Papa Francisko: Michezo isaidie mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, ili kunogesha majadiliano ya mshikamano kati ya watu na tamaduni mbalimbali duniani! Papa Francisko: Michezo isaidie mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, ili kunogesha majadiliano ya mshikamano kati ya watu na tamaduni mbalimbali duniani! 

Papa Francisko: Siku ya Michezo, Maendeleo na Amani Duniani!

Tarehe 6 Aprili ya kila mwaka, ilichaguliwa na Jumuiya ya Kimataifa ili kuenzi ufunguzi wa Michezo ya Olympic iliyofanyika kunako tarehe 6 Aprili 1896 huko Athens nchini Ugiriki. Lengo la maadhimisho haya ni kutambua na kuthamini majukumu ya michezo katika maisha ya watu. Papa Francisko anasema michezo inogeshe majadiliano ya mshikamano kati ya watu na tamaduni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 23 Agosti 2013 lilipitisha Azimio la Siku ya Kimataifa ya Michezo kwa ajili ya Maendeleo na Amani. Siku hii inaadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Aprili. Tarehe hii ilichaguliwa na Jumuiya ya Kimataifa ili kuenzi ufunguzi wa Michezo ya Olympic iliyofanyika kunako tarehe 6 Aprili 1896 huko Athens nchini Ugiriki. Lengo la maadhimisho haya ya michezo ni kutambua na kuthamini majukumu ya michezo katika maisha ya watu. Kutokana na athari za maambukizi makubwa ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, maadhimisho haya yamefanyika kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Watu wameonesha thamani na umuhimu wa michezo sanjari na kuchukua tahadhari dhidi Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake, Jumatano tarehe 7 Aprili 2021 amesema, watu wanapaswa kuwa na mang’amuzi mapana zaidi kwamba, michezo ni tukio linaloadhimishwa kama timu, ili kujenga na kudumisha mchakato unaonogesha majadiliano ya mshikamano kati ya watu na tamaduni mbalimbali duniani.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni katika uzinduzi wa Waraka wa “Dare il meglio di se”, yaani “Kujitoa Kikamilifu”: Mtazamo wa Kikristo kuhusu michezo na binadamu” uliochapishwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, michezo ni mahali pa kuwakutanisha watu katika ngazi mbali mbali. Ili kuweza kufikia lengo maalum. Michezo ni kiungo maalum cha majiundo na tunu msingi za maisha ya kiutu. Hapa ni mahali pa kukuza na kudumisha: ukarimu, unyenyekevu, sadaka, udumifu na furaha, kila mtu akijitahidi kuchangia kadiri ya uwezo na karama zake, kielelezo makini cha ujenzi wa umoja na mshikamano unaobomolea mbali tabia ya ubinafsi na uchoyo. Michezo katika mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ni Sakramenti ya wokovu; ni mtangazaji wa Habari Njema na shuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Michezo katika nafasi mbali mbali ni jukwaa la kutangaza na kumshuhudia Kristo kwa walimwengu. Ni wakati wa kuwashirikisha wengine, ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Michezo ni wakati muafaka wa kuonja: uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji kwa kukutana na watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanamichezo wa kweli ni wajumbe na mashuhuda wa Kristo Mfufuka wanapokuwa uwanjani. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hata wanamichezo wanaweza kuwa ni watakatifu, kwani daima wanaitwa na kuhamasishwa kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao kila kukicha! Michezo inapania kujenga na kuimarisha urafiki na udugu wa kibinadamu kati ya watu; kukuza na kudumisha maelewano na amani; kuheshimiana, maridhiano na utulivu kwa kuthamini tofauti zinazojitokeza kati ya watu. Tunu msingi za michezo zinapaswa kusisitizwa miongoni mwa vijana na watoto, ili kuwasaidia kutambua kwamba, kila fursa iliyopo inaweza kutumika kwa ajili ya maboresho ya maisha ya mtu: kiroho na kimwili. Kufaulu na kushindwa katika masuala ya michezo ni ukweli usioweza kupingika.

Hii iwe ni fursa ya kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha kwa ujasiri na moyo mkuu; kwa kuzingatia na kuheshimu sheria, kanuni, maadili na utu wema; mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya michezo. Lakini inasikitisha kuona kwamba, nyakati hizi, michezo inahusishwa sana na masuala ya kiuchumi, mashindano yasiyokuwa na tija, vurugu pamoja na ubaguzi kwa wale ambao hawana kiwango cha juu cha ushindi. Mashindano ya kimataifa, kimekuwa ni kichaka cha biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na umati mkubwa wa wasichana na wanawake kutumbukizwa katika utalii wa ngono pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo.

Michezo na Amani

 

 

08 April 2021, 14:29