Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko ametoa Ujumbe na salam za Pasaka kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, "Urbi et Orbi" kwa Mwaka 2021: Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Baba Mtakatifu Francisko ametoa Ujumbe na salam za Pasaka kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, "Urbi et Orbi" kwa Mwaka 2021: Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. 

Ujumbe wa Pasaka "Urbi et Orbi" 2021: Janga la UVIKO-19!

Papa: “Urbi et Orbi” kwa ajili ya mji wa Roma na ulimwengu katika ujumla wake. Amekazia: Athari za maambukizi makubwa ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 sanjari na kashfa ya vita na ghasia inayoendelea kuimarika kila kukicha sehemu mbalimbali za dunia. Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ni chemchemi ya matumaini yasiyodanganya hata kidogo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Ilikuwa ni tarehe 17 Aprili 1949, Mtumishi wa Mungu Papa Pio XII, kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, alipotuma Ujumbe wa Pasaka kwa ajili ya mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake: “Urbi et Orbi” kwa njia ya Televisheni ya Ufaransa, akiwatakia waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema heri na baraka za Sherehe ya Pasaka. Katika ujumbe huo, alikazia umuhimu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na waamini katika ujumla wao, kukutana katika uwanja wa mawasiliano na kwa wakati huo, Televisheni. Katika muktadha huu, njia za mawasiliano na mitandao ya kijamii imekuwa ni msaada mkubwa kwa maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kilele cha ukweli wa imani katika Kristo aliyeteswa, akafa na hatimaye kufufuka kutoka wafu kadiri ya Maandiko Matakatifu. Ni ufunuo wa Uungu wa Kristo Yesu unaowapatia waamini maisha ya uzima mpya na hivyo kuhesabiwa haki pamoja na kufanywa wana wateule wa Mungu. Ufufuko wa Kristo ni msingi wa ufufuko wa miili na uzima wa milele ijayo! Ndiyo maana Pasaka ni Sherehe kubwa katika Kanisa. Hii ni Sherehe ya upendo, huruma na msamaha wa Baba wa milele unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 4 Aprili 2021, ameadhimisha Sherehe ya Pasaka ya Bwana, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baadaye ametoa ujumbe wa Pasaka: “Urbi et Orbi” kwa ajili ya mji wa Roma na ulimwengu katika ujumla wake. Amekazia kuhusu athari za maambukizi makubwa ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 sanjari na kashfa ya vita na ghasia inayoendelea kuimarika kila kukicha sehemu mbalimbali za dunia. Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ni chemchemi ya matumaini yasiyodanganya hata kidogo. Huyu ni Kristo Yesu aliyehukumiwa na Ponsyo Pilato kwa sababu alidai kwamba, Yeye ni Kristo, Mwana wa Mungu. Akafa na kufufuka kwa wafu siku ya tatu kadiri ya Maandiko Matakatifu na kama alivyokuwa amekwisha kuwaambia wafuasi wake. Kristo Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani ndiye aliyefufuka kwa wafu ili kukamilisha utashi wa kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Alivumilia mateso na uzito wa dhambi za binadamu na Mwenyezi Mungu akamwinua na sasa Kristo Yesu anaishi milele yote na kwamba, ni Yeye ni Bwana! Mashuhuda wa ufufuko wa Kristo Yesu wanasema, waliyaona Madonda yake Matakatifu, kielelezo cha hali ya juu sana cha upendo wake kwa binadamu. Na kwa njia ya Madonda Matakatifu ya Yesu, waamini wanapokea neema ya matumaini yasiyo danganya hata kidogo. Yesu ni tumaini la wale wote wanaoendelea kuteseka na kuathirika kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Yesu Mfufuka ni tumaini kwa wale wote wanaokumbana na majaribu ya kiroho na kimwili, ili kuweza kusonga mbele pasi na kukata tamaa! Kristo Mfufuka awe ni nguvu na faraja kwa madaktari na wauguzi wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa waathirika kwa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Maskini na wayonge ndani ya jamii, wanahitaji na ni haki yao kupata huduma muhimu za kiafya, hasa zaidi wakati huu wa mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Chanjo dhidi ya UVIKO-19 ni nyenzo muhimu sana katika mchakato wa mapambano dhidi ya gonjwa hili. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kuitaka Jumuiya ya Kimataifa katika moyo wa uwajibikaji kiulimwengu kujizatiti zaidi ili hatimaye, kuondokana na changamoto ya kucheleweshwa ugawaji wa chanjo na hasa kwa nchi maskini zaidi duniani. Kristo Yesu Mfufuka ni faraja kwa wale wote waliopoteza fursa za ajira au wanaokabiliana na hali ngumu ya kiuchumi pamoja na kukosa hifadhi makini za kijamii. Yesu awasaidie viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kutenda kwa haki, ili watu wote na hasa familia maskini ziweze kupata msaada utakaowasaidia kuwa na hali nzuri zaidi ya maisha. Inasikitisha kuona kwamba, Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la watu maskini na wale waliokata tamaa duniani. Maskini wa kiroho na kimwili, wanapaswa kujengewa mazingira yatakayowasaidia kuwa na matumaini mapya.

Baba Mtakatifu ameyaelekeza mawazo yake nchini Haiti. Anawaalika wasielemewe sana matatizo na changamoto za maisha, bali wajiamini na kuwa na matumaini kwa siku za mbeleni. Kristo Yesu Mfufuka awe ni faraja kwa wanafunzi ambao wanashindwa kuendelea na masomo yao, wale wanaokosa hata fursa ya kukutana na marafiki zao. Kuna haja ya kujenga mahusiano na mafungamano halisi ya kibinadamu na wala si tu kwa njia ya mitandao ya kijamii, kwa sababu huu ni msaada mkubwa katika malezi na majiundo ya kiutu. Baba Mtakatifu anapenda kuungana na vijana wa kizazi kipya kutoka sehemu mbalimbali za dunia, lakini kwa namna ya pekee kabisa, anapenga kuungana na vijana wa Myanmar, wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutetea demokrasia, huku wakitaka sauti yao iweze kusikilizwa kwa amani, kwa kutambua kwamba, chuki inaweza kusambaratishwa kwa upendo peke yake.

Mwanga wa Kristo Mfufuka, uwe ni chanzo cha maisha mapya kwa wakimbizi na wahamiaji wanaokimbia vita, chuki, ghasia na umaskini. Nyuso zao za kukatisha tamaa, iwe ni fursa ya kukutana na Kristo Yesu akiwa njiani kuelekea Mlimani Kalvari. Waonjeshwe mshikamano na udugu wa kibinadamu, ili kusherehea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo hasa katika kipindi hiki cha Sherehe ya Pasaka ya Bwana. Baba Mtakatifu anazishukuru na kuzipongeza nchi zote zinazotoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji. Lebanon na nchi ya Yordan zimekuwa msaada mkubwa kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka nchini Siria. Watu wa Mungu nchini Lebanon wanaopitia kipindi kigumu katika historia ya maisha yao, wapate faraja kutoka kwa Kristo Mfufuka na msaada kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa, ili katika wito wao, Lebanon iendelee kuwa ni daraja la kuwakutanisha watu  na kuishi kwa amani na utulivu kwa kuzingatia tofauti zao msingi.

Kristo Mfufuka amani ya watu wake, asaidie kusitisha mapambano ya silaha nchini Siria ambako kuna mamilioni ya watu wanaoishi katika mazingira duni sana. Kuna watu wanateseka huko Yemen, lakini mateso yao yamekumbana na kashfa ya kimya kikuu. Nchini Libya mwanga wa matumaini unaanza kuonekana baada ya mapambano ya silaha kwa miaka kadhaa. Ni matumaini na sala ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wadau wote wanaohusika na mgogoro wa Libya wataweza kujizatiti na hatimaye kumaliza mgogoro huu wa kivita, ili hatimaye, wananchi wanaoteseka kwa vita waweze tena kuishi kwa amani na hatimaye, kuanza mchakato wa ujenzi wa nchi zao husika. Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu linawapeleka waamini na watu wote wenye mapenzi mema mjini Yerusalemu. Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu aweze kuujalia mji wa Yerusalemu amani na usalama, ili kweli uweze kuwa ni mji unaowakutanisha watu wanaojitambua kuwa ni ndugu wamoja. Waisraeli na Wapalestina wagundue tena ndani mwao ile nguvu ya majadiliano ili kuweza kufikia muafaka wa kudumu, utakaoziwezesha nchi hizi mbili kujikita katika amani, ustawi na maendeleo ya watu wake.

Katika maadhimisho ya Pasaka ya Bwana, Baba Mtakatifu Francisko ameyaelekeza mawazo yake nchini Iraq, ambako hivi karibuni alibahatika kupatembelea. Anaendelea kuwahimiza watu wa Mungu nchini Iraq kujizatiti katika njia ya amani, huku wakiendelea kutekeleza ndoto ya Mungu itakayowawezesha kujenga familia yenye ukarimu, amani na utulivu kwa watoto wote wa Mungu. Baba Mtakatifu anamwomba Kristo Mfufuka awawezeshe na kuwaimarisha watu wa Mungu Barani Afrika wanaoendelea kuona matumaini ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yakiwekwa rehani kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe pamoja na vitendo vya kigaidi kimataifa. Nchi zilizoathirika zaidi ni zile zilizoko kwenye Ukanda wa Sahel, Nigeria, Tigray pamoja na mkoa wa Cabo Delgato ulioko nchini Msumbiji. Jitihada za kupata suluhu ya amani katika migogoro na kinzani hizi ziendelezwe; kwa kuheshimu na kuthamini haki msingi za binadamu sanjari na utakatifu wa maisha unaosimikwa katika udugu wa kibinadamu, majadiliano katika ukweli na uwazi, upatanisho na mshikamano wa kweli!

Kristo Yesu Mfufuka ni Bwana wa Amani asaidie kubadilisha akili na nyoyo za watu, ili kuondokana na dhana ya vita! Awasaidie wafungwa wa kivita hasa kutoka Mashariki mwa Ukraine na Nagorno-Karabakh, kurejea na kujiunga tena na familia zao, salama salimini. Kristo Mfalme wa Amani, awasaidie viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuachana na mashindano ya utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha mpya. Tarehe 4 Aprili kila mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya kuelimisha kuhusu madhara ya mabomu ya kutegwa ardhini sambamba na kusaidia hatua za kuyaondoa kule ambako bado yamesalia. Mabomu haya ni tishio kwa maisha na usalama wa watu. Ni kikwazo cha ustawi, mafao na maendeleo fungamani ya binadamu. Zaidi ya nchi 160 ni wanachama wa mkataba wa kimataifa wa kuondokana na mabomu ya kutegwa ardhini.  Mabomu ya kutegwa ardhini anasema Baba Mtakatifu Francisko ni kikwazo cha kufanya kazi kwa pamoja katika njia ya maisha bila kuogopa uharibifu na maafa. Ulimwengu ungekuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, ikiwa kama haungekuwa na silaha hizi zinazopandikiza utamaduni wa kifo!

Pasaka ya Bwana, sehemu mbalimbali za dunia inaadhimishwa katika mazingira magumu na kwa baadhi ya sehemu, waamini wameshindwa hata kuhudhuria Liturujia Takatifu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, sheria, kanuni na taratibu hizi za kuwazuia watu kuhudhuria Ibada na Liturujia mbalimbali zitaondolewa, ili watu waweze kufurahia uhuru wa kuabudu na kidini sehemu mbalimbali za dunia, ili hatimaye, watu waweze kuruhusiwa kusali na kumtukuza Mwenyezi Mungu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika shida na mahangaiko yao, daima wakumbuke kwamba, wameponywa kwa Madonda Matakatifu ya Yesu. Katika mwanga wa Kristo Mfufuka, mahangaiko na mateso ya mwanadamu yamepata maana mpya zaidi. Mahali ambapo kifo kilitawala, sasa ni chemchemi ya uhai. Pale ambapo watu walikuwa wanaomboleza na kulia, sasa wanapata faraja. Kwa kukumbatia na kuambata Fumbo la Msalaba, Kristo Yesu ameleta maana mpya katika mahangaiko ya binadamu. Kanisa linasali ili kwamba, matunda ya uponywaji huu sasa yaweze kusambaa ulimwenguni kote. Mwishoni mwa ujumbe wake wa Pasaka: “Urbi et Orbi” kwa ajili ya mji wa Roma na ulimwengu katika ujumla wake, amewatakia watu wote heri na baraka za Sherehe ya Pasaka ya Bwana kwa mwaka 2021.

Papa Urbi et Orbi

 

 

 

 

04 April 2021, 15:29

Sala ya Malkia wa Mbingu ni nini?
 

Utenzi wa Malkia wa Mbingu ni kati ya tenzi nne za Bikira Maria (nyingine ni:Tunakimbilia Ulinzi wako,  Salam Malkia wa Mbingu, Salam Malkia). Kunako mwaka 1742, Papa Benedikto XIV alipoandika kwamba, waamini wasali Sala ya Malkia wa Mbingu wakiwa wamesimama, kama alama ya ushindi dhidi ya kifo, wakati wa Kipindi cha Pasaka, yaani kuanzia Domenika ya Ufufuko wa Bwana hadi Sherehe ya Pentekoste. Hii ni Sala ambayo husaliwa mara tatu kwa siku kama ilivyo pia Sala ya Malaika wa Bwana: Asubuhi, Mchana na Jioni ili kuweka wakfu Siku kwa Mwenyezi Mungu na Bikira Maria.

Utenzi huu kadiri ya Mapokeo ulianza kutumika kunako karne ya VI au Karne X, lakini kuenea kwake kunaanza kujitokeza katika nyaraka mbali mbali kati kati ya Karne ya XIII, ilipoingizwa kwenye Kitabu cha Sala za Kanisa cha Wafranciskani. Hii ni Sala inayoundwa na maneno mafupi manne yanayohitimishwa na Alleluiya na sala ya waamini wanaomwelekea Bikira Maria, Malkia wa mbingu, ili kufurahia pamoja naye kuhusu Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu.

Papa Francisko tarehe 6 Aprili 2015 wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, siku moja baada ya Sherehe ya Pasaka, aliwashauri waamini kuwa na moyo wa furaha wanaposali sala hii. “Tunamwendea Bikira Maria, tukimwomba afurahi, kwa sababu yule Mwanaye mpendwa aliyekuwa amemchukua mimba amefufuka kweli kweli kama alivyosema; tunajiaminisha kwa sala na maombezi ya Bikira Maria. Kimsingi furaha yetu ni mwangi wa furaha ya Bikira Maria kwani ndiye aliyetunza na anaendelea kutunza matukio mbali mbali ya maisha ya Yesu. “Tusali sala hii kwa furaha ya kuwa waana wa Mungu ambao wanafurahi kwa sababu Mama yao anafurahi”

 

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >