Tafuta

Papa Francisko: Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu, Chombo cha Upatanisho, Umoja na Mshikamano wa Udugu wa kibinadamu. Papa Francisko: Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu, Chombo cha Upatanisho, Umoja na Mshikamano wa Udugu wa kibinadamu. 

Kanisa Sakramenti ya Wokovu, Upatanisho, Umoja na Mshikamano

Ujumbe wa Papa Francisko ni kuhusu: UVIKO-19; Umuhimu wa kushuhudia Ujumbe wa Pasaka na kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya wokovu na ni chombo cha upatanisho, umoja na mshikamano wa Kitaifa. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wa Mungu nchini Brazil ambao wameathirika sana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Umoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Brazi katika mkutano wao wa 58, ulioanza kutimua vumbi tangu tarehe12 hadi 16 Aprili 2021, amegusia kuhusu: janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na madhara yake kwa watu wa Mungu nchini Brazil; Umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Ujumbe wa Pasaka na kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya wokovu na ni chombo cha upatanisho, umoja na mshikamano wa Kitaifa. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wa Mungu nchini Brazil ambao wameathirika sana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Hadi kufikia Alhamisi, tarehe 15 Aprili 2021 watu zaidi ya 13,673,500 (Laki kumi na tatu, mia sita sabini na tatu elfu na mia tano) wameambukizwa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Na watu 361,884 wamekwisha fariki dunia. Watu wengi nchini Brazil wanalia na kuwaombolezea ndugu, jamaa na marafiki waliowatoka, pengine bila hata ya kupata heshima wanayostahili. Kuna wakleri na watawa wengi ambao pia wamepoteza maisha yao, kwani hili ni gonjwa lisilobagua wala kuchagua! Wote hawa, Baba Mtakatifu anawaombea ili wapate rehema kwa Mungu wapumzike kwa amani. Mwenyezi Mungu awafariji wale wote walioguswa na misiba ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Baba Mtakatifu anawahimiza Maaskofu Katoliki Brazil kutangaza na kushuhudia ushindi wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu, chemchemi inayopyaisha matumaini. Kristo Yesu amefufuka kweli kweli na ameshinda dhambi na mauti. Hiki ni kipindi cha kupyaisha matumaini, ili Injili ya uhai iweze kusonga mbele. Imani iwasaidie waamini kuvuka kipindi hiki kigumu katika historia na maisha ya watu wa Mungu nchini Brazil. Matumaini kwa Kristo Mfufuka yawapatie fursa ya kusimama tena na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Upendo wa Kikristo unawabidiisha kuomboleza na wale wanaolia na kuwaombolezea ndugu, jamaa na marafiki zao. Huu ni mwaliko wa kuonesha mshikamano wa kidugu kwa kuwasaidia maskini na waathirika zaidi, ili hata wao pia waweze kutabasamu tena. Maaskofu wawe mstari wa mbele, kujisadaka bila ya kujibakiza hata kidogo kwa ajili ya kuonesha mshikamano wa huruma na upendo wa kibinadamu.

Yote haya yanawezekana ikiwa kama Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil litakuwa limeunganika. Baba Mtakatifu bado anakumbuka hija yake ya kitume ya mwaka 2013 aliyoifanya nchini Brazil. Bikira Maria, Mama Yetu wa Aparecida, awe ni kiungo cha umoja na mshikamano wa watu wa Mungu nchini Brazil. Kanisa ni Sakramenti ya wokovu na chombo cha amani, maridhiano na upatanisho wa Kitaifa. Kwa njia ya upatanisho, Kanisa linaweza kuwa ni chombo pia cha umoja wa Kitaifa, dhamana na wajibu wa Kanisa nchini Brazil. Kanisa lijitahidi kujenga mazingira na utamaduni wa watu kukutana katika medani mbalimbali za maisha, ili kupambana na “Virusi vya kinzani, utengano na mipasuko ya kijamii na kisiasa”. Hivi ni virusi ambavyo vinaibuliwa na ubinafsi na hivyo kuwa ni chanzo cha ukosefu wa haki jamii. Watu wa Mungu nchini Brazil katika mapambano haya, watambue kwamba, Kristo Yesu Mfufuka yuko pamoja nao na kwamba, wamwendee na kumkimbilia Kristo Yesu, kielelezo cha nguvu na umoja wao!

Ni nia na sala ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Mkutano mkuu wa 18 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, utaweza kuzaa matunda ya umoja na upatanisho wa Kitaifa, licha ya tofauti zao msingi. Bikira Maria wa Aparecida awaombee watoto wake, ili waweze kuwa ni walinzi wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, tayari kusimama kidete kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Waamini wawe ni waragibishaji wa udugu wa kibinadamu nchini Brazil.

Papa Brazil

 

 

 

 

16 April 2021, 07:10