Baba Mtakatifu Francisko: Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala amewahimiza waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kutafakari maisha ya Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Francisko: Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala amewahimiza waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kutafakari maisha ya Kristo Yesu. 

Papa Francisko Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala: Tafakari Makini!

Sala kama Tafakari kwa Mkristo ni muhtasari wa Ufunuo wa Mungu unaonafsishwa katika maisha. Kutafakari kile ambacho mtu anasoma humwongoza kukifanya kuwa chake kwa kukipambanisha na yeye mwenyewe. Hapa ni kile kitabu kile Kitabu cha maisha. Mtu hupitia mawazo kufikia ukweli. Imani na unyenyekevu humsaidia mtu kujipambanua katika mambo msingi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi yake kuhusu Fumbo la Sala anasema hii ni chemchemi ya imani na kilio kinachobubujika kutoka katika undani wa mwamini kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu.  Ameendelea kujikita katika: Sala na Utatu Mtakatifu kwa kujielekeza zaidi kwa Roho Mtakatifu anayewafunulia watu kumhusu Kristo Yesu. Roho Mtakatifu anao uwezo wa kuchunguza hata Mafumbo ya Mungu. Ni Mungu peke yake anayemjua Mungu kabisa. Kanisa linamsadiki Roho Mtakatifu kwa sababu ni Mungu na kamwe haliachi kutangaza imani kwa Mungu mmoja: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Kanisa ni Mama, Mwalimu na Shule ya Sala. Imani inapyaishwa kwa njia ya sala na kwamba, kuna mitindo mbalimbali ya sala, ili kuweza kuzungumza na Mwenyezi Mungu: Sala ya Sauti, Sala Fikara au Tafakari na Taamuli.

Baba Mtakatifu amegusia kuhusu umuhimu wa utume wa sala na changamoto zake. Kanisa lina dhamana ya kusali na kufundisha namna ya kusali vizuri zaidi. Kanisa ni shule kuu ya sala. Kristo Yesu ni njia ya kwenda kwa Baba wa mbinguni na kabla ya kupaa kwake kwenda mbinguni aliwaahidia kwamba, atawaombea kwa Baba yake wa mbinguni ili kwa jina lake awaletee Roho Mtakatifu na Roho wa kweli atakaye kaa pamoja nao milele yote. Roho Mtakatifu atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote walioambiwa na Kristo Yesu alipokuwa angali kati yao! Rej. Yn. 14: 25-26; 16:12-15. Kristo Yesu aliwaambia wafuasi wake kwamba, bado alikuwa na mambo mengi ya kuwaambia. “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari. Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni habari”. Yn. 16:13-15.

Hii ni sehemu ya Maandiko Matakatifu iliyoongoza Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 28 Aprili 2021 kuhusu Fumbo la Sala na kwa wakati huu, amejielekeza zaidi katika Sala kama Tafakari kwa Mkristo ni muhtasari wa Ufunuo wa Mungu unaonafsishwa katika maisha ya mwamini. Mababa wa Kanisa wanasema, kutafakari kile ambacho mtu anasoma humwongoza kukifanya kuwa chake kwa kukipambanisha na yeye mwenyewe. Hapa kitabu kingine kinafunguliwa: kile cha maisha. Mtu hupitia mawazo kufikia ukweli. Kadiri ya kipimo cha unyenyekevu na imani mtu hugundua mienendo inayoamsha moyo na anaweza kujipambanua. Rej. KKK. 2706. Katika Katekesi yake kuhusu Tafakari, Baba Mtakatifu amegusia kuhusu historia ya Tafakari; Umuhimu na aina mbalimbali za Tafakari za Kikristo na neema inayobubujika kutoka katika Sala ya Kikristo! Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na maendeleo makubwa sana kuhusu Tafakari, si tu kwa Wakristo bali hata kwa wale wasioamini sanjari na waamini wa dini mbalimbali duniani.

Watu wa Mungu wana haja ya kutafakari, kucheua kile walichosoma ili kugundua undani wao. Kwa bahati mbaya, kwa watu wa Mungu Barani Ulaya, tafakari imekuwa ni sehemu ya mchakato wa kupambana na msongo wa mawazo unaowaandama kila kukicha pamoja na kutaka kuziba utupu uiliomo ndani mwao. Utawakuta vijana na wazee wamekaa kwa amani na utulivu, huku macho yao yakiwa yamefumba, ili kutafakari. Huu ni mwelekeo mzuri wa maisha unaopaswa kuigwa na wengi. Kila siku mwanadamu yuko katika “pilika pilika nguo kuchanika”, ndiyo maana kuna haja ya kusimama na kutafakari kidogo, ili kurutubisha undani wa maisha ya mwanadamu. Watu wote wanahitaji kutenga muda kwa ajili ya Kutafakari! Baba Mtakatifu anakaza kusema, kama waamini wanapaswa kujenga na kudumisha utamaduni wa Kutafakari kwani Kristo Yesu ni lango kuu la sala ya Mkristo. Na tafakari inafuata mfumo huu wa maisha. Sala ya tafakari inayotolewa na Mkristo hailengi kukutana na ukweli wa mtu binafsi au hali ya kujitafuta, bali lengo kuu ni kukutana na Mwenyezi Mungu, ili kupata amani na utulivu wa ndani.

Sala ya Tafakari linawawezesha waamini kupata ustadi wa kujifahamu wao wenyewe na mwanga katika mapito ya maisha, baada ya kukutana na Kristo Yesu katika maisha ya sala. Tafakari katika historia imepata maana tofauti sana. Neno Tafakari katika Ukristo ina maanisha mang’amuzi mbalimbali ya maisha ya kiroho. Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, njia za fikara ni nyingi kama walivyo wengi walimu wa kiroho. Mkristo lazima awe na kawaida ya kutafakari kama udongo mzuri ili aweze kuzaa matunda kwa wakati wake. Jambo muhimu ni kuendelea pamoja na Roho Mtakatifu, juu ya ile njia moja ya sala: Kristo Yesu. Rej. KKK. 2707. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kuna njia mbalimbali za kutafakari na zote ni muhimu, kumbe, zinapaswa kufanyiwa kazi, ili mwamini aweze kupata mang’amuzi ya imani: kiroho na kimwili. Waamini wajifunze kusali kutoka katika sakafu ya nyoyo zao, ili kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu katika undani wa maisha yao.

Fikara hushughulisha wazo, dhana, hisi na tamaa. Msukumo huu ni wa lazima ili kunafsisha maswali ya imani, kuamsha wongofu wa moyo na hatimaye, kuimarisha utashi wa kumfuata Kristo Yesu: “Sequela Christi”. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Sala ya Kikristo inapendelea kutafakari “Mafumbo ya Kristo”. Rej. KKK. 2708. Neema ya Sala ya Kikristo inamwezesha mwamini kutambua na kuimarisha mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu, Mungu kweli na Mtu kweli, mahali pa wokovu na chemchemi ya furaha ya kweli yanayobubujika kutoka katika maisha ya Kristo Yesu. Ni kwa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu anayewaongoza na kuratibu shughuli zote hizi kiasi kwamba, waamini wanaweza kuzama tena katika Mto Yordan na kupokea Ubatizo. Waamini watambue kwamba, hata wao ni washirika wa muujiza wa harusi ya Kana ya Galilaya unaofumbatwa kwa uwepo wa Kristo Yesu anayejifunua kati ya watu wake kama Bwana harusi, aliyetangazwa na kushuhudiwa na Manabii na kwamba, Yeye ndiye kiini cha Agano Jipya linalojikita katika upendo wa kweli.

Kristo Yesu anawakirimia waja wake divai nzuri zaidi kwa ajili ya wanandoa. Anawaganga na kuwaponya maelfu ya watu. Katika sala, mwamini anakuwa kama yule mgonjwa wa ukoma aliyeponywa na kutakaswa; sawa na Bartimayo, yule kipofu ambaye ni kati ya watu wenye mvuto wa pekee sana katika fumbo la sala, alikuwa na vituko, utachoka na roho yako, kiasi cha kupewa fursa ya kujibizana na Kristo Yesu. Ni sawa na Lazaro aliyekuwa amekufa, akafufuliwa. Kwa hakika kurasa zote za Maandiko Matakatifu ni mahali muafaka pa Tafakari, ili kuweza kukutana na Kristo Yesu na hatimaye, kuweza kujifahamu wao wenyewe! Yote haya yanawezekana kwa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu.

Papa tafakari

 

28 April 2021, 15:21

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >