2021.04.05 Sala ya Malkina wa Mbingu 2021.04.05 Sala ya Malkina wa Mbingu  

Papa Francisko:Tusichoke kamwe kumtafuta Kristo Mfufuka,anatoa maisha tele!

Inaitwa Jumatatu ya Malaika kwa sababu ni siku ambayo wanawake walitangaziwa na Malaika kuwa Yesu amefufuka.Kristo ni mzima.Kristo anasindikiza maisha yangu,Kristo yuko karibu nami.Kristo anabisha katika mlango wa moyo wangu.Anayempata Yesu anagundua ni kwa jinsi gani ana amani rohoni.Ni lazima kumwachia Yesu alingie ndani yako.Ndiyo ushauri wa Papa katika tafakari kabla ya Sala ya Malkia wa Mbingu.

Na Sr. Angela Rwezaula - Vatican.

Papa Francisko ameanza tafakari yake kabla ya sala ya Malkia wa mbingu, Jumatatu tarehe 5 Aprili 2021, akiwa katika Maktaba ya Jumba la Kitume, Vatican, akiongozwa na Injili ya siku akisisizizia suala ya Tangazo la Malaika na ushuhuda halisi wa tukio la ufufuko.  Akianza amesema “Jumatatu baada ya Pasaka inafafanuliwa vile vile kama Jumatatu ya Malaika kwa sababu inakumbusha mkutano wa Malaika na wanawake waliofika katika kaburi la Yesu (Mt 28,1-15). Na kwao Malaika aliwambia “ninajua mnamtafuta Yesu, msulibiwa. Hayupo hapa. Amefufuka! (Mt 28,5-6). Papa akiendelea amesema “Kielelezo hiki “Amefufuka kinakwenda zaidi ya uwezo wa binadamu. Hata wanawake waliokuwa wamekwenda katika kaburi na walikuwa wamekuta limefunguliwa na tupu wasingeweza kuthibitisha kuwa “Amefufuka, bali kusema kuwa  kaburi lilikuwa wazi. Na wasingeweza kusema hivyo  Yesu alikuwa amefufuka bali   ni malaika kama yule Malaika aaliyekuwa amemwambia   Maria kuwa “utazaa mwana(…) na ataitwa Mwana wa Aliye juu” (Lk 1,31) . Ndiyo maana tunasema  ni Jumatatu ya Malaika kwa sababu ni Malaika tu kwa nguvu ya Mungu anaweza kusema Yesu amefufuka”, amefafanua Papa Francisko.

Mipango yote na ulinzi wa maadui na watesaji wa Yesu ilikuwa ya bure

Papa akiendelea na tafakari hiyo amesema Mwinjili Matayo ambaye anasimulia kuwa alfajiri ya Pasaka,  kulitokea tetemeko kuu. Malaika wa Bwana kwa hakika alishuka kutoka mbinguni na kukaribia, alilivingilisha jiwe na kukaa juu yake. Lile jiwe kubwa ambalo lingekuwa kama na mhuri wa ushindi wa ubaya na kifo badala yake liliwekwa chini  ya miguu na likawa kiti cha miguu ya  Malaika wa Bwana. Mipango yote na ulinzi wa maadui na watesaji wa Yesu ilikuwa ya bure. Mihuri yote ilianguka! Sura  ya Malaika aliyekaa juu ya Jiwe la Kaburi ni onesho wazi, linaloonekana, la ushindi wa Mungu dhidi ya ubaya, ushindi wa Yesu wa Mfalme wa ulimwengu huu, wa mwanga dhidi ya giza.  Kaburi la Yesu halikufunguliwa kwa ajili ya matukio ya kimwili, lakini ni tukio la Bwana. Sura ya Malaika kwa mujibu wa Matayo alikuwa anang’aa na mavazi yake meupe kama theruji. Maelezo haya ni ishara ambazo zinathibitisha mwingilio wa Bwana mwenyewe, wa kueleza wakati mpya, wa nyakati za mwisho za kihistoria. Hii ni kwa sababu katika ufufuko wa Yesu ndipo inaanza wakati wa mwisho wa historia ambayo inapelekea kudumu miaka elfu mbili lakini ya wakati wa mwisho.

Uongo wa walinzi na kupewa fedha wasiseme ukweli

Mbele ya muktadha huu wa Mungu inatokeza mambo mawili. Kwanza la walinzi ambao  hawakujua namna ya kukabiliana na nguvu za kiajabu ya Mungu na walichanganyikiwa na tetemeko la kiroho, kwani walikuwa wanaogopa sana. Nguvu ya ufufuko iliwagonga wale ambao walikuwa wametumia ili kuhakikisha kijuu juu ushindi wa kifo. “Je walinzi hawa wafanye nini? kwenda kwa wale waliokuwa wamewapa shughuli ya ulinzi na kusema ukweli. Walikuwa mbele ya chaguzi; kusema ukweli au kujiachia waaminishwe na wale waliowapa  kazi ya kulinda. Na ndiyo namna walivyo jiaminisha kwa kupewa fedha mfukoni ili waseme uongo kuwa walikuja wafuasi wale na kuiba mwili wake. Bwana fedha ambaye hata hapa katika ufufuko wa Kristo Papa amebainisha kwamba ana uwezo wa kumkana Bwana”.

Mwelekeo wa wanawake ni tofauti maana waliambiwa wasiogope

Mwelekeo wa wanawake ni tofauti, kwa sababu wao walialikwa moja kwa moja na Malaika wa Bwana kuwa wasiogope na mwisho  hawakuogopa Papa amesisisitiza. “Ninyi msiogope na msitafute Yesu katika kaburi.”  Kutoka katika maneno ya Malaika tunaweza kupokea mafundisho yenye thamani sana, kwamba tusichoke kamwe kumtafuta Kristo Mfufuka, ambaye anatoa maisha kwa wingi kwa wale wanaokutana naye. Kumpata Kristo maana yake ni kugundua amani ya moyo. Wawake wale wa Injili, baada ya wasiwasi wa kwanza, walihisi furaha kubwa ya kumwona akiwa hai, Mwalimu wao. Katika kipindi  hiki  cha Pasaka, Baba Mtakatifu anawatakia  mema wote kufanya uzoefu wa kiroho, wa kupokea katika moyo wao, katika nyumba na katika familia habari njema ya Pasaka: Kristo amefufuka na hafi tena, kifo hakina uwezo juu yake (kutoka katika Wimbo wa komunio).

Kristo ni mzima, Kristo ananisindikiza na yuko karibu nami

Papa amesema  “Tangazo la Pasaka, Kristo ni mzima, Kristo anasindikiza maisha yangu, Kristo yuko karibu nami. Kristo anabisha katika mlango wa moyo wangu kwa sababu niache aingie, Kristo ni hai. Katika siku hizi za Pasaka, itakuwa vema kwetu sisi kurudia kusema “Kristo anaishi!” Hakika ukweli huu unatupeleka kusali leo hii na wakati wa kipindi chote cha Pasaka, sala ya “Regina Caeli, laetare”, yaani Malkia wa Mbingu furahaia.  Papa ameongeza kusema kuwa “Malaika Gabrieli alikuwa amemsalimia kwa mara ya kwanza “Furahia, wewe  uliyejaa  neema (Lk 1,28). Na sasa furaha ya Maria imejaa kwani Yesu anaishi, upendo umeshinda. Kwa maana hiyo upendo huo uweze kuwa hata furaha yetu! Amehitimisha.

Ushuhuda wa furaha

Mara baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu Papa Francisko ametoa salamu zake kwa washiriki wote wa sala kwa njia ya vyombo vya habari na wazee akikumbusha umuhimu wa kujionesha hasa katika kipindi cha Pasaka “ushuhuda wa furaha”. Papa amesema: Wazo langu linawaendea kwa namna ya pekee wazee na wagonnjwa ambao wameunganishwa kwa njia ya vyombo vya habari wakiwa katika nyumba zao au nyumba za mapunziko. Kwao ninawatumia neno la kuwatia moyo na kuwa naw utambuzi wa ushuhuda wao: Niko karibu nao. Na kwa wote ninawatakia kuwa na imani kuu katika siku hizi za Oktava ya Pasaka ambayo inarefusha kumbu kumbu ya ufufuko wa Kristo. Tumieni kila fursa nzuri kwa ajili ya kushuhudia furaha na amani ya Bwana Mfufuka.

PAPA JUMATATU YA MALAIKA
05 April 2021, 15:18

Sala ya Malkia wa Mbingu ni nini?
 

Utenzi wa Malkia wa Mbingu ni kati ya tenzi nne za Bikira Maria (nyingine ni:Tunakimbilia Ulinzi wako,  Salam Malkia wa Mbingu, Salam Malkia). Kunako mwaka 1742, Papa Benedikto XIV alipoandika kwamba, waamini wasali Sala ya Malkia wa Mbingu wakiwa wamesimama, kama alama ya ushindi dhidi ya kifo, wakati wa Kipindi cha Pasaka, yaani kuanzia Domenika ya Ufufuko wa Bwana hadi Sherehe ya Pentekoste. Hii ni Sala ambayo husaliwa mara tatu kwa siku kama ilivyo pia Sala ya Malaika wa Bwana: Asubuhi, Mchana na Jioni ili kuweka wakfu Siku kwa Mwenyezi Mungu na Bikira Maria.

Utenzi huu kadiri ya Mapokeo ulianza kutumika kunako karne ya VI au Karne X, lakini kuenea kwake kunaanza kujitokeza katika nyaraka mbali mbali kati kati ya Karne ya XIII, ilipoingizwa kwenye Kitabu cha Sala za Kanisa cha Wafranciskani. Hii ni Sala inayoundwa na maneno mafupi manne yanayohitimishwa na Alleluiya na sala ya waamini wanaomwelekea Bikira Maria, Malkia wa mbingu, ili kufurahia pamoja naye kuhusu Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu.

Papa Francisko tarehe 6 Aprili 2015 wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, siku moja baada ya Sherehe ya Pasaka, aliwashauri waamini kuwa na moyo wa furaha wanaposali sala hii. “Tunamwendea Bikira Maria, tukimwomba afurahi, kwa sababu yule Mwanaye mpendwa aliyekuwa amemchukua mimba amefufuka kweli kweli kama alivyosema; tunajiaminisha kwa sala na maombezi ya Bikira Maria. Kimsingi furaha yetu ni mwangi wa furaha ya Bikira Maria kwani ndiye aliyetunza na anaendelea kutunza matukio mbali mbali ya maisha ya Yesu. “Tusali sala hii kwa furaha ya kuwa waana wa Mungu ambao wanafurahi kwa sababu Mama yao anafurahi”

 

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >