Mchango wa Ijumaa Kuu kwa Mwaka 2021: Mchakato wa ujenzi wa mshikamano wa udugu wa upendo kwa kuwawezesha watu wa Mungu wanaoishi kwenye Nchi Takatifu kukabiliana na changamoto za maisha. Mchango wa Ijumaa Kuu kwa Mwaka 2021: Mchakato wa ujenzi wa mshikamano wa udugu wa upendo kwa kuwawezesha watu wa Mungu wanaoishi kwenye Nchi Takatifu kukabiliana na changamoto za maisha. 

Mchango wa Ijumaa Kuu 2021: Ujenzi wa Udugu wa Kibinadamu

Mchango wa Ijumaa Kuu: Kardinali Sandri katika tafakari yake, anachota utajiri na amana kubwa kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Anakazia umuhimu wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu katika masuala ya kidini, kiuchumi, kiekolojia, kisiasa na hata katika mawasiliano ya jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mtakatifu Paulo VI, kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, alitembelea Nchi Takatifu mwezi Januari 1964 na kuguswa na mahitaji ya Wakristo. Katika Wosia wake wa Kitume “Nobis in animo” yaani “Umuhimu wa Kanisa katika Nchi Takatifu” uliochapishwa tarehe 25 Machi 1974, alikazia umoja na mshikamano wa waamini. Huo ukawa ni chimbuko la Sadaka na mchango wa Ijumaa kuu kwa ajili ya Nchi Takatifu: "Pro Terra Sancta".  Mtakatifu Paulo VI alihimiza sana umuhimu wa uwepo endelevu wa Kanisa katika Nchi Takatifu, kama amana na urithi wa imani; ushuhuda endelevu wa Jumuiya ya Wakristo unaoonesha jiografia ya ukombozi. Tangu wakati huo, Kanisa linaendelea kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanaoteseka kunyanyaswa na hata kuuwawa huko Mashariki ya Kati, lakini hasa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Sadaka na mchango wa Ijumaa kuu kutoka kwa Makanisa yote duniani, ni alama ya upendo na mshikamano wa Kanisa kwa watu wa Mungu wanaoishi katika Nchi Takatifu. Huu ni ushuhuda wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika uekumene wa damu, huduma na sala pamoja na kuendeleza majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu katika misingi ya: haki, amani na maridhiano.

Ni kwa njia ya ushuhuda wa umoja, upendo na mshikamano Kanisa linataka kuwajengea waamini na watu wote wenye mapenzi huko Mashariki ya kati Injili ya amani na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi ili kuondokana na: vita, vitendo vya kigaidi, misimamo mikali ya kiimani, dhuluma na nyanyaso kwa misingi ya kidini. Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki katika ujumbe wake kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwa mwaka 2021 anawaalika, Ijumaa kuu kuongozwa na sehemu hii ya Maandiko Matakatifu yasemayo: “Nimesulubiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu”.Gal. 2:20. Mtakatifu Paulo katika sehemu hii ya Maandiko Matakatifu anakazia msingi wa udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika upatanisho, haki na amani, hasa katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Kardinali Leonardo Sandri katika tafakari yake, anachota utajiri na amana kubwa kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Anakazia umuhimu wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu katika masuala ya kidini, kiuchumi, kiekolojia, kisiasa na hata katika mawasiliano ya jamii. Kwa waamini, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu awe ni msingi wa udugu wa kibinadamu unaokita mizizi yake katika zawadi ya upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Lengo liwe ni kufutilia mbali mnyororo wa: vita, chuki, hasira na kinzani za kijamii, ili kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao kwa kutambua kwamba, wote ni wamoja, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kukombolewa na Kristo Yesu. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kwa Nchi Takatifu na Mashariki ya Kati katika ujumla wake, limepelekea majanga makubwa katika maisha ya watu wa Mungu katika eneo hili. Uchumi umeporomoka, watu wengi hawana tena ajira; utu, heshima na haki zao msingi ziko hatarini. Vita isiyokoma na vikwazo vya uchumi Kimataifa ni kati ya mambo yanayoendelea kuwaathiri watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati.

Kardinali Leonardo Sandri anasema, katika Sura ya Pili ya Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti" anazungumzia kuhusu wageni njiani yaani: wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Msamaria mwema anawekwa mbele ya walimwengu kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa maskini. Mchango na sadaka ya Ijumaa kuu ni kwa ajili ya: Utunzaji wa Madhabahu na nyumba za Ibada ni kielelezo cha ukarimu kutoka kwa waamini. Lengo ni kuendelea kutunza maeneo matakatifu ya Fumbo la Umwilisho na Pasaka, mahali ambapo Wakristo wanapata msingi wa utambulisho wao pamoja na maisha bora zaidi. Kwa njia hii, Wakristo katika Nchi Takatifu wameendelea kuonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaotembelea Nchi Takatifu.

Mchango wa Ijumaa Kuu
02 April 2021, 15:07