Bango la Mkutano wa Kikundi cha Benki ya Dunia na Mfuko wa Fedha ya Kimataifa. Bango la Mkutano wa Kikundi cha Benki ya Dunia na Mfuko wa Fedha ya Kimataifa. 

Papa Francisko:Kufikiria mitindo mipya na ubunifu kwa ajili ya wakati ujao wa dunia!

Papa Francisko ametuma ujumbe wake kupitia Kardinali Peter Turkson,rais wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu kwa washiriki wa Mkutano wa Banki ya Dunia na Mfuko wa Fedha wa Kimataifa.Katika ujumbe wake anasema"Ulimwengu baada ya janga uwe wa mshikamano,jumuishi na kuhakikisha ufikiaji wa wema kwa nchi zote na watu wote hasa chanjo kwa sasa".

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Wakati ambao fedha zinakuwa katika huduma ya wema wa watu, mahali ambao walio hatarini na waliobaguliwa wanawekwa katikati na mahali ambamo dunia, ambayo ni nyumba yetu ya pamoja vinatunzwa, ndiyo matashi mema ya Papa Francisko ambayo amewatakia familia nzima ya kibinadamu na ambayo amefafanua katika ujumbe wake aliowatumia Kikundi cha Banki ya Dunia na Mfuko wa kifedha wa Kimataifa katika fursa ya Mkutano wao wa msimu huu 2021. Ili kufikia malengo hayo kwa mujibu wake, anasema kuna haja ya kufikiria mitindo mipya, ubunifu na fungamanishi kwa washiriki wa kijamii, kisiasa na kiuchumi. “Kuanzia utambuzi, katika wakati huu wa janga, mshikamano wa chanjo ambao unafadhiliwa ipasavyo, ili sheria ya soko isishinde juu ya sheria ya upendo na afya ya wote”.

Urejesho gusirudi katika hali ya kawaida

Papa Francisko anashukuru kuweza kushirikisha ujumbe wake katika kazi inayoendelea ambayo haiwezi kupuuza safu za mzozo mkubwa wa kijamii na kiuchumi, kiekolojia na kisiasa uliosababishwa na Covid - 19 na mara moja ameeleza matumaini kwamba kazi hizi zitaelekezwa kuelekea mfano wa kuanza upya na inaoweza kutekeleza suluhisho endelevu zaidi kwa ajili ya  faida ya wote. Papa anaandika: “Wazo la kuanza upya haliwezi kuridhishwa na kurudi nyuma kwa mfano usio sawa na usioweza kudumishwa wa maisha ya kiuchumi na kijamii, ambapo idadi ndogo sana ya watu duniani inamiliki nusu ya utajiri wake”.

Hata katika fedha, utamaduni wa kukutana ushinde

Papa Francisko amekumbusha washiriki jinsi leo hii wanaume na wanawake wengi wanaishi pembezoni mwa jamii na kiukweli wametengwa na ulimwengu wa kifedha na kwa maana hiyo inadhihirisha kwamba ikiwa ulimwengu wa janga la kutoka tukiwa bora tunahitaji kubuni aina mpya na za ubunifu za ushiriki wa kijamii, kisiasa na kiuchumi, nyeti kwa sauti ya maskini na kujitoa kuwajumuisha katika ujenzi wa mustakabali wetu wa pamoja”. (rej. Fratelli Tutti, 169). Hili ni suala la kuhamasisha utamaduni wa kukutana pia katika nyanja ya uchumi na kifedha, ambapo kila mtu anaweza kusikilizwa na ambapo ukuaji wa uaminifu na uhusiano unaruhusu kila mtu kustawi. Jambo la lazima na la dharura kwa mujibu wa Papa Francisko, kwa maana hiyo, “ni kushinda leo hii maono ya kibinafsi ya kupona kwa nchi moja moja ili kutoa uhai kwa ajili ya mpango ambao umetazamiwa na taasisi mpya au kupyaishwa ule uliokuwapo, hasa ule wa utawala wa ulimwengu, mpango ambao husaidia kujenga mtandao mpya wa uhusiano wa kimataifa kwa ajili ya maendeleo ya watu wote. Kwa hiyo, hata mataifa maskini lazima yahakikishe kushiriki katika michakato ya kufanya maamuzi na ufikiaji wa soko, kwa kiasi kikubwa ili kupunguza deni la kimataifa ambalo janga hili limefanya kuwa mzigo mzito zaidi. Kwa kupunguza mzigo wa deni wa nchi na jumuiya nyingi leo hii ni ishara kubwa ya kibinadamu ambayo inaweza kusaidia watu kuendelea na kupata chanjo, afya, elimu na kazi”.

Deni la kiekolojia kuelekea ulimwengu wa kusini

Papa Francisko katika ujumbe huo anatoa mwaliko wa kutopuuza “deni lingine: yaani deni la kiekolojia ambalo liko juu ya yote kati ya kaskazini na kusini mwa ulimwengu na kwa sababu ya uharibifu wa mazingira uliosababishwa na mwanadamu”,  Papa anasema ana imani katika suluhisho linalowezekana la kulipa deni hili na anaandika: “Ninaamini kwamba tasnia ya kifedha, ambayo inasimama kwa ubunifu wake mkubwa, itathibitisha kuwa na uwezo wa kuunda njia za kukokotoa hesabu za deni hili la kiekolojia, ili nchi zilizoendelea ziweze kulipia, na sio tu kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi yao ya nishati isiyoweza kurejeshwa au kwa kuzisaidia nchi maskini kutekeleza sera na mipango ya maendeleo endelevu, lakini pia kwa kulipia gharama za uvumbuzi zinazohitajika kwa sababu hiyo . (taz. Laudato si ', 51-52)”.

Kipaumbele ni cha faida na wema kwa wote

Katika Ujumbe wake, Papa Francisko anaangazia umakini wa kile ambacho  kinapaswa kuwa lengo la maisha yote ya kiuchumi, ambayo ni faida kwa wote. Ikiwa kanuni hii inashirikishwa, matokeo kwa jumuiya ya kimataifa ni mshikamano ambao unakwenda zaidi ya vitendo vya ukarimu mara kwa mara. Inamaanisha kuwa maisha ya wote yana kipaumbele kuliko kujilimbikiza mali kwa walio wachache tu. Inamaanisha pia kupambana na sababu za kimuundo za umaskini, ukosefu wa usawa, ukosefu wa kazi, ardhi na makazi, kunyimwa haki za kijamii na za kazi ... Mshikamano, unaoeleweka kwa maana yake ya kina, ni njia ya kutengeneza historia. (Ndugu Wote, 116).

Wito wa kuhakikisha chanjo ya kupambana na Covid kwa kila mtu

Masoko, hasa masoko ya kifedha, Papa Francisko ameendelea kueleza kuwa , hayajitawali peke yake, kwa sababu kanuni na sheria zinahitajika ili kuhakikisha kuwa fedha inafanya kazi kwa malengo ya kijamii yanayohitajika sana wakati wa dharura ya sasa ya afya duniani kwa sababu, kulingana ujumbe huo , “hatuwezi ruhusu sheria ya soko kutawala sheria ya upendo na afya ya wote”  .Wito wa  Papa Fransisko kwa wakuu wa serikali, wafanyabiashara na mashirika ya kimataifa kwa maana hiyo ni  “kufanya kazi pamoja ili kutoa chanjo kwa wote, hasa kwa walio hatarini zaidi na wahitaji”(taz Urbi et Orbi Ujumbe wa Noeli 2020).

Kitovu kiwe kwa wenye mazingira magumu zaidi na nyumba yetu ya pamoja

Papa Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa kuwatakia Mikutano ya msimu huu 2021 ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa iwe kazi yenye matunda kwa siku za usoni ambapo fedha ziweze hudumia kwa ajili ya faida ya wote, na zaidi  walio katika mazingira magumu na waliotengwa waweze kuwa kitovu na ambapo dunia, nyumba  yetu ya pamoja, inatunzwa vizuri. Na juu ya washiriki wote amewaombea zawadi za Mungu ya hekima, ufahamu, ushauri mwema, nguvu na amani.

09 April 2021, 09:53