Baba Mtakatifu Francisko amewaandakia watu wa Mungu nchini Ufilippini ujumbe wa imani, matumaini na mapendo wanapoadhimisha Jubilei ya Miaka 500 ya uinjilishaji nchini humo! Baba Mtakatifu Francisko amewaandakia watu wa Mungu nchini Ufilippini ujumbe wa imani, matumaini na mapendo wanapoadhimisha Jubilei ya Miaka 500 ya uinjilishaji nchini humo! 

Papa Francisko:Miaka 500 ya Ukristo Nchini Ufilippini: 1521-2021

Jubilei ya Miaka 500 ya Uinjilishaji nchini Ufilippini: Wamisionari kutoka sehemu mbalimbali za Ufilippini wakutana! Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, anawapongeza na kuwashukuru kwa kujikita kikamilifu katika tunu msingi za Injili ya familia kwa kuiga mfano bora wa Familia Takatifu; Umuhimu wa Fumbo la Msalaba na Pentekoste katika maisha na utume wa Kanisa mahalia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, mintarafu Maandiko Matakatifu, Jubilei ni kipindi cha kumbukumbu, toba na wongofu wa ndani; muda muafaka wa mapumziko; muda wa kujichotea nguvu pamoja na kufurahia matunda ya kazi ya uumbaji. Ni muda wa kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Familia ya Mungu nchini Ufilippini inaadhimisha kilele cha Jubilei ya Miaka 500 ya Ukristo nchini humo. Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 14 Machi 2021 aliungana watu wa Mungu kutoka Ufilippini wanaoishi ndani na nje ya mji wa Roma, ili kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya imani kwa watu wa Mungu nchini Ufilippini. Idadi yao inakadiriwa kufikia takribani milioni 10 wanaoishi katika nchi mbalimbali za dunia. Kristo Yesu, daima amekuwa mwandani wa safari na maisha yao ya imani wanapokuwa ughaibuni. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko kwa mara  nyingine tena, amewatumia ujumbe wa matashi mema, watu wote wa Mungu nchini Ufilippini wanapoadhimisha sasa katika ujumla wao, Jubilei ya Miaka 500 ya Uinjilishaji nchini Ufilippini, kwa kuwakutanisha wamisionari kutoka sehemu mbalimbali za Ufilippini.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, anawapongeza na kuwashukuru kwa kujikita kikamilifu katika tunu msingi za Injili ya familia kwa kuiga mfano bora wa Familia Takatifu; Umuhimu wa Fumbo la Msalaba na Pentekoste katika maisha na utume wa Kanisa. Mama Kanisa anapenda kuiweka Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu kuwa ni kielelezo na mfano bora wa kuigwa na familia za Kikristo. Familia Takatifu ni shule ya tunu msingi za Kiinjili, changamoto na mwaliko kwa familia za Kikristo kujenga familia zinazokita mizizi yake katika Injili ya uhai, upendo na mshikamano wa kidugu. Baba Mtakatifu anawataka watu wa Mungu nchini Ufilippini, kumfungulia Kristo Yesu, malango ya familia zao, tayari kuwarithisha watoto wao imani ambayo hata wao wameirithi kutoka kwa wazazi wao. Watu wa Mungu nchini Ufilippini wanapongezwa na Mama Kanisa kwa kuzama katika tunu msingi za maisha ya familia, utambuzi wao kama jumuiya ya waamini pamoja na kukuza udugu wa kibinadamu katika maisha yao. Matokeo yake ni kwa wananchi wa Ufilippini kuwa ni watu wenye imani thabiti, matumaini na mapendo!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, watu wa Mungu nchini Ufilippini wanatambua fika jinsi ya kumsindikiza Kristo Yesu katika Njia ya Msalaba. Katika mchakato wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Uinjilishaji nchini Ufilippini, walikumbwa na tetemeko la ardhi, kimbunga, kulipuka kwa volcano na kwa sasa kuna maambukizi makubwa ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Licha ya matatizo na changamoto zote hizi, bado watu wa Mungu nchini Ufilippini anasema Baba Mtakatifu, wanaendelea kupeta katika hija ya Njia ya Msalaba. Wanaendelea kufanya kazi, kwa kusaidiana kama Simoni wa Kirene. Kwa hakika wamekuwa ni mashuhuda wazuri kwa kujiaminisha daima kwa Mwenyezi Mungu, ambaye kamwe hajawatelekeza wala kuwageuzia kisogo, licha ya magumu na changamoto wanazokabiliana nazo. Baba Mtakatifu Francisko kuhusu Pentekoste anasema, hapa ni hatima na mwanzo mpya wa safari ya maisha ya Bikira Maria aliyediriki kufuatana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yake, hata akawa imara na thabiti kumfuata katika Njia ya Msalaba. Akakesha na kusali, akimsubiri Roho Mtakatifu kuwashukia Mitume na kuwapatia nguvu na ari ya kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Bikira Maria ni Mama anayejali ustawi na mafao ya watoto wake, kamwe hawezi kuwaacha pweke na yatima. Katika safari ya maisha yao, watu wa Mungu nchini Ufilippini watambue kwamba, wamekuwa daima wakisindikizwa kwa sala, maombezi na tunza ya Bikira Maria. Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria katika Pentekoste mpya ya Kanisa katika mchakato wa uinjilishaji nchini Ufilippini, awalinde na kuwasindikiza ili kutafakari kwa kina na mapana Injili ya Familia, Njia ya Msalaba na Pentekoste mpya katika mchakato wa uinjilishaji nchini Ufilippini. Maandiko Matakatifu yanasema “Mmepata bure, toeni bure” Mt. 10:8. Huu ni wito wa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya imani. Baba Mtakatifu anakiri na kusema, ni shuhuda amini kwa jinsi ambavyo watu wa Mungu nchini Ufilippini wanavyojitahidi kurithisha imani kwa watoto wao ndani na nje ya nchi yao. Anawashukuru wale wote waliojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili na kwamba, hii itakuwa ni chachu ya kupyaisha imani na ari yao ya kutaka kurithisha imani kwa watoto wao. Wote waliopokea imani, wawe na shauku ya kutaka kuwarithisha jirani zao, ili kuwanogeshea matumaini na furaha ya Injili.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kukumbuka hija yake ya kitume nchini Ufilippini iliyomwezesha kukutana na bahari ya watu wa Ufilippini, akaonja ukarimu wao na kuona jinsi walivyokuwa wanachakarika, wanafurahia na kuadhimisha imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hizi ni amana na tunu msingi za maisha ya kiroho zinazopaswa kusongeshwa mbele hata katika nyakati za shida na changamoto za maisha. Katika mchakato wa utume wa Uinjilishaji, wanao watakatifu kutoka Ufilippini wanaowaombea na kuwasindikiza. Hawa ni Mtakatifu Pedro Calungsod na Mtakatifu Lorenzo Ruiz. Hawa ni Makatekista wawili ambao wametangaza na kushuhudia utakatifu wa maisha katika utume wao. Walipokea bure na wametoa bure kabisa kwa ndugu zao katika Kristo Yesu. Watu wa Mungu nchini Ufilippini watambue kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro yuko pembeni mwao na anawaombea baraka kutoka kwa Kristo Yesu, wapate ulinzi na tunza kutoka kwa Bikira Maria pamoja na watakatifu wa Mungu akina Nino!

Papa Jubilei 500
08 April 2021, 15:15