Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mtakatifu Katarina wa Siena alikuwa ni "mwanamke wa shoka" mfano bora wa ufuasi wa kristo Yesu katika toba, wongofu wa ndani na upatanisho unaosimikwa katika tunu msingi za Injili. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mtakatifu Katarina wa Siena alikuwa ni "mwanamke wa shoka" mfano bora wa ufuasi wa kristo Yesu katika toba, wongofu wa ndani na upatanisho unaosimikwa katika tunu msingi za Injili. 

Mt. Katarina wa Siena: Mwanamke wa Shoka, Mfano Bora wa Ufuasi

Mama Kanisa anaadhimisha kumbukumbu ya Miaka 560 tangu Katarina wa Siena alipotangazwa kuwa Mtakatifu. Kwa hakika mtakatifu huyu ni mfano bora wa kuigwa katika ufuasi wa Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha, imani na Injili ili kunogesha mchakato wa utamaduni wa upendo, kielelezo cha imani tendaji na matumaini

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kila mwaka ifikapo tarehe 29 Aprili, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Katarina wa Siena, “Catharina wa Siena” Bikira na Mwalimu wa Kanisa. Katarina kwa lugha ya Kigiriki maana yake ni “Mwanamke asiyekuwa na mawaa”. Huyu alikuwa ni mtawa wa Shirika la Wadominikani, mwanataalimungu mahiri, mwanafalsafa wa kutupwa na mtu aliyekuwa na maono mapana katika maisha. Alifariki dunia kunako tarehe 29 Aprili 1380 akiwa mjini Roma. Papa Pio II akamtangaza kuwa Mtakatifu kunako mwaka 1461. Na ilipogota tarehe 4 Oktoba 1970, Mtakatifu Paulo VI akamtangaza Mtakatifu Katarina wa Siena kuwa ni Mwalimu wa Kanisa. Ilikuwa ni mwaka 1939 Papa Pio XII alipomtangaza kuwa ni Msimamizi wa Italia pamoja na Mtakatifu Francisko wa Assisi. Katika historia na maisha yake, anakumbukwa sana kama mjumbe wa amani, mshauri wa Mababa watakatifu waliolazimika kukimbilia uhamishoni kutokana na misigano ya kisiasa. Alikuwa kweli ni “mwanamke wa shoka, aliyesaidia mchakato wa toba na wongofu wa ndani, unaosimikwa katika Injili ya upendo; amani na upatanisho wa kweli.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Kardinali Augusto Paolo Lojudice, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Siena-Colle Val d'Elsa-Montalcino, amewatakia heri na baraka tele katika maisha na utume wao. Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kulijalia Kanisa, Mwanamke hodari na mwamini mwaminifu, anayewachangamotisha waamini wote kukita maisha yao katika tunu msingi za Kiinjili na kuacha kudema na malimwengu. Mama Kanisa anaadhimisha kumbukumbu ya Miaka 560 tangu Katarina wa Siena alipotangazwa kuwa Mtakatifu. Kwa hakika mtakatifu huyu ni mfano bora wa kuigwa katika ufuasi wa Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha, imani na Injili ili kunogesha mchakato wa utamaduni wa upendo.

Ni Mtakatifu aliyejisadaka kwa ajili ya umoja wa Kanisa, akasali na kujitosa kwa moyo wake wote. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali na kumwomba Mtakatifu Katarina wa Siena ili aweze kuombea umoja wa Kanisa na kuisaidia Italia katika kipindi hiki kigumu cha historia yake, bila kulisahau Bara la Ulaya. Mwishoni, Baba Mtakatifu ametoa baraka zake za kitume, kwa wale wote walioshiriki katika Ibada ya Kumbukumbu ya Mtakatifu Katarina wa Siena, hapo tarehe 29 Aprili 2021.

Katarina wa Siena
30 April 2021, 15:40