Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.
Papa Francisko kama Askofu wa Roma anarudia kwa mara nyingine tena kutoa daraja la ukuhani katika jimbo lake. Mwaka jana, tukio hilo liliharishwa kutokana na janga la Covid-19 na kufanywa na Makamu wake Kardinali Angelo De Donatis katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Roma. Kwa maana hiyo tarehe 25 Aprili 2021 saa tatu kamili, siku ambayo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika IV ya Kipindi cha Pasaka na siku ya Mchungaji mwema, Papa Francisko ataongoza Ibada hiyo katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, Vatican. Vijana watakaowekwa wakfu wa kikuhani ni tisa na kwa sasa wako katika mafungo ya kiroho kwa kijiandalia vema siku hii muhimu kwao na kwa Kanisa la Roma.
Hata hivyo majiundo yao yamepitia katika seminari tofauti za jimbo. Vijana sita wamesomea katika Seminari Kuu ya Kipapa ya Roma. Hawa ni Georg Marius Bogdan, Salvatore Marco Montone, Manuel Secci, Diego Armando Barrera Parra, Salvatore Lucchesi na Giorgio De Iuri. Wawili wamesomea katika Taasisi ya Redemptoris Mater na ambao ni Riccardo Cendamo na Samuel Piermarini na wakati hu huo mmoja amesomea kwenye Seminari ya Mama wa Mungu Upendo (Madonna del Divino Amore), jina lake ni Mateus Henrique Ataide da Cruz. Maadhimisho hayo katika Kanisa Kuu yataanyika kijimbo na kutangazwa moja kwa moja kupitia vyombo vya habari Vatican, Telepace, Tv2000 na kwenye ukurasa wa Facebook wa jimbo.
