Mama Kanisa amemtangaza Mtumishi wa Mungu Simeone Cardon na watawa wenzake 5 kuwa Wenyeheri na watakuwa wanakumbukwa kila mwaka tarehe 16 Mei. Waliuwawa kwa sababu ya chuki dhidi ya imani. Mama Kanisa amemtangaza Mtumishi wa Mungu Simeone Cardon na watawa wenzake 5 kuwa Wenyeheri na watakuwa wanakumbukwa kila mwaka tarehe 16 Mei. Waliuwawa kwa sababu ya chuki dhidi ya imani. 

Mwenyeheri Simeone Cardon na Wenzake 5: Mashuhuda wa Imani

Mtumishi wa Mungu Siméon Cardon na watawa wenzake watano, waliuwawa kikatili usiku wa kuamkia tarehe 14 Mei 1799. Wote hawa kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko wametangazwa kuwa wenyeheri na Kardinali Semeraro, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa tarehe 17 Aprili 2021 kwenye Abasia ya Casamari. Wenyeheri hawa walikuwa kutoka na chuki dhidi ya dini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kanisa linashiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa kutangaza na kushuhudia upendo wa huruma ya Mungu katika maisha na utume wake. Kanisa bado linasafiri kuelekea katika ukamilifu wake, kumbe, Injili itaendelea kutangazwa na kushuhudiwa; watu wataendelea kutubu na kuongoka, hadi kufikia utimilifu wake katika Fumbo la Ufufuko. Utume, ni kiini cha imani ya Kikristo na kwamba, Kanisa daima linapaswa kupyaishwa kutoka katika undani wake; ndiyo maana, Kanisa bado linaendelea kukazia umuhimu wa toba na wongofu wa ndani, ili kuambata harufu ya utakatifu unaobubujika kutoka kwa watakatifu, wafiadini na waungama imani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Msalaba ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa maisha na utume wa Wakristo. Ni katika muktadha huu, mateso, dhuluma, nyanyaso na mauaji ni mambo ambayo yameandika historia tangu mwanzo wa Kanisa. Lakini pamoja na patashika nguo kuchanika, hii ni sehemu ya mchakato wa uinjilishaji, ili kuhakiki uthabiti wa imani, na kuendelea kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu kama wamisionari walioitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu.

Waamini wawe na imani kwamba, kamwe Mwenyezi Mungu hatawaacha na wala hawana sababu msingi ya kuogopa! Huu ndio ukweli unaofumbatwa katika maisha ya waungama na wafiadini. “Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-kondoo.” Ufu. 7:14. Katika hija ya maisha yao hapa duniani, Wakristo wataendelea na mapambano ya maisha ya kiroho. Mwenyeheri Siméon Cardon alizaliwa Cambrai, nchini Ufaransa na wakati wa Mapinduzi ya Ufaransa alikataa katukatu kula kiapo cha utii kwa Mfalme Napoleone, hivyo ilimbidi kuikimbia Ufaransa na kunako mwaka 1795 kujikuta akiwa Frosinone, nchini Italia na hivyo kujiunga na Shirika la Cistercians wa Casamari. Akaweka nadhiri zake za daima tarehe 5 Mei 1797. Alikuwa ni mtawa aliyeonesha mfano bora wa maisha; akawajali na kuwathamini wagonjwa, kiasi kwamba, baadhi yao wakatubu na kumwongokea Mungu na kuwa watawa. Mwenyeheri Siméon Cardon na watawa wenzake watano, waliuwawa kikatili usiku wa kuamkia tarehe 14 Mei 1799. Akawasamehe watesi na wauaji wake.

Watawa waliouwawa pamoja naye ni Padre Domenico Maria Zawrel, Bro. Albertino Maria Maisonade, Bro. Modesto Maria Burgen, Br. Maturino Maria Pitri pamoja na Zosimo Maria Brambat. Wote hawa kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko wametangazwa kuwa wenyeheri na Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu. Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa tarehe 17 Aprili 2021 kwenye Abasia ya Casamari. Wenyeheri hawa watakuwa wanakumbukwa na Mama Kanisa kila mwaka tarehe 16 Mei. Mchakato wa kuwatangaza kuwa Wenyeheri ulianza tarehe 27 Juni 2013, kwani hawa ni wale waliouwawa kikatili kutokana na chuki dhidi ya imani “In odium fidei” na kukamilika mwaka 2015 na tarehe 26 Mei 2020 Baba Mtakatifu Francisko akaridhia kwamba, majina yao yaandikwe kwenye kitabu cha Wenyeheri.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 18 Aprili 2021 amewakumbuka, wafuasi hawa wanyenyekevu wa Kristo Yesu. Hawa ndio wale waliouwawa kutokana na chuki dhidi ya imani “In odium fidei”. Wakasimama kidete kulinda Ekaristi Takatifu, kwa ujasiri, kiasi hata cha kupokea kifodini. Askari wale walifanya kufuru dhidi ya Kanisa, Monasteri na walitaka kukufuru pia Ekaristi Takatifu. Ushuhuda wa imani yao, ni changamoto inayowasukuma waamini kuwa waaminifu kwa Mwenyezi Mungu, kiasi hata cha kuweza kuleta mabadiliko katika jamii, ili iweze kusimikwa katika haki na udugu. Kardinali Marcello Semeraro, katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa waamini kutoogopa na kuendelea kumtumainia Mwenyezi Mungu hata pale ambapo wanakabiliana na kifo mbele ya macho yao. Kifodini chao kimekuwa ni sehemu ya furaha na udugu wa Kikristo. Wenyeheri hawa wapya walikuwa na udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu, kiasi kwamba, mwanzoni, walionekana kutaka kukikimbia kifo, lakini kwa ujasiri wakarejea na kusimama imara katika imani, ili kulinda Ekaristi Takatifu.

Ukristo si maisha ya “kudemka”, bali ni sehemu ya mchakato wa mapambano ya maisha ya kiroho. Haya ni mapambano yanayokita mizizi yake katika toba, wongofu wa ndani, sala na matendo ya huruma sanjari na kujiachia katika ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu, Baba mwenye huruma na mapendo. Waamini wakumbuke kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa sana na Mwenyezi Mungu kama ambavyo aliwahi kusema Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na kwamba wao pia wanapaswa kujiaminisha katika upendo wa Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. Utakatifu ni mchakato unaowawezesha waamini kumfungulia Mungu dirisha la maisha yao, ili aweze kuwakirimia nguvu na furaha ya kweli. Ikumbukwe kwamba, Utakatifu ni mwaliko kwa waamini wote na wala si taji kwa watu wachache ndani ya Kanisa na huu ndio ukombozi wa kweli!

Mashuhuda wa Imani
20 April 2021, 15:10