Siku Mama Dunia Kimataifa Siku Mama Dunia Kimataifa 

Leo ni Siku Mama Dunia Kimataifa,Papa:kuponya uhusiano na uumbaji

“Restore Our Earth” yaani kurudisha Dunia yetu ndiyo kauli mbiu inayoongoza siku ya Mama Dunia Kimataifa ili kuimarisha uhusiano endelevu na kazi ya uumbaji ambayo ndilo lengo la Jumuiya ya kimataifa.Baba Mtakatifu Francisko aliwahimiza wengi kuheshimu maumbile,kwa nyaraka mbili:'Laudato si' na 'Fratelli tutti'.Ujumbe kwa njia ya mtandao amesisitiza uhusiano chanya na Muumba,jirani na kazi ya uumbaji.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Katika muktadha wa siku ya kimataifa ya Dunia mama, Papa Francisko katika ujumbe wake mfupi kwa njia ya mtandao tarehe 22 Aprili 2021 anaandika kuwa: “Tumevunja uhusiano ambao ulikuwa unatuunganisha na Muumba, viumbe wengine na kazi nyingine za uumbaji. Tunahitaji kuponesha huu uhusiano ulioharibiwa ambao ni msingi kwa ajili ya msaada wetu na kiungo kizima cha maisha.  Vile vile ujumbe wa pili unasema utimilifu wa maisha na furaha vinapatikana kwa kujitoa sisi wenyewe kwa ajili ya Injili na kwa ndugu, kwa kujifungua, kukaribisha na kuwa na huruma.

Hata hivyo tukirudi katika muktadha wa Siku ya kimataifa ya Mama dunia ambayo uadhimisha kila ifikapo tarehe 22 Aprili ya kila mwaka ni fursa kubwa ya kuweza kutafakari kwa kina juu ya utegemezi uliopo baina ya watu na viumbe mbalimbali ambavyo vinashirikiana katika dunia hii. Baba Mtakatifu Francisko mara ka mara amekuwa na wasi wasi na zaidi amehimiza zaidi kuheshimu maumbile, kwa nyaraka mbili za kitume :'Laudato si'  inayohusu utunzaji wa bora wa mazingira nyumba yetu ya pamoja  pia 'Fratelli tutti' yaani “Wote ni ndugu”, kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii. Katika mbio za kuelekea utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu ya ajenda ya mwaka 2030, ambayo inauwezo wa kubadili dunia, ni muhimu sana kutazama hali hizi ni miaka 9 tu imebaki ili kutathimini kitu gani kinaendelea katika mama yetu dunia kabla ya malengo hayo.

“Restore our Earth”, yaani “rejesha dunia yetu ndiyo mada inayoongoza Siku hii ya Kimataifa ya dunia mama”. Na wakati huo mgogoro mkubwa wa tabianchi ni kiini cha agenda za sera za kisiasa ulimwengini, japokuwa ni lazima kutazama ikiwa kweli ahadi za wanasiasa zinatafuta matendo ya dhati ili kuondoa madhara makubwa ya dunia hii? Huu ni mwaka wa 51 tangu kuanzishwa kwa siku hii ambapo ilianzishwa mnamo tarehe 22 Aprili 1970. Lakini hata hivyo baada ya miaka yote hiyo bado tunajikuta na tumaini lile lile kwamba Siku ya Mama Dunia inaweza kweli kukugn’utua dhamiri za wote ulimwengu na kuwa ishara mpya uwakilishi wa mapinduzi hasa ya kukabiliana na dharura za majanga ya mazingira yetu ambayo yameharibiwa sana mafuriko, vimbunga, kuongezeka kwa joto, maji ya bahari, ukame, ukataji hovyo wa misitu na moto.

22 April 2021, 15:19