadre na watawa wanaoendelea kusadaka maisha yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ni wakati wa kujenga na kudumisha umoja na udugu wa mshikamano na watu wa Mungu. Sala inayomwilishwa katika huduma ya upendo ni silaha madhubuti katika mapambano dhidi ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Ni wakati wa kupyaisha imani katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, kwani ukombozi wa mwanadamu umefumbatwa juu ya Msalaba, chemchemi ya: imani, matumaini, nguvu na ujasiri wa kusonga mbele bila kugubikwa na woga unaosababisha taharuki kwa watu wa Mungu. Mfuko wa Msamaria Mwema “Fondazione Buon Sammaritano” unasimamiwa na kuratibiwa na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu kwa kushirikiana na Ubalozi wa Vatican nchini Armenia, tarehe 25 Aprili 2021, Jumapili ya Mchungaji mwema, wamewasilisha dawa na vifaa tiba kama mchango wa Baba Mtakatifu Francisko katika mapambano dhidi ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 nchini Armenia.

Askofu mkuu José A. Bettencourt, Balozi wa Vatican nchini Armenia amekabidhi vifaa hivi kwa Padre Mario Cuccarollo, Mkurugenzi mtendaji wa Hospitali ya “Redemptoris Mater” huko Ashotsk nchini Armenia. Tukio hili limehudhuriwa na baadhi ya wanajumuiya wa eneo hili. Dawa na vifaa tiba ni kwa ajili ya waathirika wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Hospitali hii inamilikiwa na kuendeshwa na Shirika la Wakamiliani lililoanzishwa na Mtakatifu Kamili wa Lellis (St. Camillo de Lellis”. Kwa takribani miaka 25 hospitali hii imekuwa ikitoa huduma kwa watu wote wa Mungu bila ubaguzi, kwa gharama nafuu kwa wale wanaomudu na bure kwa maskini wote na watu wanaokabiliana na hali ngumu ya kiuchumi. Kumbe, kumbukizi la miaka minane tangu Baba Mtakatifu Francisko achaguliwe kuliongoza Kanisa, imekuwa ni siku ya kumshukuru Mungu kwa huruma na upendo wake, unaomwilishwa katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Camillo wa Lellis alifariki dunia mwaka 1614 baada ya kutumikia wagonjwa kwa miaka 40 bila kuchoka. Mwaka 1745 alitangazwa Mtakatifu na Papa Benedikto wa XIV. Mwaka 1886 Mtakatifu Camillo alitangazwa kuwa mlezi na msimamizi wa wagonjwa na wale wote wanaojitolea kuwahudumia wagonjwa, kama madaktari na wauguzi. Shirika la Mtakatifu Camillo lijulikanalo kama Wahudumu wa Wagonjwa limeenea katika mabara matano duniani; Mapadri na Mabruda wanahudumia wagonjwa katika nchi 32 duniani. Barani Afrika wako nchini: Tanzania, Uganda, Kenya, Burkinafaso, Benini na Madagascar. Nchini Tanzania Wakamilliani wanapatikana makao makuu ya Shirika yaliyoko Yombo-Vituka, Dar es Salaam, Hospitali Kuu ya Taifa, Muhimbili-Dar es salaam, Parokia ya Yombo-Kiwalani pamoja na Parokia ya Yombo-dovya, zote ziko Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Armenia
26 April 2021, 14:27