Papa Francisko Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala: Mama Kanisa ni Mwalimu na Shule ya Sala na Umoja wa Waamini. Papa Francisko Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala: Mama Kanisa ni Mwalimu na Shule ya Sala na Umoja wa Waamini. 

Papa: Kanisa Ni Mwalimu na Shule ya Sala na Umoja wa Waamini!

Papa Francisko: Fumbo la Sala: Kanisa ni Mwalimu na Shule ya Sala. Imani inapyaishwa kwa njia ya sala; Amegusia kuhusu umuhimu wa Utume wa Sala na changamoto zake. Kanisa lina dhamana ya kusali na kufundisha namna ya kusali vizuri. Kanisa ni shule kuu ya Sala. Waamini wengi wamejifunza kusali kutoka kwa wazazi na walezi wao wakati walipokuwa watoto wadogo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko bado anaendelea na Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala, chemchemi ya imani na kilio kinachobubujika kutoka katika undani wa mwamini kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Kitabu cha Matendo ya Mitume, kinaelezea jinsi waamini walivyozama katika Sala huku wakiomba moyo wa ujasiri. “Hata walipofunguliwa, wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa na wakuu wa makuhani na wazee. Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo… Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu. Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.” Mdo. 4: 23-24. 29-31.

Baba Mtakatifu katika Katekesi yake Jumatano tarehe 14 Aprili 2021, ametafakari kuhusu Fumbo la Sala na kwamba, Kanisa ni Mwalimu na Shule ya Sala. Imani inapyaishwa kwa njia ya sala; Amegusia kuhusu umuhimu wa Utume wa Sala na changamoto zake. Kanisa lina dhamana ya kusali na kufundisha namna ya kusali vizuri zaidi. Kanisa ni shule kuu ya Sala. Waamini wengi wamejifunza kusali kutoka kwa wazazi na walezi wao wakati walipokuwa watoto wadogo. Wazazi walikuwa wanawafundisha watoto wao Sala za Usiku kabla ya kwenda kulala. Hiki ni kipindi muafaka ambacho wazazi wanaweza kusikiliza undani wa maisha ya watoto na kuwapatia ushauri makini unaobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu. Kanisa linalo safiri hapa duniani linajiunga katika sala yake na ile sala ya watakatifu ambao linaomba maombezi yao. Shule mbalimbali za maisha ya kiroho ya Kikristo hushiriki kutoa Mapokeo hai ya sala na ni viongozi bora wa maisha ya kiroho. Kwa ufupi, watumishi wa sala ni familia ya Kikristo, Wahudumu wenye daraja na watawa, katekesi za watoto pamoja na vikundi vya sala. Rej. KKK 2686-2687.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, maisha ya Parokia na Jumuiya mbalimbali za Kikristo yamegawanyika katika vipindi vya Liturujia ya Kanisa na sala ya jumuiya. Hii ni amana na utajiri mkubwa katika maisha ya kiroho. Katekesi inalenga kile ambacho Neno la Mungu litatafakariwa katika sala ya mtu binafsi, likitekelezwa katika sala ya Liturujia na likipenyezwa ndani ya mioyo kwa nyakati zote ili kuzaa matunda yake katika maisha mapya. Hapa ni mahali pa kukuza na kulea ibada na uchaji wa Mungu. Rej. KKK 2688. Moyo na utamaduni wa sala unajionesha katika nyakati mbalimbali za maisha, wakati wa matatizo na changamoto za maisha; “wakati wa kuteleza na kuanguka” na hata wakati wa kufufuka. Sala ni roho ya imani, kwani waamini wanaweza kukua na kukomaa kadiri wanavyojitahidi kujifunza kusali. Watu wa sala, mara nyingi wanaombwa, kuwasindikiza jirani zao katika shida na mahangaiko yao kwa njia ya sala!

Imani bila sala, mwamini “hawezi kufua dafu hata kidogo”. Sala binafsi na sala ya jumuiya ni muhimu sana katika maisha ya mwamini. Ndani ya Kanisa anasema Baba Mtakatifu Francisko, kila kukicha kuna makundi yanayojisadaka kwa ajili ya sala yanayoendelea kujitokeza, kiasi kwamba, kuna watu ambao sala ni kati ya vipaumbele vyao vya kwanza katika maisha. Ndani ya Kanisa kuna monasteri na nyumba za kitawa ambamo wanaishi humo watu waliowekwa wakfu kwa Mungu. Maeneo haya yamekuwa na mvuto sana wa maisha ya kiroho. Pamekuwa ni chemchemi ya sala na mchakato wa ujenzi wa umoja wa udugu wa kibinadamu. Ni viungo muhimu katika ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya Kanisa na jamii katika ujumla wake, chemchemi ya utamaduni wa Bara la Ulaya na tamaduni nyinginezo. Sala na kazi ni chachu inayosongesha mbele maendeleo ya ulimwengu.

Maisha na utume wa Kanisa unapata chimbuko na asili yake katika maisha ya sala. Ikiwa kama Shetani, Ibilisi anataka kupambana na Kanisa, kwanza kabisa anaharibu ari na moyo wa sala. Waamini lazima wajenge tabia ya kusali na wala si kuangalia jinsi watu wanavyo sali, kwa kufungua nyoyo zao kwa Roho Mtakatifu. Mageuzi ndani ya Kanisa yatafanikiwa tu, ikiwa kama yanapata chimbuko lake katika maisha ya sala. Mwamini anaweza kudhani kwamba, yote yanakwenda kama yalivyopangwa hata bila sala, lakini baadaye, atagundua kwamba, amepoteza dira na mwelekeo wa maisha, anakosa nguvu na joto la upendo. Watakatifu wa Mungu daima wamekuwa na maisha magumu, lakini wameweza kusonga mbele na kukabiliana na changamoto za maisha kwa njia ya sala ambazo wamezichota kutoka katika amana na utajiri wa Mama Kanisa. Kwa njia ya sala wakapyaisha imani, matumaini na mapendo. Watakatifu wa Mungu machoni pa walimwengu wanaonekana kana kwamba, “si mali kitu”. Hawa ni watu wanaopambana kwa kutumia silaha ya sala na wala si fedha, madaraka au njia za mawasiliano ambazo nazo kwa sasa zimekuwa na nguvu na ushawishi mkubwa!

Kuhusu udumifu katika maisha ya sala bila kuchoka, Kristo Yesu katika Injili ya Luka anauliza swali msingi “walakini atakapokuja Mwana wa Adamu, Je, ataiona imani duniani?”. Lk. 8:8. Baba Mtakatifu anaongeza kwa kuuliza swali Je, atawakuta wafanyabiashara wa imani? Taa ya imani itaendelea kuwaka duniani, ikiwa kama waamini wanasali kweli kweli. Sala inaweza kuwainua wanyonge, wadhaifu na wadhambi katika maisha yao. Waamini wasali ndani ya Kanisa pamoja na Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Baba Mtakatifu amehitimisha Katekesi yake kuhusu Fumbo la Sala kwa kusema kwamba, Kanisa lina dhamana ya kusali na kufundisha waamini namna ya kusali vizuri zaidi. Mama Kanisa anapaswa kuhakikisha kwamba, anarithisha moyo wa sala kwa vizazi vyote. Ni kwa njia ya mwanga wa imani, Kanisa linapata nguvu ya kuinjilisha; kuwahudumia maskini sanjari na kukutana kama jumuiya kwa ajili ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa. Bila imani yote ni bure na bila sala, imani inazimika. Ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anasema Kanisa ni: Nyumba, Shule ya sala na Umoja!

Fumbo la Sala

 

14 April 2021, 15:19

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >