Mafuriko makubwa kutokana na kimbunga kiitwacho Seroja Mashariki ya Flores kimeleta madhara makubwa nchini Indonesia na Timor Mashariki. Mafuriko makubwa kutokana na kimbunga kiitwacho Seroja Mashariki ya Flores kimeleta madhara makubwa nchini Indonesia na Timor Mashariki. 

Papa akumbuka waathiriwa wa mafuriko nchini Indonesi na Timor Mashariki

Mara baada ya Katekesi,Papa Francisko amekumbuka na kusali kwa ajili ya wale wote waliopoteza maisha yao,majeruhi na kupoteza makazi huko Kusini Mashariki mwa bara la Asia yaani Indonesia na Timor ya Mashariki kutokana na mafuriko makubwa yaliyosababaishwa na Kimbunga kikali ambacho tangu Jumamosi kimeleta madhara makubwa.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Zaidi ya watu mia moja wamekufariki, lakini idadi inaendelea kusasishwa kila wakati, kwa sababu ya kimbunga kiitwacho Seroja ambacho kimegonga mashariki mwa Indonesia na Timor ya Mashariki na mvua kubwa, ambayo imesababisha mito kufurika na  maporomoko ya ardhi. Barabara nyingi zimezibwa na vijiji vyote vimezama kwenye matope. Kuna makadirio ya mamia, labda maelfu, ya waliokimbia makazi yao. Ni hali ya kushangaza ambayo Papa amezungumzia hata mwishoni mwa katekesi yake, Jumatato tarehe 7 Aprili 2021.

Katika maneno ya Papa amesema: “Ninapenda kuhakikishia kumbukumbu yangu katika sala kwa wahanga wa mafuriko yaliyoikumba Indonesia na Timor ya Mashariki katika siku za hivi karibuni. Bwana awapokee marehemu, awape nguvu familia na kuwasaidia wale wote ambao wamepotea makazi yao”.

Wakati huo huo, hali mbaya ya hewa inapunguza juhudi za utoaji wa misaada katika eneo la ulimwengu huo  ambapo matukio ya hali kama hizi sio mapya.  Hii ni kutokana na kwamba mara kwa mara mvua za msimu huleta mafuriko na maporomoko ya ardhi, na kuathiri mamilioni ya watu wanaoishi katika maeneo ya milima au karibu na mabonde ya mafuriko kwa mujibu wa Joaquim José Gusmão dos Reis Martins, katibu mkuu wa nchi wa ulinzi wa raia.

07 April 2021, 16:14